IGP |
Jeshi la
Polisi Makao Makuu jana lilimhoji na kumuachia bila masharti Katibu wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Kinondoni na
Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Henry Kileo, kwa tuhuma za kumtishia
maisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe. Kileo
ambaye aliongozana na wanasheria wawili, walifika makao makuu ya jeshi
hilo saa 6:30 mchana, lakini walizuiwa kuingia katika mahojiano kwa muda
wakitakiwa kupunguza idadi ya watu waliotakiwa kushiriki katika
mahojiano hayo.
Kileo
alitaka kuingia na wanasheria wake wawili, pamoja na wawakilishi wawili
wa Chadema ambao alikuwa ameongozana nao, lakini alizuiliwa na kutakiwa
kuingia na mwanasheria mmoja tu, jambo lililozua mabishano kati yao na
askari waliokuwa mapokezi.
Baadaye Kileo alikubaliwa kuingia na wanasheria wawili badala ya mmoja, lakini wawakilishi wa chama walikataliwa.
Pia, waandishi wa habari waliokuwa wakipiga picha baada ya Kileo
kuwasili eneo hilo, walizuiwa na kufukuzwa hadi nje ya jengo hilo kwa
maelezo kuwa hakukuwa na taarifa za kutakiwa kuwapo katika ofisi hizo.
Licha kukubali kutoka nje ya jengo, lakini waliendelea kufukuzwa kwa
madai ya kuwa hawakutakiwa kuonekana wamesimama nje ya jengo hilo. Hata
hivyo, waandishi waliendelea kusimama mpaka mahojiano yalipomalizika.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka katika mahojiano
hayo ambayo yalidumu kwa takribani saa 1:30, mwakilishi wa Mwanasheria
wa Kileo, Musa Mfinanga, alisema waliambiwa kuwa zipo tuhuma za
kumtishia maisha Zitto na Kileo anahusishwa.
Mfinanga alisema kwa mujibu wa maelezo ya polisi, tuhuma hizo zilitolewa
katika gazeti moja la kila siku (Siyo NIPASHE) la Novemba 11, mwaka
huu.
“Kileo ameitwa hapa kuhojiwa kwa madai kuwa anatuhumiwa kumtishia maisha
Zitto Kabwe, tuhuma ambazo polisi wanadai zilitolewa kupitia gazeti. Na
polisi wanadai tayari wameshamhoji Zitto kuhusiana na tuhuma hizo,”
alisema na kuogeza:
“Sisi tumetoa maelezo yetu na baada ya kumaliza kutoa maelezo hayo, wakamuachia Kileo bila masharti yoyote.”
Naye Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, alisema kabla ya kuanza
mahojiano kulikuwa na mabishano ambayo yalidumu kwa takribani saa moja,
baada ya kutakiwa kujaza fomu ya maonyo, pasipo kujua sababu ya Kileo
kuitwa na kuhojiwa na jeshi hilo.
Alisema polisi walitaka kumhoji Kileo kama mtuhumiwa wakati hakutumiwa
samansi kuonyesha anatuhumiwa badala yake alimpigiwa simu, jambo ambalo
hawakubaliani nalo.
“Unapomtuhumu mtu ni lazima umpe samansi, lakini hawakufanya hivyo,
walimuita kwa simu tu, pili, walitaka ajaze fomu namba mbili ambayo ni
fomu ya onyo,” alisema na kuongeza:
“Kwa hiyo ikatuchukua muda mrefu kwa sababu ilibidi tuwaeleweshe taratibu za kisheria.”
Mallya alisema: “ Tulikubali kufanya mahojiano baada ya polisi
kubadilisha kauli, kwamba wanafanya mahojiano hayo kama sehemu ya
kuchukua maelezo yake.”
Kwa upande wake, Kileo alisema anaamini hizo ni propaganda za kisiasa ambazo Jeshi la Polisi halikupaswa kuzifuatilia.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona jeshi hilo linaacha kushughulikia
masuala ya msingi na kujihusisha na propaganda za kisiasa.
Pia aliongeza kuwa ni mbinu za Jeshi hilo kufifisha na kuwasahaulisha
wananchi wasiendelee kufuatilia masuala ya msingi ambayo yanaendelea
hivi sasa.
“Nimekuwa surprised (nimeshangazwa) sana kuona Jeshi la Polisi linaacha
kufuatilia mambo ya msingi na kuendekeza propaganda za kisiasa, Zitto ni
nani hata nimtishie kumuua?” alihoji na kuongeza:
“Wapo watanzania wengi ambao wametishiwa kuuawa wakiwamo waandishi wa
habari, kina Dk. Stephen Ulimboka na wengine wengi ambao mpaka sasa
Jeshi la Polisi halijachukua hatua zozote,” alisema Kileo.
“Eti leo hii linafanya kazi yake kupitia taarifa ya kwenye gazeti
wakati wapo watu ambao walihusishwa kabisa kwenye matukio ya kihalifu,
lakini polisi wamenyamaza,” alisema.
Kileo alisema ni vema Jeshi la Polisi likaacha kuingia katika propaganda
za kisiasa kwa ajili ya kuwasahaulisha wananchi juu ya masuala ya
msingi, badala yake liwaeleze juu ya kinachoendelea kuhusu matukio ya
kutisha ambayo wamefanyiwa baadhi ya waandishi wa habari, Dk.
Ulimboka, Dk. Sengondo Mvungi na Watanzania wengine.
IRINGA WANENA
Katika hatua nyingine, Chadema katika mikoa ya Iringa na Tanga kimeunga
mkono hatua ya Kamati Kuu kuwavua nafasi za uongozi aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu, Zitto na wenzake.
Zitto alivuliwa uongozi Ijumaa iliyopita sambamba na aliyekuwa mjumbe wa
Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa
wa Arusha, Samson Mwigamba, kwa tuhuma za kukisaliti chama.
Wote wanatuhumiwa kuandaa waraka ambao ulikuwa na tuhuma dhidi ya chama na viongozi wake ngazi ya taifa.
Chadema mkoa wa Iringa kimesema hatua zilizochukuliwa na Kamati Kuu dhidi ya viongozi hao ni sahihi.
Mjumbe wa Kamati ya Uendaji wa Chadema Nyanda za Juu Kusini, Abdu
Changawe, aliwaambia waandishi wa habari mjini Iringa jana kuwa chama
hicho kinaongozwa na katiba na kama mtu yeyote atakayehusika
kutoiheshimu katiba hiyo, lazima katiba itamshughulikia kikamilifu.
“Kutokana na tabia zao za usaliti ndani ya chama sisi kama wanachama wa
Chadema Iringa tunapongeza maamuzi yote na pia tunatoa msimamo wetu kuwa
yeyote aliye na tabia kama hiyo ajirekebishe haraka kabla sheria
haijachukua mkondo wake,”alisema Changawe.
Aidha, alisema kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha kuwa haki
inatendeka sehemu zote na pia wamejipanga kuwa tayari kutokumbatia uovu
wa aina yoyote kwani mafanikio ya chama mpaka sasa yamegarimu damu za
watu, mali za watu na hata wengine kufungwa magerezani.
TANGA WAKANA UASI
Kwa upande wake, Chadema Mkoa wa Tanga kimekemea viongozi waliyoibuka
kupinga maamuzi ya Kamati kuu ya kuwavua nyadhifa Zitto na wenzake na
kwamba kitendo hicho ni kinyume cha Katiba ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Chadema Mkoa wa
Tanga, Jonathan Bahweje, alikemea viongozi hao kuwa wanakiuka katiba
kifungu cha saba ibara ya saba na 16 (V) inayoipa mamlaka na uwezo
Kamati Kuu ya kuteua na kumuondoa mtu yeyote atakaebainika kwenda
kinyume cha katiba.
Bahweje alieleza kuwa viongozi hao wanatenda kosa la kikatiba na kwamba
hawana haki ya kuhoji wala kukosoa kilichotendeka kwa kuwa wao ni ngazi
za chini, hivyo hawawezi kutengua maamuzi ya chombo kilichopo juu yao.
CHASO YAONYA
Shirikisho la Wanachama wa Chadema Vyuo Vikuu (Chaso) Mkoa wa Dar es
Salaam, limesema watu wanaojitokeza hivi sasa na kutoa matamko
yanayopinga uamuzi wa kumvua Zitto na wenzake nafasi za uongozi
wanatumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mratibu Mkuu wa Chaso, Elihuruma Jackson Himida, alisema hayo jana
alipozungumza na NIPASHE na kusema katika kutekeleza mbinu zao
alizoziita ‘chafu’, watu hao wamekuwa wakijitambulisha kuwa ni wanachama
wa Chadema wakati siyo kweli.
Alisema Chaso itatoa majibu leo kuhusiana na matamko yanayoendelea
kutolewa na watu hao ili Watanzania wajue ukweli halisi wa kile
kinachoendelea juu yao.
Alisema uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Sekretarieti ya Chaso,
kilichofanyika jana kujadili watu hao, ambao alisema hawamo hata kwenye
kumbukumbu za Chadema kuwa ni wanachama wake, lakini wanashangazwa kuona
waandishi wa habari wakiwashabikia.
Kauli hiyo ya Elihuruma imetolewa siku moja baada ya juzi watu
waliojitambulisha kuwa ni wanachama wa Chadema, wakiwamo wanafunzi wa
vyuo vikuu kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kile
walichokiita mgogoro wa kiutawala kati ya wapigania demokrasia na
wahafidhina ndani ya chama hicho.
MJUMBE APINGA KAMATI KUU
Pia jana Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema Taifa, Joseph Patrick, naye
aliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alipinga
uamuzi uliofanywa na CC dhidi ya Zitto na Dk. Kitila na kusambazwa kwa
waraka uliowaponza, akisema unakidhalilisha chama.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment