Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba amesema kuwa anatafakari iwapo awanie urais katika Uchaguzi Mkuu
wa 2015, kutokana na kuwapo kwa watu wengi hasa ndani ya CCM,
wanaomtaka kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Makamba ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu
(NEC) ya CCM alisema: “Kwanza ni kweli kwamba kuna ushawishi kuhusu
suala hilo kutoka kwa vijana walioko nje na ndani ya chama, wanataaluma,
baadhi ya wazee na watu wengine iwe kwa makundi au mtu mmoja mmoja
wamekuwa wakinishawishi kugombea kwa muda sasa.”
Aliongeza: “Mwanzoni sikuona uzito sana, yaani
sikuzingatia sana, lakini kwa kadiri siku zinavyokwenda ni kwamba
ushawishi umekuwa mkubwa na hivyo niseme ni jambo ambalo sasa
ninalitafakari kwa kina”.
Alisema ikiwa ataamua kuwania urais, atafanya
hivyo wakati mwafaka kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na chama
hicho, lakini akasema kwa sasa si wakati wake. Makamba alikuwa akijibu
hoja za gazeti hili lililotaka ufafanuzi wake kutokana na kuwapo kwa
taarifa kwamba ameanza harakati za kuusaka urais katika Uchaguzi Mkuu wa
2015.
Gazeti hili lilidokezwa kuwa hatua yake hiyo
imemwingiza katika mvutano usio rasmi na wanasiasa ambao tayari
wameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini,
wakiwamo wale wa kambi ya urais aliyokuwa akidaiwa kuwa mmoja wao.
Awali iliaminika kuwa Makamba alikuwa katika kambi
ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini wachambuzi wa masuala
ya kisisa wanasema ‘katika siku za karibuni mwenendo wake unaashiria
kwamba si mmoja wa wanaomuunga mkono kiongozi huyo, bali ni mtu mwenye
mipango yake binafsi ya kisiasa”.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema
mwenendo wa Makamba umewakasirisha baadhi ya wanasiasa hususan
wanaomuunga mkono Lowassa ambao mara kadhaa wamesikika hadharani
wakimlalamikia kwamba ni msaliti.
Hata hivyo, Makamba katika maelezo yake anasema
hajawahi kuwa katika kundi lolote la kumuunga mkono mtu yeyote kwani
yeye haamini katika makundi. “Ninaamini katika kundi moja, nalo ni CCM,”
alisema.
Aliongeza: “Kwa hiyo mtu yoyote akinikasirikia kwa
sababu zozote zile za kisiasa nitamshangaa maana sijawahi mahali popote
na kwa namna yoyote kujitanabaisha kwamba mimi nipo kwenye kundi
fulani, au kundi la mtu yeyote.”
Sababu za mashaka
Miongoni mwa nyedo zinazotiliwa shaka za
mwanasiasa huyo ni hatua yake ya kushiriki katika Mkutano Mkuu Maalumu
wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) uliofanyika Zanzibar ambako pamoja na
mambo mengine aligawa simu zaidi ya 100 aina ya Samsung Galaxy kwa
wajumbe wa mkutano huo.
Imethibitika kwamba mpango huo ulikuwa ni wake
binafsi na haukuwashirikisha waliokuwa wakiamini kwamba wako naye katika
harakati za kumuunga mkono Lowassa.
No comments:
Post a Comment