Friday, December 27, 2013

Jairo, Nyoni wasafishwa kimyakimya

Serikali imewasafisha aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo huku ikimpandisha cheo aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali Deo Mtasiwa.
Nyoni alisimamishwa kazi pamoja na aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa  na wote kwa pamoja walikuwa na tuhuma za kutumia vibaya madaraka yao wakiwa watumishi wa umma.
Jairo kwa upande wake alisimamishwa kazi kutokana na kuchangisha fedha kinyume cha sheria kwa lengo la kusaidia mchakato wa kupitisha bajeti ya wizara yake, katika mwaka wa fedha 2011/2012 na sasa ameondolewa kwenye utumishi wa umma, huku Bunge likiwa bado halijapata taarifa ya utekelezaji wa maazimio yanayomuhusu.
jairo 
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Nyoni kwa sasa amerejea kwa mwajiri wake wa awali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akishikilia nafasi ya mmoja wa wakuu wa idara, huku Dk Mtasiwa akiwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Katibu Mkuu Kiongozi
 Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amelithibitishia gazeti hili kuhusu watumishi hao na kwamba taratibu zimefuatwa.
“Mimi ninachojua ni kwamba Blandina alikuwa mwajiriwa wa TRA na mkataba wake ulikuwa haujaisha… Siyo kwamba alikuwa na mikataba miwili, kwenye utumishi wa umma huwa kuna utaratibu wa kuazima watumishi wa umma.
Ndiyo maana unaweza kukuta mwanajeshi anatolewa jeshini na kupelekwa uraiani au mtumishi kutoka idara moja kwenda nyingine. Kwa upande wetu sisi tulishamwondoa kwenye ukatibu mkuu na kule TRA hakuwa na tatizo,” alisema Balozi Sefue.
Kuhusu Dk Mtasiwa alisema: Uteuzi wa Dk Mtasiwa ulikuwa wazi na hata alipoapishwa mambo yote yalitangazwa hadharani.” Aliendelea kufafanua kuhusu Jairo akisema: “Jairo alishaondolewa kwenye ukatibu mkuu, siyo mtumishi tena wa umma.” Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alimtetea Nyoni akisema kuwa amerudi kwenye ajira yake ya awali.
“Siyo kwamba ameajiriwa TRA, amerudi tu kwenye ajira yake ya zamani, alikuwa akifanya kazi hapa akaazimwa na sasa amerudi,” alisema Kayombo na kuongeza: “Kwani amefanya kosa gani? Kuna mashtaka yoyote aliyofanya unaweza kuyathibitisha?”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Bernard Mchomvu ambaye alisema Nyoni alishasafishwa na Serikali ndiyo maana wamempokea. “Yule aliazimwa tu na Serikali…Sasa kama Serikali imesham-clear sisi tutamkataaje?” alihoji na kuongeza:
“Kwa sababu sikumwomba huyo mtu, nimeambiwa kwamba huyo yuko safi mimi nifanyeje? Unajua watu wanafurahia wengine wakipata matatizo, hata kama mtu ameua, basi walete ushahidi. Hata unaposema nchi imejaa rushwa, ulete ushahidi… kama Serikali imeshamsafisha, ningemkataa ningekuwa mtu wa ajabu.”

No comments:

Post a Comment