Gazeti la Tanzania Daima Toleo na. 3280 la tarehe 26 Novemba 23
limenukuu kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini George
Simbachawene wakati akizungumza na kipindi cha Kumepampazuka
kilichorushwa na Redio One juu ya Serikali kupandisha bei ya umeme kama
Shirika la Umeme (TANESCO) lilivyoomba.
Katika habari hiyo Simbachawene amenukuliwa akisema kwamba endapo kuna
mwananchi yeyote atakayeona gharama za umeme ni kubwa ni vema akaamua
kuwasha kibatari au akae giza.
Rais Jakaya Kikwete anapaswa kumwagiza Waziri wa Nishati na Madini Prof
Sospter Muhongo kuwaomba radhi wananchi kwa kauli hiyo iliyotolewa na
Naibu Waziri Simbachawene kwa niaba ya wizara anayoiongoza.
Aidha, ni vyema Rais Kikwete kwenye hotuba yake kwa taifa ya mwisho wa
mwezi huu akawaeleza wananchi iwapo uamuzi huo wa kupandisha kwa mara
nyingine bei ya umeme ndio utekelezaji wa ahadi ya maisha bora aliyoitoa
kwa watanzania kuanzia kwenye uchaguzi wa mwaka 2005.
Hii ni kwa sababu kupandisha bei ya umeme kuna athari ya kuchangia
katika ongezeko la gharama na ugumu wa maisha kwa kuwa shughuli za
uzalishaji na maisha ya kila siku zinategemea kwa kiwango kikubwa
nishati.
Kauli hiyo ya Simbachawene inadhihirisha mtazamo finyu wa kisera kwa
Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba mahitaji ya
nishati ya umeme ni kwa ajili ya kuondoa giza ambapo mbadala wa haraka
ni kibatari.
Serikali inayoongozwa na CCM inapaswa kutambua kwamba mbadala wa nishati
kwenye uzalishaji, huduma za kijamii na maisha ya kila siku ya wananchi
katika karne ya sasa ya sayansi na teknolojia hauwezi kuwa kibatari.
Kwa upande mwingine, umma ni muhimu ukafahamu kwamba uamuzi huu wa
Serikali kupandisha bei ya umeme wakati huu ni matokeo ya kutekeleza
masharti ya Benki ya Dunia ambayo Serikali ilipewa Washington DC Oktoba
2013 bila kuzingatia hali halisi ya uchumi wa nchi na ustawi wa
wananchi.
Aidha, uamuzi huu ni wa kuwabebesha wananchi mzigo wa gharama za muda
mrefu za ufisadi katika sekta ya nishati nchini na ubovu wa mikataba
inayoendelea kutumika mpaka hivi sasa katika sekta hii nyeti.
Hata hivyo Waziri wa Nishati na Madini Prof Muhongo alisema uongo
bungeni kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013 nilipohoji kuhusu
masuala muhimu ya nishati ambayo iwapo hatua muafaka zingechukuliwa kwa
wakati zingeepusha nchi kulazimika kuongeza kwa mara nyingine gharama za
umeme.
Naomba Rais Kikwete katika hotuba yake kwa taifa arejee hotuba
nilizowasilisha kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inayoongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tarehe 27
Julai 2012 na 22 Mei 2013 na kutoa majibu ya kweli kwa wananchi katika
masuala yote tuliyohoji kuhusu nishati.
Nakala ya Hotuba hizo zinapatikana katika tovuti ya bunge na kwenye mtandao wa http://mnyika.blogspot.com
( Hotuba ya Julai 2012- http://mnyika.blogspot.com/2012/07/hotuba-ya-kambi-rasmi-ya-upinzani.html na Hotuba ya Mei 2013- http://mnyika.blogspot.com/2013/05/hotuba-ya-msemaji-wa-kambi-rasmi-ya.html )
Udhaifu uliotajwa kwenye hotuba hizo na katika kauli za Waziri Muhongo
na Naibu Waziri Simbachawene kwa nyakati mbalimbali unaweza kusababisha
Matokeo Mabaya Sasa- Bad Results Now (BRN) badala ya Matokeo Makubwa
(Big Results) kwenye sekta ya nishati.
Hivyo iwapo Rais kupitia hotuba yake kwa taifa mwishoni mwa mwezi huu wa
Novemba 2013 hataeleza hatua alizochukua kuondoa udhaifu huo; nitaeleza
hatua za ziada ambazo tutachukua katika kuisimamia Serikali kunusuru
uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi kutokana na ongezeko la bei ya
umeme na mapungufu mengine kwenye sekta ya nishati.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
No comments:
Post a Comment