Waraka wa Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Ndg Absalom Kibanda kwa Rais Jakaya Kikwete
MHESHIMIWA Rais wangu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Nakusalimu kwa
salamu ya utii inayotambua na kuheshimu kwa dhati mamlaka makubwa na ya
juu uliyonayo kama mkuu wa taifa letu ambalo mazingira yake ya leo
yanapaswa yawe wenye mwelekeo wa kushangilia kama si kujivunia uhuru
ambao tuliupata mwaka 1961 na 1964 kwa kutegemea upande tulipo katika
muungano wetu.
Mheshimiwa Rais, najisikia faraja iliyojaa
majonzi moyoni kupata fursa hii adhimu kukuandikia waraka ambao msukumo
wake unasukwasukwa na dhamira njema kabisa ambayo aghalabu kiini chake
si kingine bali mapenzi mema kwa nchi na viongozi wetu wote.
Ni faraja kwa kuwa nimepata fursa ghali na adimu ya kuteta na kiongozi
wetu mkuu kwa upendo, uhuru na kwa kujiamini, huku nikiwa na uchungu
pia kwa sababu ujumbe ambao unabebwa na waraka huu ni wa kuumiza sana
nafsi, roho, akili na mwili.
Mheshimiwa Rais, wewe ni
kiongozi wa Watanzania wote tukiwamo sisi ambao baadhi ya wateule wako
wameamua kwa sababu wanazozijua wao na wakati mwingine wakidai kwa
maelekezo ya wakuu wao kutujengea taswira zinazotufanya tuonekane tu
watu wa ovyo na kada ya wanajamii waliokosa utu na eti tunaopaswa
kufundishwa hekima na somo la uzalendo ambalo limekuwa sehemu ya makuzi
yetu nyumbani, shuleni, jeshini na ndani ya jamii.
Kabla
sijafikisha ujumbe ambao nimeubeba kwa mfano wa mzigo mzito moyoni,
napenda kwanza kupitia fursa hii kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,
mwingi wa rehema na neema kwa kuniwezesha kuuona mwanga wa siku hii
njema ya leo ambayo kama si kwa kudra na mapenzi yake, yumkini
ingeongeza hesabu za siku ambazo kiwiliwili changu kingekuwa katika
kaburi la sahau ambalo kila kukicha linameza roho za makumi kama si
mamia ya Watanzania wasio na hatia wanaopoteza maisha kutokana na kazi
za mikono ya majahili, miungu watu waliojitwalia haki ya kuchagua aina
ya maisha na vifo vya watu wengine.
Baada ya hilo, kwa
niaba ya mamilioni ya Watanzania wenzangu ambao hawana fursa ya
kuwasiliana nawe kwa njia kama hii ya waraka niliyoitumia, napenda
kutumia pia wasaa huu kukushukuru wewe binafsi kwa namna ulivyojitoa
usiku na mchana pasipo kuchoka kuliongoza taifa hili katika mazingira
magumu yaliyojaa changamoto za kila namna ambazo wakati mwingine sina
shaka hata kidogo kwamba zimekuwa zikikunyima raha na kukosa usingizi.
Wakati nikikuandikia ujumbe huu, picha na taswira yako inayonijia
ni ile ya Machi 8, mwaka huu siku uliponitembelea kando ya kitanda
nilichokuwa nimelazwa katika Hospitali ya Milpark, Johanesburg kule
Afrika Kusini ikiwa ni siku mbili tangu nilipovamiwa, nikajeruhiwa na
kupewa ulemavu na majahili ambao hadi leo hii wameweza kuukwepa mkono
mrefu wa vyombo vya dola unavyoviongoza.
Mheshimiwa Rais,
japo nilikuwa nina maumivu makali na machungu ya kupoteza jicho, kidole
na kupasuliwa kwa mifupa ipatayo minane katika paji langu la uso,
ukiacha taya lililoachanishwa kikatili na watesi wangu wale, bado
ninaweza kukumbuka kwa ufasaha namna ulivyozungumza nami ukionyesha
jinsi ulivyokuwa ukiguswa na kuumizwa sana na tukio lile.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, tangu niliporejea nchini miezi
sita iliyopita sijapata kukutana nawe ana kwa ana ingawa nilipata fursa
ya kukutumia salamu zangu za shukrani kupitia kwa marafiki zako kadhaa
akiwamo msaidizi na mshauri wako nambari moja, Makamu wa Rais, Dk.
Mohammed Gharib Bilal ambaye siku zote wakati nikiwa katika matibabu
nchini Afrika Kusini na hata baada ya kurejea nchini, alionekana kuwa
mtu wa kukosa amani kabisa pasipo kunijulia hali kwa njia ama ya simu,
wasaidizi wake na mwisho kwa kuonana nami ana kwa ana.
Nayarejea haya yote huku nikitambua kwamba, wakati ninapoandika waraka
huu ndiyo kwanza umerejea kutoka nchini Marekani ambako ulikwenda
kuchunguzwa afya yako ambayo nina matumaini makubwa ni njema hasa kwa
kuzingatia ukweli kuwa, ulikwenda huko siku chache tu baada ya
kuiwakilisha vyema nchi yetu katika msiba mzito wa shujaa wa mapambano
ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, mzee wetu, Nelson Mandela.
Ninapoyatafakari matibabu ghali niliyopata nchini Afrika Kusini kwa
msaada wa mwajiri wangu na safari yako nchini Marekani, vinanikumbusha
swali la mmoja wa wasaidizi wangu hapa ofisini aliyetaka kujua ni sababu
gani hasa ambazo zimekuwa zikisababisha wasomi na viongozi wetu
kuchunguzwa na kutibiwa katika hospitali za nje, tofauti na ilivyokuwa
kwa Madiba ambaye kwa nyakati zote tangu afya yake ianze kumtatiza
alikuwa akipata matibabu huko huko kwao Afrika Kusini?
Niseme kweli, japo nilikuwa na jibu au majibu ya swali lake, sikuwa na
maelezo ya kutosheleza yaliyokuwa na mwelekeo wa kukata kiu ya swali
lake, ingawa kwa kupapasa nilifanya kila juhudi kuutetea utaifa wangu na
viongozi wake ilhali miye mwenyewe nikiendelea kukosa raha kwa namna
nilivyokuwa nikitoa majibu ambayo yalikuwa yakionyesha hali ya kuukubali
unyonge, kukiri ufukara, kuficha udhaifu wetu kama taifa na kutetea
makosa ambayo aghalab ninyi viongozi wetu na wale wa kabla yenu mngeweza
kuwa watu mliostahili kuwa na majibu halisi.
Rais wangu,
swali na majibu vilisababisha kimoyomoyo, nijiulize maswali mengi
mengine na moja ya maswali hayo yakiwa ni wapi tulipopotea njia hata
tukafikia hatua ya kusababisha kuwa na kundi kubwa la watu waliokata
tamaa, wanaoteswa na ufukara, ukosefu wa ajira na kila aina ya kero na
karaha zinazozonga maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa
Rais, hali hiyo ilinipeleka moja kwa moja nchini Afrika Kusini na
hususan katika Hospitali ya Milpark ambako huko ndiko miye mwenyewe na
Watanzania wenzangu wengine tulikonusuru maisha yetu, huku baadhi kama
ilivyo kwa Dk. Sengondo Mvungi wakipoteza maisha yao baada ya kukimbizwa
huko.
Mheshimiwa Rais, naomba unisamehe kwa kulisema hili
nitakaloliandika hapa kwamba, jibu nililolipata haraka haraka kuwa moja
ya chagizo la matukio ya namna hii kutokea, halikuwa jingine bali ni
kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa viongozi wetu hususan wale tuliowapa
dhamana ya kuongoza sekta kadhaa nyeti kama ya afya na ustawi wa jamii.
Ushahidi wa kupwaya huko kwa viongozi hususan wale walio chini
yako, ndiko huko huko ambako kumedhihirika pia wiki iliyopita bungeni
Dodoma, ambako tulishuhudia zahama nyingine iliyowang’oa madarakani
mawaziri wako muhimu wanne kwa sababu kama hizo hizo za mkwamo wao au
watendaji wa chini yao katika kusimamia ipasavyo na kuchukua hatua kwa
wakati, kila yatokeapo matatizo yanayogusa maeneo wanayoyaongoza.
Nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu, mheshimiwa Rais iwapo
nitaficha shauku ya moyo wangu ambayo ilikwenda sambamba na tukio lile
la Dodoma lililowagusa baadhi ya mawaziri ambao anguko lao linaweza
likaelezwa kuwa ni ‘ajali ya kisiasa’ nikitumia msamiati ulioutumia wewe
mwenyewe kwa mara ya kwanza ulipozungumzia tukio la kujiuzulu kwa
waziri wako mkuu wa kwanza, Edward Lowassa.
Haja ya moyo
wangu, nikiwa mhariri, mwanahabari, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF) na mdadisi wa kawaida tu wa mambo, ilikuwa kuona anguko
la namna hiyo hiyo likimfika Waziri wa Habari ambaye amethibitisha
pasipo na shaka kuwa pamoja na kuwa msomi wa Shahada ya Falsafa (Phd),
ni kiongozi asiyejua anachofanya kwa kiwango cha kuwa mtu ambaye vichwa
vya watu wengine ndivyo vinavyofikiri kwa niaba yake.
Nilitamani afikwe na zahama hiyo si kwa sababu ya kuwa na hasira au
kumchuria mabaya, bali kwa kuzingatia ukweli kwamba yeye ni mtu ambaye
bado anasongwa na matongotongo ya mfumo wa kibabe wa zama za magazeti ya
Serikali na yale ya chama tawala, ambayo yanalazimika kuandika yale tu
yanayofurahisha nyoyo na akili za watawala.
Mheshimiwa
Rais, ingawa natambua na kuheshimu ukweli mchungu kwamba, suala la nani
awe waziri na nani asiwe ni jambo la wewe mwenyewe kupenda na kuchagua
na kwamba ulishasema mapema kabisa mbele yetu kwamba urais wako hauna
ubia, bado naamini pia kwamba, wewe ni mtu msikivu na mkweli uliye
tayari kusikia na kustahimili mambo mengi machungu unayokabiliana nayo
kila siku.
Kwa sababu hiyo, basi napenda kukueleza kwa
kuweka kumbukumbu sahihi ili mbele ya safari kabla na baada ya kumaliza
urais wako uje kuyatafakari na kuukumbuka ushauri huu kwako kwamba,
waziri uliyempa dhamana ya kulea na kuendeleza vyombo vya habari, ni mtu
wa kuhofiwa, jeuri, mwenye kiburi, asiyeshaurika na dikteta
asiyekutakia mema wewe binafsi, vyombo vya habari, serikali yako na
taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa rais sijui kama unajua kwamba
tangu umteue amefanya kazi na vyombo vya habari vya umma na hata baada
ya sisi kufanya juhudi kubwa ya kuwa karibu naye kikazi kwa makusudi na
kwa ujeuri mkubwa, amekataa wito na kupuuza maoni na ushauri wetu na kwa
namna ya kusikitisha amesikika akitamba waziwazi kwamba anao uwezo wa
kulifungia au kulifutia usajili gazeti lolote ambalo ataliona linakwenda
kinyume cha maadili ya uandishi wa habari.
Waziri huyu
ambaye alitarajiwa kuwa na silika za kuwa mlezi bora kutokana na jinsia
yake na historia yake ya kupata kuwa mwanaharakati kabla ya kuingia
serikalini, ndiye ambaye mamlaka makubwa uliyomtwisha, ameyageuza na
kuwa mwavuli wa kuvisulubisha vyombo vya habari vyenye uthubutu wa
kukosoa serikali na kuandika ukweli mchungu ambao asingependa kuona
ukiripotiwa.
Mheshimiwa Rais, pengine baya zaidi kwa tasnia
hii ni kwamba waziri huyo ana bahati mbaya ya kuwa na mmoja wa
wasaidizi na washauri wake katika sekta yetu ya habari ambaye naye,
hulka zake tangu aingie katika tasnia ya habari amekuwa ni mtu wa
kujipendekeza, kupenda makuu, kuzusha na kutokuwa na mawazo huru. Huyu
si mwingine bali Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO).
Ni jambo la bahati mbaya kwamba waziri huyu msomi pengine kwa sababu ya
kutojua vyema rekodi na historia ya msaidizi wake huyo, ambaye japokuwa
naye pia ni mteule wako, amejikuta akiwa mhanga wa fikra pandikizi
zinazopenyezwa wizarani chini ya uratibu mahususi unaofanywa na baadhi
ya wateule wako ambao wameshaanza kujipanga kusaka urais baada ya wewe
kustaafu.
Mheshimiwa Rais, nimelazimika kuyasema yote haya
baada ya kula kiapo cha moyoni huku nikirejea mafunzo tuliyokuwa
tukikaririshwa utotoni chini ya imani ya wana TANU, ambayo hata sisi
ambao hatukuwa wanachama wa chama hicho tulilazimika kuikariri kwa
kuitamka kila kukicha; ‘Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.’
Rais wangu, gazeti la MTANZANIA limerejea tena mitaani. Japokuwa ni
rahisi kuhesabu miezi, napenda kukueleza kwamba, ilikuwa ni miezi
mitatu michungu sana kwetu kihisia na katika hali halisi.
Nitakuwa mzushi sawa sawa na hao ninaowashangaa leo, iwapo nitasema
kulikuwa hakuna hitilafu au makosa ya kiuandishi ambayo yaliwapa
kisingizio cha mikakati waliyoipanga mapema kabisa, wasaidizi wako hao
kwa kulifungia gazeti letu hili.
Mheshimiwa Rais, nasema
haya kwa sababu ni ukweli ulio bayana kabisa kwamba, habari
zilizoandikwa na kutoa mwanya kwa serikali yako kutuadhibu gazeti hili,
hazikulenga kuchochea na wala hazikuchochea kabisa chuki yoyote dhidi ya
yeyote na mamlaka unazoziongoza kwa namna na kwa njia yoyote ile.
Siyo siri hata kidogo, mkurugenzi aliyetangaza uamuzi huo alifanya
hivyo akijua watu wengi hawajui mapito na dhamira yake. Tunajua yeye
alimshauri vibaya waziri na serikali huku akijua vyema kwamba, yuko hapo
alipo kwa maelekezo mahususi ya kundi la watu wenye malengo binafsi
ambao mheshimiwa rais, niko tayari wakati wowote na mahali popote
kukueleza kwa kina na kwa undani ili wakati utakapotaka kuchukua maamuzi
ya haki na kweli ujue undani halisi wa mambo haya.
Leo hii
wakati tukirejea tena sokoni, tayari tumeshasikia kuendelea kuwapo kwa
mikakati ile ile ya kuhakikisha gazeti hili na jingine ambalo halipendwi
na watu hao hao kwa sababu binafsi yakiinaingizwa tena mtegoni na
kufungiwa kifungo kingine kama hiki tulichomaliza au kinachofanana na
kile kilichoifika MwanaHalisi.
Mheshimiwa Rais, naandika
waraka huu nikikumbuka semi zako mbili unazotumia; ‘tunajenga nyumba
moja kwanini tugombee fito?’ na ile ya ‘akili za kuambiwa changanya na
zako’ ambazo kwa muktadha wa waraka wangu huu kwako zinaweza zikawa za
msaada sana kwako na pengine kwetu sisi wa MTANZANIA ambao tunashangilia
kurejea mtaani kwa gazeti letu lililodhulumiwa fursa ya kuchapwa kwa
muda wa siku 90.
Nimelazimika kukutumia wewe Rais si kwa
lengo la kuchosha akili zako au kukupotezea muda, isipokuwa kwa kutambua
hadhi, heshima na mamlaka makubwa uliyonayo juu ya wateule wako hao
ambao wameamua kwa sababu ya jeuri za kimamlaka walizonazo kuumiza watu
na kutupa sifa na majina mabaya tusiyostahili. Hakika wazungu walikuwa
sahihi waliposema ‘power currupts’.
Mheshimiwa Rais,
lingekuwa ni jambo la kheri kwa Serikali na kwa taifa letu zima iwapo
kusudi la kufungia magazeti linalopangwa na wateule wako kuwa utamaduni
wa kudumu, lingekuwa ni kujenga mustakabali mwema kwako wewe binafsi,
chama chako, Serikali unayoiongoza na nchi yetu kuliko hili la sasa
lenye dhamira ya kufunga watu midomo, kutesa, kuzusha na kuharibu
taswira yetu kama watu binafsi, taasisi na taifa.
Ni kwa
sababu hizo, mheshimiwa Rais ndiyo maana baada ya kusukwasukwa na moyo
na kuumizwa mno kifikra nikaona nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu na
haki za maelfu ya Watanzania ambao tunaamini wanahitaji huduma ya
magazeti haya katika kukidhi mahitaji yao muhimu ya kimaisha, kielimu na
kiufahamu kila kukicha na kuacha dhamira hizi za kishetani zikiendelea
kuongoza sekta yetu.
Mheshimiwa Rais, siyo siri hata kidogo
kwamba, ingawa mawazo hasi dhidi ya uhuru wa kikazi na kiwajibikaji wa
vyombo vya habari na wanahabari yanaonekana kutawala kauli na maamuzi ya
baadhi ya viongozi na washauri wako kwa kiwango cha kukushawishi hata
wewe binafsi kukubaliana nayo, ukweli ni kwamba, nyuma ya maneno matamu
wanayotumia kutupaka matope, kutujeruhi na kutupa kila aina ya sifa
mbaya kuna ajenda za kutuharibia sisi, kukuharibia wewe, kukomoa,
kuumiza na zaidi kulikwamisha taifa.
Nitakuwa mhariri
nisiyewajibika, iwapo nitakaa kimya ilhali nikijua fika kwamba, leo hii
ndani ya wizara iliyopewa dhamana ya kulea vyombo vya habari, baadhi ya
wateule wako na watendaji wake wamekalia viti walivyonavyo si kwa sababu
ya kuwa kwao na uwezo kustahimili ukosoaji, au upeo wao wa kuchochea
maendeleo ya kitaaluma, bali kwa kuendeleza na kuyatumikia matakwa ya
utarishi wa kifikra na kimatendo.
Kwa waraka huu mheshimiwa
Rais, wakati tukikuahidi kwa dhati kabisa wewe binafsi na Watanzania
wenzetu kwamba, tutaendelea na kazi kwa kuzingatia miiko na maadili ya
uandishi wa habari, sambamba na kuheshimu sheria zilizopo, tunapenda
kuliweka hili bayana kwamba, tutakuwa wa mwisho kuwatii viongozi
dhalimu, madikteta, waliokosa utu na ambao kwao hila ndiyo msingi mama
wa kupotosha na kupindisha mambo kwa sababu tu ya kulinda maslahi na
malengo yao binafsi au yale ya makundi yenye hila.
Rais
wangu, nimeona nitakuwa mtu nisiyekutakia mema wewe binafsi na taifa kwa
ujumla, iwapo nitakaa kimya na kuruhusu fikra za kikaburu zikijijenga
vichwani mwa viongozi wetu.
Mheshimiwa Rais, tutakuwa
tumeshindwa kutimiza wajibu wetu kama wanahabari, wahariri na viongozi
iwapo tutahalalisha kwa sababu ya ukimya wetu majina mabaya tunayoitwa
leo na wateule wako kama wasaliti, wachochezi na wazushi.
Miye binafsi naamini kwa dhati kabisa kwamba iwapo wewe utaamua kwa moyo
na nia njema kulinusuru taifa letu na majahili hao walio ndani ya
Serikali yako, basi siku moja historia itakuja kuandika kwa usahihi na
ufasaha jina lako na letu..
Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment