Sehemu ya hotuba ya mh. Zitto Kabwe. (Verbatim)-Kaliua, Tabora 9/11/2013
".......Kwa hiyo tunahitaji nguvu kazi kubwa sana. Siyo kazi ndogo na
ndiyo maana kwa kufanya kazi kubwa kama hii, na ninapokuwa na ajenda
kubwa, ni mtaji sana kuwa na support ya Watanzania wa ndani ya chama
changu na nje ya chama changu.
Kinachonisikitisha ni kwamba
wakati niko nafanya kazi kubwa kama hii, kazi ambayo ina hatari kwa
maisha yangu, kwa sababu watu wana nguvu sana. Mimi mtoto wa masikini tu
na ninatoka Kigoma. Sina nguvu yoyote. Ndugu yangu ni mwenyezi Mungu
(Allah Subhanahu Wa Ta'Ala). Basi nguvu yangu ni ninyi watu kuwategemea.
Kwamba unapokuwa unafanya kazi hii ya kupambana na watu wa namna hii
upate nguvu. Bahati mbaya sana, tena sana, sana. Navunjwa nguvu na watu
wengine wanaonivunja nguvu ni watu ambao mko chama kimoja ambapo kwa
hali ya kawaida walipaswa kutia nguvu.
Inasikitisha kwa sababu
unapokuwa mwanasiasa lazima kuwe na mashambulizi ili yakukomaze. Nani
huyo mwanasiasa asiyepata mashambuzi haiwezekani au siyo.
Lakini unapokuwa una ajenda ambayo unaisukuma halafu unapigwa mishale na
watu wako, si utaanza kwanza kujilinda na ile mishale halafu hiyo
ajenda unaisahau. Anayefaidika ni nani?. Ni adui.
Na huu ndiyo
ujumbe ambao nataka hasa watu wa CHADEMA wajue. Tuna kazi kubwa. Kazi
ya kupambana na dude CCM siyo mchezo. CCM ni kama lipweza hivi lina
miguu mingi. Ili uliue lazima upige miguu mingi karibari mpaka afe na
wakati anapotaka kufa lazima atetereke, lazima atumie watu kuwavuluga,
lazima. Huwezi kuwa na chama ambacho kimekaa madarakani kama CCM kwa
muda mrefu sana, halafu kinaona wananchi wamekichoka, halafu eti kikae
kimya kikubali kutoa madarakani. Kinachokifanya ni kuonyesha kwamba,
aah, watu wote ni walewale. Bora zimwi likujualo. Ndiyo kazi
inayofanyika.
Ninataka niwahakikishie wanaCHADEMA kwamba
hakuna mgogoro wowote CHADEMA. Kuna watu wachache, wachache sana ambao
hawana kazi isipokuwa kazi ni kugonganisha viongozi ili viongozi
wasielewane, ili viongozi wasipoelewana ndiyo faida kwao, ndiyo
wanakula, ndiyo wanaonekana wanafanya kazi.
Na kuna uwezekano mkubwa sana watu hao wanatumika na watu wa nje ya chama ili kuvuluga.
Nataka niwaonye kwamba hatuwezi hata kidogo kushika dola kama ninyi
wenyewe wananchi mnatuona hatuko wamoja. Mtatupa dola mkituona siyo
wamoja? (Hapana-Sauti ya wananchi). Si mtatuona kama CCM tu.
Kwa hiyo siyo ufahari hata kidogo kwa CHADEMA kuonekana na yenyewe ina
migogoro kama CCM. Siyo fahari. Inawavunja moyo nyie, nyie mnatuamini
kwamba sisi tutaleta mabadiliko.
Ngojeni niwaambie. Historia
ya chama chetu ni historia ya kidemokrasia. Chama hiki kimeanza mwaka
92. Mwenyekiti wetu wa kwanza Mzee Mtei. Mwaka 95, Mzee Mtei na Marehemu
Bob Makani walisimama kugombea Urais ndani ya chama, na Urais ulikuwa
na nguvu kweli kweli. Baadaye chama kikaamua kwamba, aah, CHADEMA
itamsapoti Mrema wakati huo. Je, mliwahi kusikia hadharani Bob Makani na
Mzee Mtei wanagombana. Mwaka 1998, Marehemu Mzee Bob Makani na Mzee
Ndesamburo waligombea uenyekiti wa Taifa wa chama, kina Mbaruko hawa ni
mashahidi. Mwaka 98, Marehemu Mzee Bob Makani akashinda. mlisikia
migogoro? (Hapana-sauti ya wananchi).
Mwaka 2009, kwa kufuata misingi hiyo hiyo ya demokrasia, mimi niligombea uenyekiti.
Kwa nini uwe nongwa, si ndiyo demokrasia tu. Si ndiyo demokrasia tu na mkimaliza mnaenda kujenga chama.
Na tumeenda kujenga chama na tumeibua mambo ndani ya bunge dhidi ya
CCM. Tumeibua hoja zenye nguvu ndani ya bunge dhidi ya Chama Cha
Mapinduzi. Tumeibua hoja za kumpiga chini Waziri Mkuu na Mawaziri wanane
wakafukuzwa kazi ili kumuokoa Waziri Mkuu. Haya yamefanyika baada ya
2009.
Sasa watu wanaona uchaguzi unakaribia, halafu
sijatangaza. Vulugu zinaanza, maneno yanaanza, uzushi unaanza ili
kutugawa bila sababu, bila sababu yoyote, bila sababu yoyote ile.
Kwa kweli kwa mtu kama mimi ambaye nimeingia kwenye siasa mdogo sana.
Kigoma wamenichagua na miaka 29, na kubeba majukumu makubwa sana
kisiasa, makubwa kwa maendeleo ya Mkoa wangu.
Sasa hivi
tunafanya kazi ya kanda ya jimbo letu hili la kanda ya Magharibi.
Tumeibua hoja nzito nzito bungeni. Kwa umri mdogo sana.
Kwa
mishale ya kisiasa ninayopigwa, nadhani Mwenyezi Mungu amenipa sifa ya
ziada ya uvumilivu (Makofi-kutoka kwa wananchi), lakini mimi ni
binadamu, msisahau hilo. Mimi ni binadamu, mkinifinya ninaumia
(Kicheko-kutoka kwa wananchi). Ninatoka damu kama mwingine yoyote.
Nimechoka kupigwa mishale, nimechoka (Kicheko-kutoka kwa wananchi).
Kwa hiyo ni lazima tuambizane kuwa turudi kwenye reli ya kujenga
misingi ya chama hiki ili tuwakomboe wanyonge. Tuhakikishe hatuwaangushi
wananchi.
Hivi mnakumbuka kulikuwa na chama chenye nguvu kama
NCCR-Mageuzi. Mnakumbuka kulikuwa kuna mtu mwenye nguvu kama Augustino
Mrema. Lakini walifanyaje?. Walianza kusema Marando msaliti. Mabere
Marando alachafuka, akawa ananuka.
Leo Marando yuko wapi?. Siyo
Kamanda wetu?. Siyo mwanasheria wetu?. Halafu Mrema yuko wapi?. Amebaki
na Mbunge mmoja, yeye mwenyewe. Lazima tujifunze.
Lazima
tujifunze kuruka viunzi vya CCM kutaka kambi ya upinzani igawanyike.
Kutaka vyama vya upinzani vipasuke. Lazima mjifunze kuruka viunzi.
Na ninyi ndiyo mnapaswa kuwa nguzo yetu. Ninyi mnapaswa kutuambia
kwamba tunataka muwe wamoja. Na sisi tumeamua kanda yetu hii na sasa
tunazunguka. Kwenye ziara tumebakiza Urambo. Tulikuwa tumebakiza Kariua,
lakini bado kwa sababu jimbo hili ni kubwa na ninakubaliana na risala
ya viongozi lazima turudi twende kwenye kata za kutosha.
Tunataka tuihamishe Tabora. Kigoma irejee heshima yake. Mpanda iamuke
zaidi ili kanda yetu iongoze katika siasa za mageuzi na kuhakikisha
kwamba CHADEMA inatoa wabunge wengi zaidi. (makofi-Kutoka kwa wananchi).
Ni lazima wanachama na uongozi ambao badala ya kufanya kazi ya
kumshughurikia adui wanaanza kuleta chokochoko ndani ya chama
wachukuliwe hatua za kinidhamu bila upendeleo. Bila upendeleo wowote
(Makofi-kutoka kwa wananchi).
Sababu mkishaanza kuwa na
upendeleo ndiyo mnaenda kuwa kwenye maneno ya CCM. Kila siku CCM
wanasema CHADEMA, aaah, CHADEMA yao ni chama cha kidini. Chama cha
Wakristo hicho, lakini tunasema, kama ni chama cha Wakristo, Arfi wa
Mpanda ni Mkristo?. Hapana. Zitto Mkristo?. Hapana.
Lakini leo ukiona kundi la watu fulani wanamshambulia Arfi, wanamshambulia tu. Watu watafikiria.
Kila siku CCM wanashambulia wanasema CHADEMA chama cha Wachaga. Upuuzi mtupu. Tunasema hapana.
Viongozi wetu angalieni. CHADEMA ni kiti tu. Kwa nini msisimamie?.
Lakini wapumbavu wanaoenda kutumiwa na CCM bila kujiangalia wamejikuta
wanawashambulia watu ambao ndiyo ngao ya kuonyesha umoja ndani ya chama.
Lazima tukatae hayo mambo na lazima viongozi tuhoji haya mambo na
tusipoonya tutaonekana tutaonekana tunashiriki au siyo?. (Ndiyo-sauti ya
wananchi). Tutaonekana tunafanyaje?.
Tunaonekana tunashiriki na sisi.
Waha tuna msemo, tunasema hivi, UKIMUONA KIFARANGA YUKO JUU YA CHUNGU UJUE CHINI KUNA MAMA YAKE.
by- Zitto Kabwe
No comments:
Post a Comment