Kutokana
na kuwepo kwa taarifa ya Ndugu A.O. Chitanda, huku pia waandishi wa
habari wakitaka kujua na kupata ukweli kutoka Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA, tunapenda kutoa ufafanuzi mfupi;
Kwanza
suala la maamuzi ya Kamati Kuu ya kuwavua uongozi ndani ya chama, Ndugu
Zitto Kabwe na Dkt. Kitila Mkumbo, mjadala wake kwa upande wa
chama umeshafungwa, huku taratibu za kikatiba za ndani ya chama
zikiendelea.
Pili suala la restructuring ya Makao Makuu ya Chama. Chitanda ametoa taarifa akiwataja wakurugenzi wafuatao, kuwa ni
wapya;
- Mkurugenzi wa Oganaizesheni Mhe. Singo Kigaila Benson.
- Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano ya ndani Mhe. John Mnyika (Mb).
- Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji Mhe. Anthony Komu.
- Mkurugenzi wa Bunge na Halmashuri Mhe. John Mrema.
- Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Mhe. Wilfred Lwakatale.
Wakurugenzi wote aliowataja si wapya. Mkurugenzi pekee ambaye uteuzi
wake ni mpya na umefanyika hivi karibuni na kuthibitishwa ni Mwanasheria
Peter Kibatala, atakayesimamia Kurugenzi ya Sheria na Haki za Binadamu.
Kama
ni suala la kuangalia mtu anatokea wapi (ambalo halijawahi
wala haliwezi kuwa moja ya vigezo), ili kuonesha ukweli na kubainisha
uongo wa watu wanaojaribu kufanya kazi ya CCM wakisema wao ni
wanCHADEMA, kwa kutumia propaganda zile zile na kuzifanya kuwa ni kete
zao za kisiasa, tunaweza kutaja maeneo ya wanakotoka au asili yao kama
ifuatavyo;
- Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji, Antony Komu- Kilimanjaro.
- Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare- Kagera.
- Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni, Benson Kigaila- Dodoma.
- Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John John Mnyika- Mwanza
- Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, John Mrema- Kilimanjaro.
- Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala- Morogoro.
Hadi
sasa uteuzi wa kurugenzi za Makao Makuu ya CHADEMA haujakamilika.
Bado kuna nafasi zinazotakiwa kujazwa kwa kufuata taratibu za chama.
Hii ni kwa sababu
restructuring,
inayofanyika ndani ya chama, hadi sasa inaendelea katika ngazi ya Makao
Makuu na kanda, kisha itaendelea kwa ngazi za mikoa, wilaya, majimbo,
kata, kijiji na hatimaye kitongoji.
Katika restructuring hiyo ya
nafasi za uteuzi, inayoendelea sasa ambayo inakwenda hatua kwa hatua,
hadi kuwa na makatibu wa kuajiriwa ngazi ya chini ya chama, chama
kinazingatia uwezo, uadilifu na utayari wa mtu katika kutoa utumishi
bora kwa wanaCHADEMA na Watanzania wote katika nafasi husika.
Suala
la maslahi ya watumishi wa CHADEMA ni utaratibu wa chama
ambao unajadiliwa, kufikiwa uamuzi na kisha kuridhiwa kwenye vikao vya
chama, kama ilivyofanyika kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichoketi
karibuni.
Katika suala hili la maslahi ya watumishi wanaojitolea
Makao Makuu ya CHADEMA ambayo si siri, Ndugu Chitanda amesema uongo
mkubwa. Kwanza si kweli kuwa Ofisa Mwandamizi anaweza kulipwa posho
kubwa kuliko Mkurugenzi wa kurugenzi husika.
Ndugu huyo
anadhihirisha uongo huo yeye mwenyewe kwa kuandika hivi; “800,000/= za
awali na sasa itakuwa ni kuanzia Tshs. 1,500,000-2,500,000/= kwa
Mkurugenzi na kutoka Tshs. 6,800,000/= kwa Afisa Mwandamizi na sasa ni
Tshs. 1,000,000-1,500,000/=”.
Pia si kweli kuwa kila mtumishi
anayejitolea Makao Makuu analipwa. Mathalani, wakurugenzi wenye nafasi
za ubunge, hawalipwi hata shilingi moja kwa kazi zote wanazokitumikia
chama na Watanzania kwa ujumla.
Kwa maelezo hayo ya kutengeneza,
ni kwamba hadi sasa Ofisa Mwandamizi anapokea posho kubwa kuliko
Mkurugenzi na hata baada ya ‘restructuring’ atapata posho kulingana na
Mkurugenzi. Anapaswa kuwa mkweli. Mtu anayetaka kuonekana muungwana,
anapaswa kujiweka mbali na uongo pamoja, maneno ya kutunga pamoja na
upotoshaji wa makusudi.
Kama ilivyoandikwa hapo juu,
*restructuring* inaendelea. Ni hatua kwa hatua. Itafika ngazi za chini
kama Baraza Kuu lilivyoagiza. Kwa sababu hiyo hadi sasa uteuzi wa
Makatibu wa Mikoa na Wilaya haujafanyika.
Hata hivyo ruzuku
imekuwa ikipelekwa kila kanda, mkoa, wilaya na jimbo kama ilivyoridhiwa
na Kamati Kuu. Na hii ni zaidi ya pikipiki, kompyuta na magari
yaliyopelekwa kila kanda. Angelikuwa mkweli, nagelisema na hili pia.
Ndugu
Chitanda anajichanganya katika taarifa yake yote. Hii ni moja ya
sifa ya kukosa hoja hivyo mtu anaamua kuibua viroja au kutunga maneno
kwa sababu ya kushindwa kusema ukweli.
Anaonesha kuwa alikuwa mtu
aliyeaminiwa hadi kuwa katika vikao muhimu, lakini wakati huo huo
anasema kuna ubaguzi! Tunapaswa kumhurumia kwa kushindwa kuunganisha
hata mawazo yake na kupata mtiririko wa hoja zenye mantiki! Angelikuwa
mkweli angesema katika vikao vya sekretarieti na CC, aliingiaje kama
kuna ubaguzi wa dini!
Kwa sababu anazozijua yeye, Ndugu Chitanda
ameamua kujipachika cheo ambacho hajawahi kuwa nacho. Amejiita kuwa ni
Katibu wa Sekretarieti ya Makao Makuu.
Ndani ya CHADEMA pamoja na
kwamba nafasi hiyo imetajwa ndani ya Katiba ya Chama, hakuna mtu ambaye
ameteuliwa kutumikia nafasi hiyo. Kama anaweza athibitishe kwa kutoa
barua ya uteuzi kutoka kwa Katibu Mkuu.
Mahali pengine
amejitambulisha kuwa ni Katibu Ofisi ya Katibu Mkuu. Ofisi hiyo ina
Katibu Mtendaji mmoja ambaye ni Mzee Victor Kimesera, mmoja wa waasisi
wa CHADEMA.
Operesheni ya Chama inayoendelea nchi nzima kwenye majimbo 103, si suala la siri wala lengo bovu kama anavyotaka umma uamini.
Ni
mwendelezo wa mpango mkakati wa chama kupitia progamu za Vuguvugu
la Mabadiliko (M4C), unaotekelezwa kwa hatua mbalimbali na kwa mbinu
tofauti tofauti pamoja na dhana ya CHADEMA ni msingi.
Operesheni
hiyo ambayo ni mwendelezo wa nyingi za namna hiyo zinazokwenda ngazi za
chini kabisa za chama, zikilenga kuimarisha taasisi na mifumo, imeanza
wiki hii na ilitangazwa mbele ya waandishi wa habari.
Tungependa
kumalizia ufafanuzi huu mfupi kwa kutoa tahadhari kwa umma kuwa makini
na matamko ya watu wa namna hii. Maana tunajua kwa uhakika yako mengi ya
namna hii yatatokea kadri ambavyo Watanzania wanakaribia kuona
na kuishi matumaini ya mabadiliko ya kiutawala na mfumo ndani ya nchi
yao.
Mathalani katika taarifa yake, Ndugu Chitanda amedhihirisha
na kuonesha kuwa ni aina ya watu ambao wanaCHADEMA na Watanzania kwa
ujumla wanapaswa kuwaangalia kwa macho ya kuhoji na tahadhari ya hali ya
juu, anasema hivi;
“Kwa kuwa siamini kwamba kuvuliwa nyadhifa
kwa Zitto Kabwe na Dkt Kitila Mkumbo ni kwa sababu ya waraka wa ushindi,
bali ninaamini kuvuliwa kwao ni kutokana na hofu ya uchaguzi, ubaguzi
wa kikabila na kikanda.”
Aya hiyo pekee inayotumia lugha
wanayotumia mahasimu wa CHADEMA, wakiongozwa na viongozi waaandamizi wa
CCM, wanaohangaika kutokana na Watanzania kuwakataa, wakijiandaa
kuwaondoa madarakani kwa sababu sera zao zimeshindwa, inatosha kuonesha
uhalisia wa taarifa yake yote.
Ni kauli za namna hii (kuwatisha
na kutaka kuwatenganisha Watanzania) ambazo zimekuwa zikitumiwa na
watawala kama njia pekee ya kutaka kuzuia upepo wa mabadiliko unaovuma
nchi nzima, zimekuwa zikiwaunganisha zaidi Watanzania kuiunga mkono
CHADEMA bega kwa bega, ili kupata haki na matumaini ya wanyonge, katika
mapambano ya awamu ya pili, kuelekea uhuru wa kweli.
Imetolewa leo Novemba 30, 2013, Dar es Salaam na;Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA