Friday, November 29, 2013

Jeshi  la Polisi Makao Makuu  jana lilimhoji na kumuachia bila masharti Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)  Wilaya ya Kinondoni na Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Henry Kileo, kwa tuhuma za kumtishia maisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe. Kileo ambaye aliongozana na wanasheria wawili, walifika makao makuu ya jeshi hilo saa 6:30 mchana, lakini walizuiwa kuingia katika mahojiano kwa muda wakitakiwa kupunguza idadi ya watu waliotakiwa kushiriki katika mahojiano hayo.

Kileo alitaka kuingia na wanasheria wake wawili, pamoja na wawakilishi wawili wa Chadema ambao alikuwa ameongozana nao, lakini alizuiliwa na kutakiwa kuingia na mwanasheria mmoja tu, jambo lililozua mabishano kati yao na askari waliokuwa mapokezi.
Baadaye Kileo alikubaliwa kuingia na wanasheria wawili badala ya mmoja, lakini wawakilishi wa chama walikataliwa.
Pia, waandishi wa habari waliokuwa wakipiga picha baada ya Kileo kuwasili eneo hilo, walizuiwa na kufukuzwa hadi nje ya jengo hilo kwa maelezo kuwa hakukuwa na taarifa za kutakiwa kuwapo katika ofisi hizo.
Licha kukubali kutoka nje ya jengo, lakini  waliendelea kufukuzwa kwa madai ya kuwa hawakutakiwa kuonekana wamesimama nje ya jengo hilo. Hata hivyo, waandishi waliendelea kusimama  mpaka mahojiano yalipomalizika.
Akizungumza na waandishi wa habari  baada ya kutoka katika mahojiano hayo ambayo yalidumu kwa takribani saa 1:30, mwakilishi wa Mwanasheria wa Kileo, Musa Mfinanga, alisema waliambiwa kuwa zipo tuhuma za kumtishia maisha Zitto na Kileo anahusishwa.
Mfinanga alisema kwa mujibu wa maelezo ya polisi, tuhuma hizo zilitolewa katika gazeti moja la kila siku (Siyo NIPASHE) la Novemba 11, mwaka huu.
“Kileo ameitwa hapa kuhojiwa kwa madai kuwa anatuhumiwa kumtishia maisha Zitto Kabwe, tuhuma ambazo polisi wanadai zilitolewa kupitia gazeti. Na polisi wanadai tayari wameshamhoji Zitto kuhusiana na tuhuma hizo,” alisema na kuogeza:
“Sisi tumetoa maelezo yetu na baada ya kumaliza kutoa maelezo hayo,  wakamuachia  Kileo bila masharti yoyote.”
Naye Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, alisema kabla ya kuanza mahojiano kulikuwa na mabishano ambayo yalidumu kwa takribani saa moja, baada ya kutakiwa kujaza fomu ya maonyo, pasipo kujua sababu ya Kileo kuitwa na kuhojiwa  na jeshi hilo.
Alisema polisi walitaka kumhoji Kileo kama mtuhumiwa wakati hakutumiwa samansi kuonyesha anatuhumiwa badala yake alimpigiwa simu, jambo ambalo hawakubaliani nalo.
“Unapomtuhumu mtu ni lazima umpe samansi, lakini hawakufanya hivyo, walimuita kwa simu tu,  pili, walitaka ajaze fomu namba mbili ambayo ni fomu ya onyo,” alisema na kuongeza:
“Kwa hiyo ikatuchukua muda mrefu kwa sababu ilibidi tuwaeleweshe taratibu za kisheria.”
Mallya alisema: “ Tulikubali kufanya mahojiano baada ya polisi kubadilisha kauli, kwamba wanafanya mahojiano hayo kama sehemu ya kuchukua maelezo yake.”


Kwa upande wake, Kileo alisema anaamini hizo ni propaganda za kisiasa ambazo Jeshi la Polisi halikupaswa  kuzifuatilia. 


Alisema ni jambo la kusikitisha kuona jeshi hilo linaacha kushughulikia masuala ya msingi na kujihusisha na propaganda za kisiasa.
Pia aliongeza kuwa ni mbinu za Jeshi hilo kufifisha na kuwasahaulisha wananchi wasiendelee kufuatilia masuala ya msingi ambayo yanaendelea hivi sasa.
“Nimekuwa surprised (nimeshangazwa) sana kuona Jeshi la Polisi linaacha kufuatilia mambo ya msingi na kuendekeza propaganda za kisiasa, Zitto ni nani hata nimtishie kumuua?” alihoji na kuongeza:
“Wapo watanzania wengi ambao wametishiwa kuuawa wakiwamo waandishi wa habari, kina Dk. Stephen Ulimboka  na wengine wengi ambao mpaka sasa Jeshi la Polisi halijachukua hatua zozote,” alisema Kileo.
 “Eti leo hii linafanya kazi yake kupitia taarifa ya kwenye gazeti wakati wapo watu ambao walihusishwa kabisa kwenye matukio ya kihalifu,  lakini polisi wamenyamaza,” alisema.
Kileo alisema ni vema Jeshi la Polisi likaacha kuingia katika propaganda za kisiasa kwa ajili ya kuwasahaulisha wananchi juu ya masuala ya msingi, badala yake liwaeleze juu ya kinachoendelea kuhusu matukio ya kutisha ambayo wamefanyiwa  baadhi ya waandishi wa habari,  Dk. Ulimboka, Dk. Sengondo Mvungi na Watanzania wengine.
IRINGA WANENA
Katika hatua nyingine, Chadema katika mikoa ya Iringa na Tanga kimeunga mkono hatua ya Kamati Kuu kuwavua nafasi za uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto na wenzake.
Zitto alivuliwa uongozi Ijumaa iliyopita sambamba na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kwa tuhuma za kukisaliti chama.
Wote wanatuhumiwa kuandaa waraka ambao ulikuwa na tuhuma dhidi ya chama na viongozi wake ngazi ya taifa.
Chadema mkoa wa Iringa kimesema hatua zilizochukuliwa na Kamati Kuu dhidi ya viongozi hao ni sahihi.
Mjumbe wa Kamati ya Uendaji wa Chadema Nyanda za Juu Kusini, Abdu Changawe, aliwaambia waandishi wa habari mjini Iringa jana kuwa chama hicho kinaongozwa na katiba na kama mtu yeyote atakayehusika kutoiheshimu katiba hiyo, lazima katiba itamshughulikia kikamilifu.
“Kutokana na tabia zao za usaliti ndani ya chama sisi kama wanachama wa Chadema Iringa tunapongeza maamuzi yote na pia tunatoa msimamo wetu kuwa yeyote aliye na tabia kama hiyo ajirekebishe haraka kabla sheria haijachukua mkondo wake,”alisema Changawe.
Aidha, alisema kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha kuwa haki inatendeka sehemu zote na pia wamejipanga kuwa tayari kutokumbatia uovu wa aina yoyote kwani mafanikio ya chama mpaka sasa yamegarimu damu za watu, mali za watu na hata wengine kufungwa magerezani.
TANGA WAKANA UASI
Kwa upande wake, Chadema Mkoa wa Tanga kimekemea viongozi waliyoibuka kupinga maamuzi ya Kamati kuu ya kuwavua nyadhifa Zitto na wenzake na kwamba kitendo hicho ni kinyume cha Katiba  ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Chadema Mkoa wa Tanga, Jonathan Bahweje, alikemea viongozi hao kuwa wanakiuka katiba kifungu cha saba ibara ya saba na 16 (V) inayoipa mamlaka na uwezo Kamati Kuu  ya kuteua na kumuondoa mtu yeyote atakaebainika kwenda kinyume cha katiba.
Bahweje alieleza kuwa viongozi hao wanatenda kosa la kikatiba na kwamba hawana haki ya kuhoji wala kukosoa kilichotendeka kwa kuwa wao ni ngazi za chini, hivyo hawawezi kutengua maamuzi ya chombo kilichopo juu yao.
CHASO YAONYA
Shirikisho la Wanachama wa Chadema Vyuo Vikuu (Chaso) Mkoa wa Dar es Salaam, limesema watu wanaojitokeza hivi sasa na kutoa matamko yanayopinga uamuzi wa kumvua Zitto na wenzake nafasi za uongozi wanatumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mratibu Mkuu wa Chaso, Elihuruma Jackson Himida, alisema hayo jana alipozungumza na NIPASHE na kusema katika kutekeleza mbinu zao alizoziita ‘chafu’, watu hao wamekuwa wakijitambulisha kuwa ni wanachama wa Chadema wakati siyo kweli.
Alisema Chaso itatoa majibu leo kuhusiana na matamko yanayoendelea kutolewa na watu hao ili Watanzania wajue ukweli halisi wa kile kinachoendelea juu yao.
Alisema uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Sekretarieti ya Chaso, kilichofanyika jana kujadili watu hao, ambao alisema hawamo hata kwenye kumbukumbu za Chadema kuwa ni wanachama wake, lakini wanashangazwa kuona waandishi wa habari wakiwashabikia.
Kauli hiyo ya Elihuruma imetolewa siku moja baada ya juzi watu waliojitambulisha kuwa ni wanachama wa Chadema, wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kile walichokiita mgogoro wa kiutawala kati ya wapigania demokrasia na wahafidhina ndani ya chama hicho.
MJUMBE APINGA KAMATI KUU
Pia jana Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema Taifa, Joseph Patrick, naye aliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alipinga uamuzi uliofanywa na CC dhidi ya Zitto na Dk. Kitila na kusambazwa kwa waraka uliowaponza, akisema unakidhalilisha chama.
SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment