Dar es Salaam. Vita vya maneno kati ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe imefika pabaya.
Vita hiyo ya maneno iliyoanzishwa na Lema katika
kikao cha wabunge wiki iliyopita kwamba Zitto anafanya unafiki kukataa
posho, jana iliingia katika hatua nyingine baada ya mwakilishi huyo wa
Arusha kumshushia tuhuma Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba anakataa
posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika
mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii
Forum huku akisema kuwa, suala hilo halihitaji vikao vya chama
kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususani mitandao ya kijamii
kwani hata Zitto hutumia mitandao hiyo.
Katika hoja yake, Lema alisema kuwa Zitto ambaye
ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
anakataa posho ya Sh70,000 kwa kikao kimoja cha Bunge, lakini anapokea
Sh700,000 mpaka Sh1,000,000 kwa kikao kimoja cha kamati yake na haswa
vile vinavyoandaliwa na mifuko ya jamii.
Hata hivyo, zitto alikanusha shutuma hizo akimtaka
Lema kutoa ushahidi kama kuna mjumbe yoyote wa kamati ya PAC anayepokea
posho, huku akieleza kuwa hawezi kubishana na Mbunge huyo wa Arusha
mjini kwani yeye Zitto ni kiongozi wake ndani ya Chadema.
“Naomba kutaja masilahi yangu katika hili, wabunge
wa kawaida wakialikwa katika vikao hivyo huwa wanalipwa Sh500,000 kwa
kikao kwa siku . Mimi nimewahi kuhudhuria vikao hivyo mara mbili na
nikalipwa hivyo pamoja na chai na chakula cha mchana.” alisema Lema.
Lema alisema posho hizo za wabunge ni tofauti na
zile za Mwenyekiti wa PAC kwani yeye pamoja na posho ya Sh700,000 mpaka
Sh1,000,000 hupewa mafuta ya gari au tiketi ya ndege ya kumtoa alipo na
kumrudisha na kukodiwa hoteli yenye hadhi ya nyota nne mpaka tano ambayo
kwa siku gharama yake ni Dola za Marekani 100 mpaka 600 kwa siku .
Akijibu hoja hizo, Zitto alisema tangu siku nyingi
alikwisha piga marufuku kwa PAC kupokea posho kutoka taasisi au
mashirika yanayosimamiwa na kamati hiyo.
“Toka nimekuwa Mwenyekiti wa POAC (Kamati ya
Hesabu za Mashirika ya Umma) sio tu nilipiga marufuku posho bali pia
niliwashitaki PCCB (Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa) wabunge
wanaochukua posho kutoka kwa taasisi za Serikali,” alisema Zitto.
Alieleza baada ya hatua hiyo, wabunge walihojiwa
na PCCB kuhusu jambo hilo mpaka aliyekuwa Spika wa Bunge wakati huo,
Samuel Sitta alipoingilia kati na kuwatetea wabunge hao.
“Hiyo ilikuwa mwaka 2009 kabla hata Lema hajawa
mbunge, wajumbe wa kamati ya PAC wanalipwa posho za vikao kama wabunge
wengine, lakini mimi sichukui posho hizo za vikao,” alisema na
kuongeza:.
“Sio tu PAC hata kwenye Baraza la Madiwani na
Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Kigoma na popote kule. Hata NGO
(Mashirika yasiyo ya Kiserikali) zikinialika kwenye vikao vyao sichukui
posho za vikao. Nafasi yoyote ninayoalikwa kama mbunge sichukui posho za
vikao,” alisema Zitto.
No comments:
Post a Comment