Uchambuzi wa dr. Lwaitama kuhusu sakata la zitto na maamuzi ya kamati kuu ya chadema onday, November 25, 2013
Lwaitama: CCM, CHADEMA na 'Umoja ni Ushindi'
Asante ... kwa uchambuzi wenye tafakuri tunduizi. Nitajaribu baadaye
kufuata nyazo zako. Lakini kitu kimoja kiko wazi. Chadema kama taasisi
imechukua uamuzi sahihi. Kaulimbiu ya CCM ya tangu Aprili 2012 ni eti
"Umoja ni Ushindi" hivyo malumbano ya kutuhumiana ufisadi na ugamba
yanabomoa umoja na kupunguza uwezekano wa ushindi kwa hiyo lazima
kuwavumilia viongozi wandamizi walio na nguvu ndani ya CCM vile kuwavua
vyeo vyao katika chama kutatufanya tushindwe kushinda katika chaguzi.
Chadema imetekeleza kaulimbiu mbadala na kusema; hapana, viongozi
wandamizi wanaocheza karata nje ya uwanja na kuandamwa na tuhuma za
usaliti tutathubutu kuwavua uongozi hata kama hilo litayumbisha chama
kwa muda kwa sababu ya umaarufu wao au kuwa kwao na uwezo mkubwa wa
uchambuzi wa mambo hautakizua chama kama taasisi kuwavua vyeo au hata
kuwafukuza uanachama.
Mfano wa Dakta Salim Ahmed Salim ni
muafaka hapa. Alipigwa vita na kutuhumiwa hata mauaji ya mwaasisi wa
Zanzibar ya baada ya Mapinduzi lakini hata baada ya kuzushiwa mambo
mengi ya hovyo na mwisho wa siku CCM kikashinda uchaguzi 2005 bendera
yake ikipeperushwa na mgombea ambaye hakuwa na sifa za uadilifu na
umahiri wa uchambuzi wa masuala ya kitaifa na kimataifa wa kulingana na
wa Dakta Salim Ahmed Salim . Lakini vile yeye ni mwenye hulka ya
unyenyekevu na kutojiona bora kuliko wenzake na kutotawaliwa na dhana ya
kuwa bila yeye kuwa Rais basi hakuna la maana chama chake kingeweza
kikafanya, aliendelea kuwa mwanachama wa CCM na mwaka 2010 alijitokeza
kumpigia kampeni ya urais kipindi cha pili mgombea ambaye mtandao
ulimbeba 2005.
Bila shaka mgombea wa urais wa CCM wa 2005 na
2010 alinufaika na kuchafuliwa kisiasa kwa Dakta Salim. Labda tofauti ya
wale waliovuliwa uongozi na Chadema na Dakta Salim Ahmed Salim ni wao
kutokuwa na nidhamu ya kichama cha ukombozi ambayo inadai kuwa au
ujiondoe kama hujaridhika na uongozi uliopo au ukibaki basi uwe tayari
kuvumilia kuchafuliwa na wale wasio na uwezo wa kiakili kama wewe pale
unapotaka kuwaondoa madarakani tena kwa kucheza nje ya uwanja wa mchezo
wa siasa unaofuata sheria zinazotungwa na wale wale ambao kwa wakati huo
ndio wenye uwingi wa kura katika vikao halali za chama husika.
Vinginevyo wewe utakuwa unakisaidia chama tawala cha CCM kwa kuanzisha
zogo kuhusu eti mapungufu ya viongozi waliopo kwa kujiaminisha kuwa wewe
ni bora kuliko wao ambapo na wao wanajiona ni bora kuliko wewe. Kwani
Kambona si alikuwa kiongozi mahiri na mwenye maono kuliko hata wazee
wetu kama Mzee Kawawa? Lakini historia ya TANU ikiandikwa yeye
ataonekana msaliti na Mzee Kawawa ataonekana shujaa, siyo? Kwani Rais
Reagan na Rais George Bush ndio walikuwa wenye akili na umahiri kuliko
viongozi wa Republican Party ya enzi zao au ndio walikuwa muafaka
kuongoza ili kuleta umoja ndani ya chama?
Alipokufa Dakta
Mondlane ni kwa nini wasomi kama Marcelino dos Santos walimpisha Samora
Machel kuongoza Frelimo kama si kutii dhana ya nidhamu ya juu ndani ya
chama cha ukombozi kuzuia kuanzisha migogoro inayowasaidia watawala wa
wakati huo kujinadi kama wenye utulivu na hivyo kutokuwepo na mbadala.
Kwa nini hadi leo Malkia wa Uingereza ni mama Elizabeth badala ya Prince
Charles? hivi kuongoza taasisi lazima aliyeonekana anafaa lazima awe
mwenye akili au umahiri wa uchambuzi wa mambo kuliko wenzake?
Kuanzisha mtandao wa siri wenye lengo la kubadili uongozi wa juu wa
chama cha ukombozi ni usaliti na anayeandaa mkakati huo wa siri hawezi
kujinadi kama eti mwanademokrasia, yeye ni mwanamakundi ya siri siri
ndani ya chama husika kama hao anaowatuhumu yeye kuwa na makundi yao
yakuwadumisha kwenye uongozi. Haiwezekani kusema ni sawa kutumia mbinu
za kisirisiri nje ya utaratibu uliopo halafu ukajinadi kuwa mtetezi wa
demokrasia na wenzako eti wahafidhina.
Ningewaelewa hawa
waliovuliwa uongozi kama wangejenga hoja hiyo ndani ya chama chao kwa
uwazi kabisa na hoja hiyo ikikosa kupata kuungwa mkono basi wangetulia
na kujaribu tena na tena hadi hoja yao ipate kuungwa mkono na wajumbe
wengi wa vikao husika vya chama chao. Vinginevyo wangejitoa uanachama wa
chama husika. Hivyo ndivyo mwanademokrasia anavyotarajiwa kufanya. Mimi
nilijitoa TANU tangu 1973 na sijarudi CCM hadi leo vile najua hoja
zangu zitakuwa na uungwaji mkono finyu kwa sasa katika vyombo vya
maamuzi, labda pale CCM kikiondolewa madarakani kikabaki na waumini wa
kweli wa ujamaa na umajumui wa kiafrika.
Kama wewe ni akina
Abdul Nasser anayepanga mapinduzi ya kutumia nguvu kisisiri basi sema
hivyo nayo inaitaji ujipange kufanikisha hilo wakati muafaka na
ukishindwa katika mipango yako kubali kushindwa na anzisha chama chako
au kama Ndugu yangu Mabere Marando jiunge na chama unachokubaliana nacho
zaidi ya hicho ulimo.
Haiwezekani eti chama cha maana kiogope
kuondoka kwa wanachama wafuasi wa mwanachama au kiongozi mmoja au
wawili au watatu wanaojiona wao ni bora kuliko wenzao. Kwa kitendo cha
Chadema kuwavua uanachama viongozi wao wanadamizi wanaokiri tena na tena
kuwa walisuka mtandao wa siri wa kuwaondoa katika chaguzi zijazo
viongozi wenzao wanaowaona wao kuwa ni wahafidhina na wao ni
wanademokrasia ni kitendo cha ujasiri na kujenga uhalali wa kudumu wa
Chadema hata kama kitayumba na kutorokwa na wanachama kiasi kidogo au
kikubwa kwa sasa na hata kukosa ushindi kwenye changuzi za wakati huo.
Uchambuzi wenye kusukumwa na tafakuri tunduizi unanituma niseme heko
Chadema kwa kuthubutu hata kama chama kitashindwa katika uchaguzi wowote
ujao. Kitendo hiki pekee kimeonesha njia kwa kusema kuwa dhana ya
"Umoja ni Ushindi" ni dhana bora kuacha itekelezwe na CCM ya mafisadi
ambao kwao kuwa na timu ambayo ina akina Ronaldo kibao kila mmoja
akikimbia na mpira kufunga yeye badala ya kutoa pasi ni jadi ya CCM ya
leo. Lengo ni labda kutafuta kumzidishia umaarufu Ronaldo mhusika
binafsi na labda kwa CCM ya sasa hilo ni sawa kwa vile CCM haijioni kama
chama cha ukombozi tena bali chama dume na chama tawala milele na
milele. Chadema ya Freeman Mbowe, Dakta Slaa, John Mnyika, Mabere
Marando, Prof Baregu na Prof Safari, kutaja wachache, ni bora iendelee
kujiona kama chama cha ukombozi kuona ni sawa kukataa dhana ya ki-CCM ya
"Umoja ni Ushindi"
Uchambuzi wangu unaweka kando urafiki na
udugu wa kifamilia wa karibu kati yangu na Dakta kitila Mkumbo na
mwanangu Zitto Kabwe na heshima na mapenzi yangu kwao kama wachambuzi
mahiri wa mambo vinabaki pale pale. Wanaweza kuishi bila hata kuwakwenye
chama chochote kama mimi na bado wakaendelea kutetea mabadiliko
Tanzania katika nafasi zao katika jamii.
No comments:
Post a Comment