Suala la udini na ukabila ndani ya CHADEMA kuendana na mtizamo na mawazo yangu-Albert Msando
Leo ni tarehe 1/12/2013. Mwezi wa mwisho wa mwaka 2013. Ni siku ya Jumapili.
Nimeonelea vyema niongelee suala (sio hoja) la udini na ukabila ndani
ya CHADEMA kuendana na mtizamo na mawazo yangu ambavyo kwa pamoja
vinasababisha msimamo wangu binafsi.
Kumekuwa na malalamiko na
manung'uniko mengi kwamba CHADEMA ni chama cha kidini na kikabila
(baadae ilibadilika ikawa kikanda). Majibu au maelezo yametolewa kila
mara lakini kama ilivyo kawaida bado maswali yapo.
Kwa nini udini na ukabila? Kuna ukweli au ni hisia? Hakuna ukweli ila ni hisia ambazo ni sahihi kuwepo (justified concerns).
Udini na ukabila ni masuala ambayo hayakubaliki sehemu yeyote ile
katika jamii yetu. Ni dhambi. Pia ni kosa kumbagua au kumpendelea mtu
kwa sababu ya kabila lake au dini yake ambayo kwake yeye yako sawa
kabisa.
Udini:
Kwenye siasa vyama viwili vimeandamwa sana kuhusu udini. Chadema na CUF. Kwamba kimoja ni cha Wakristo kingine cha Waislamu.
Chanzo:
Kwa tafakari yangu ya juu juu hii ni kwa sababu ya sura ya uongozi wa
juu wa vyama hivi. Chadema imekuwa na viongozi wengi Wakristo wakati CUF
imekuwa na viongozi wengi Waislamu. Hii inajumuisha wabunge wa vyama
hivi vyote viwili!! Mfano Chadema ina Wakristo wengi zaidi ya Waislamu
(wengine walikuwa wachungaji na bado wanaitwa hivyo) na CUF ina Waislamu
wengi zaidi ya Wakristo.
Pia vyama hivi vimejikuta vina
wafuasi katika maeneo ambayo ni waumini wa dini mojawapo jambo ambalo
linafanya hayo mawazo yapate nguvu zaidi. Kwa mfano CUF maeneo ya Tanga
na Zanzibar na Chadema maeneo ya Kilimanjaro nk.
Jambo jingine
ni viongozi wa dini hizi mbili pia wamekuwa wakionekana kujitanabaisha
na viongozi wa vyama hivi kwenye matukio na shughuli mbalimbali.
Kwa mfano, utakuta kanisa linamualika kiongozi mkristo wa Chadema
kwenye Harambee au kiongozi wa Chadema anahudhuria msiba wa kiongozi wa
dini mkristo lakini hautamsikia kiongozi huyo akihudhuria Harambee ya
msikiti au mazishi ya kiongozi wa dini ya Kiislamu. And vice versa is
also true.
Mawazo na hisia zinajengeka hapo...ni vigumu kuepuka hisia na mawazo kujengeka kati hali kama hiyo.
Hiyo haitokani na ukweli kwamba kiongozi huyo mkristo au muislamu ni
mdini bali inatokana na uwezo mdogo wa kiongozi husika kuona madhara ya
kushindwa kutambua hatari ya hisia hasi kwa matendo yake.
Chadema (tuache CUF) kwa kiasi kikubwa tumeshindwa kuvuka mstari na
kuwafikia waumini wa Kiislamu aidha kwa kupitia viongozi wetu Wakristo
au viongozi wetu Waislamu ili kuwathibitishia kwamba chama chetu hakina
agenda ya dini.
Ni tabia ya mwanadamu kumsikiliza na kumfuata
yule ambaye wana jambo linalofanana kwa wepesi zaidi kuliko yule ambaye
ni mtu wa mbali au hawafanani. Hivyo mara nyingi binadamu atamsikiliza
au kumfuata yule ambaye anajipambanua kwamba atamtetea maslahi yake. Sio
kwa sababu ni mdini ila kwa sababu anajisikia salama zaidi yeye binafsi
na pia anaona anamsaidia 'mwenzake'.
Hatuwezi kuepuka uwepo wa
hizo hisia kama hatutachukua hatua stahiki. Tukibaki kujidanganya
kwamba ni propaganda tatizo halitaondoka badala yake haitakuwa hisia
tena ila ukweli mchungu na itatuathiri umoja wetu kama chama na taifa
kwa ujumla.
Malalamiko ya udini yapo na yanatokana na sababu
ambazo baadhi nimezitaja. Ila sababu KUBWA ni utashi wa viongozi wakati
wa maamuzi. Mara nyingi huwa hawaangalii tafsiri atakayotoa mwanachama
au Mwananchi kuhusu maamuzi fulani kwenye masuala ambayo yatagusa dini
au imani yake.
Mfano, ni kiongozi gani amelisimamia waziwazi
suala la mahakama ya kadhi kwenye Katiba mpya? Ni nani amesema anakubali
au anakataa mahakama ya kadhi?
Hatuna viongozi ambao
wanajipambanua kwa MISIMAMO yao kuhusu mambo ambayo ni ya msingi kwa
Mwananchi. Tuna viongozi ambao tunapenda kujificha kwenye kichaka cha
'kauli ya chama' 'ilani ya uchaguzi' 'msemaji wa chama' 'sera ya chama'
nk.
Ni nadra sana utamsikia kiongozi akisema 'Mimi Albert
Msando naunga mkono uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi. Mimi ni mkristo
lakini naamini kwamba Waislamu wanastahili kuwa na mahakama yao'. Wengi
wetu hatuthubutu.
Chadema haina udini hata kidogo. Ila
inashindwa kuondoa hisia hizo kwa kuchukua hatua badala ya matamko na
kukanusha. Ni lazima tukae chini na viongozi wa Waislamu na madhehebu
mengine kuwaeleza kwamba hatuna agenda ya siri dhidi ya Uislamu au
Waislamu na pia hatuna agenda ya siri kwa faida ya Wakristo au Ukristo.
Tuwaeleze malengo na nia yetu kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
Ukabila:
Hili sababu ni kama za suala la kidini ila
lenyewe ni matokeo ya uzembe zaidi. Tunaliacha liendelee bila sababu
zozote za msingi.
Chadema haiko Kilimanjaro au kanda ya
kaskazini peke yake. Ni kweli ina wabunge wengi kutoka upande huu lakini
pia kama chama kipo kila kona ya Tanzania bara.
Tunaweza
kujitetea kuhusu nafasi za uchaguzi lakini ni uzembe kuteua aidha
wabunge au viongozi kutoka kanda ya kaskazini. Siamini kwamba wenye
uwezo na mapenzi mema na Chadema wako kaskazini peke yake. Tunaweza
kuteua viongozi kutoka maeneo mengine kwa idadi kubwa na kusema wazi
kwamba mpango huo ni kuweka usawa katika uwakilishi. Sio KOSA!!!
Viongozi wetu wana changamoto ya kuweka mpango kazi kuthibitishia
wanachama na watanzania kwa ujumla kwamba sisi Chadema sio wadini wala
wakabila(wakanda).
Pia sioni sababu ya Mzee Mtei kuendelea
kutoa matamko kuhusu maamuzi au mwenendo wa Chadema kwa umma. Anaweza
kutoa ushauri au hata maelekezo kwa viongozi bila kutangazia umma.
Mwananchi wa kawaida kwa msaada wa adui yetu anaruhusiwa kuwa na hisia
kwamba chama ni cha Mbowe na Mtei! Kwa sababu tu Mbowe amemuoa mtoto wa
Mtei. Jambo ambalo ni ukweli kwamba Mbowe ameoa kwa Mtei. Lakini kuoa
sio sababu ya kusema eti chama ni cha familia. Sisi wote hatuwezi kuwa
wajinga kiasi cha kukubali hilo! Ni upuuzi kusema tunaweza kuruhusu.
Mimi binafsi Mbowe ni msimamizi wa ndoa yangu. Lakini sio sababu ya
mimi kuwa mwanachadema au Diwani wa Chadema. Na siwezi kuacha kumkosoa
kama atakosea kwa sababu tu ni msimamizi wangu. Mambo yetu ya kifamilia
hayana nafasi kwenye mambo ya chama. Lazima tutoke kwenye makoti yetu na
tuseme waziwazi kuhusu hili jambo na tuache kufanya teuzi ambazo
zinajenga sura ya ukabila au ukanda.
Msimamo wangu:
Chadema sio chama cha kidini wala kikanda. Kila mtanzania ana haki na nafasi ndani ya Chadema.
Ni jukumu la viongozi wote kuhakikisha kwamba udini na ukanda havipewi
nafasi. Matendo yetu kwa yale tunayoyasimamia na uteuzi tunaofanya
yaonyeshe sura hiyo. Huu ni WAJIBU wa kiongozi mwenye kuitakia mema
Chadema na nchi yetu.
Tuache porojo na siasa kwa kutoa majibu mepesi pale tunaposhutumiwa. Tufanye kwa vitendo. Let us attack the problem.
AGM 2013 Dec.
No comments:
Post a Comment