Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amevunja
ukimya na kusema hayuko tayari kwa sasa kuwataja Watanzania wenye
mabilioni huko Uswisi na kuitaka Serikali ifanye uchunguzi.
Zitto ndiye aliyeibua hoja bungeni kuwa kuna Watanzania walioficha Sh315 bilioni katika taasisi za fedha nchini Uswisi.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Zitto alisema
anasita kutaja majina hayo sasa ili kuepusha kile alichosema majina hayo
kutumiwa vibaya bila kujali kama Watanzania walizipata fedha hizo
kihalali au la na kuzihifadhi nje ya nchi.
Alisema ameshauri mchunguzi wa kimataifa anafaa kufanya kazi hiyo.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), amesema wastani wa Sh729.3
bilioni hutoroshwa kila mwaka kwenda nje ya nchi.
Alisema kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jaji Fredrick Werema kwamba yeye (Zitto) hakutoa ushirikiano wa kamati
inayochunguza sakata hilo si ya kweli.
“Nataka niwahakikishie, nimekutana mara nne na
kamati hii. Nimewapa mpaka jina la mchunguzi wa kimataifa atakayeweza
kuwasaidia katika uchunguzi huu, leo naambiwa sitoi ushirikiano,”
alisema Zitto.
Alisema mchunguzi huyo wa kimataifa ana uzoefu
katika uchunguzi wa suala kama hilo na angeweza kuwatambua kwa majina na
kiasi cha fedha na pia uhalali na uharamu wa fedha hizo.
Alisema ameshangazwa na hatua ya Serikali kumbeza
pale alipopendekeza suala la kutafutwa mchunguzi wa kimataifa lakini
siku chache baadaye ikatangaza magazetini nafasi ya kazi hiyo.
Tangazo hilo lilichapwa Desemba 17, mwaka huu siku
ambayo Zitto alisema kwamba angesoma maelezo binafsi kujibu kauli ya
Jaji Werema. Hata hivyo, alisema alikosa nafasi. Zitto amesema
hashurutishwi na azimio la Bunge kutaja majina hayo kwa sababu yeye siyo
chombo cha uchunguzi ambacho kinapaswa kuwa na mkono mrefu.
Alisema wakati akikabidhi majina ya Watanzania
hao, angependa ushahidi huo uwe umefanyiwa uhakiki na vyanzo vyake vya
kimataifa na vyombo vya usalama vya Serikali nchini.
“Siko tayari kutaja kwa sasa. Narudia tena kwa
sasa hayo majina maana naweza kusababisha wahukumiwe na umma bila
kupitia utaratibu uliowekwa na sheria zetu hapa nchini,” alisema Zitto.
No comments:
Post a Comment