Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz (49), ametajwa kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania kwa sasa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jarida la
Marekani la Forbes na kutoa taarifa yake juzi, Rostam amekamata nafasi
hiyo na ya 27 katika Afrika akiwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni
moja (Sh1.6 trilioni).
Mbunge huyo wa zamani wa Igunga, ameingia kwa mara
ya kwanza katika orodha ya matajiri 50 wa Afrika ya jarida hilo, pamoja
na wafanyabiashara wengine wa Tanzania, Reginald Mengi na Mbunge wa
Singida Mjini (CCM), Mohamed Dewji ‘Mo’. Katika orodha hiyo pia yumo
Said Bakhresa ambaye aliwahi kutajwa siku za nyuma.
Rostam, ambaye aliachana na siasa mwaka 2011,
amempiku Bakhresa, ambaye mwaka jana Jarida la Ventures Africa la
Nigeria lilimtaja kuwa ndiye aliyekuwa tajiri namba moja wa Tanzania.
Bakhressa katika kipindi hicho alikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 620
milioni (Sh971 bilioni).
Katika orodha hiyo ya Ventures Africa, Bakhresa alifuatiwa na Rostam, Mengi na mfanyabiashara mwingine maarufu, Ali Mufuruki.
Mengi anashika nafasi ya pili kwa Tanzania na ya 34 Afrika akiwa na utajiri wa Dola 550 milioni (Sh861 bilioni).
Forbes linaonyesha kuwa Bakhresa amefungana na Mo
katika nafasi ya tatu ya orodha ya matajiri wa Tanzania na ya 38 kwa
Afrika, wote wakiwa na utajiri wa Dola 500 milioni (Sh783 bilioni).
Rostam, Mengi na Bakhresa hawakupatikana jana
kuzungumzia suala hilo huku Mo akisema kwamba asingeweza kuzungumzia
suala hilo kwa kuwa jana alikuwa katika mapumziko ya Sikukuu ya Ashura.
Tajiri wa Nigeria, Aliko Dangote, ambaye anajenga
Kiwanda cha Saruji huko Mtwara ndiye anayeshika nafasi ya kwanza katika
orodha ya Afrika, akiwa na utajiri wa Dola20 bilioni (Sh31.7 trilioni),
akifuatiwa na familia ya Johanny Rupert ya Afrika Kusini yenye utajiri
wa Dola7 bilioni (Sh10.7 trilioni) na Nick Oppenheimer, pia wa Afrika
Kusini mwenye utajiri wa Dola 6.6 bilioni (Sh10.3 trilioni).
No comments:
Post a Comment