Kwa mara nyingine katika kipindi
kisichozidi wiki mbili, polisi nchini Tanzania wamenasa shehena kubwa
ya meno ya tembo yakiwa yamefichwa katika kontena, bandarini Zanzibar.
Watu wawili wamekamatwa wakihusishwa na meno hayo.Kamishna Mussa amesema, kwa sasa kiasi hicho cha meno ya tembo bado hakijafahamika kutokana na kuendelea kwa kazi ya kupakua kutoka kontena hilo.
Hivi karibuni raia watatu wa China walikamatwa nchini Tanzania kwa kukutwa na meno 706 ya tembo, sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini humo.
Kukamatwa kwa meno haya ya tembo, kumekuja wakati tayari serikali imetangaza kusitisha Operesheni Tokomeza Ujangili, ambayo ililenga kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka kutokana na kuuawa katika hifadhi za taifa nchini Tanzania. Wanyama wanaolengwa zaidi na majangili kutokana na meno yao na pembe ni tembo na faru.
Matukio ya kukamatwa kwa meno ya tembo kutoka Afrika Mashariki yamekuwa yakiripotiwa kila mara. Oktoba, 20, 2012, tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya dola milioni 3.4 za Kimarekani yalikamatwa Hong Kong, yakidaiwa kusafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.
Pia Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa Vietnam akiwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 18 sawa na dola zaidi ya elfu 11, yakisafirishwa kwenda nje.
No comments:
Post a Comment