Moshi. Wakili maarufu mkoani Kilimonjaro,
Elizabeth Minde, ameliomba Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania,
kuangalia upya sheria ya gharama za kufungua kesi mahakamani ambazo
alisema zimepanda mno na kusababisha wananchi wa kipato cha chini,
kushindwa kufungua kesi pale wanapoona haki yao imepokonywa.
Minde ambaye pia ni Mkurugenzi wa shirika
lisilokuwa la kiserikali la Haki za Binadamu, Usawa wa Jinsia na Msaada
wa Kisheria mkoani Kilimanjaro (Kwieco), alisema kupanda kwa gharama za
kufungua kesi, ni moja ya sababu za wananchi kushindwa kupata haki zao.
Alisema kwa sasa gharama za kufungua kesi kwa
baadhi ya mashauri, zimepanda na kwamba kesi moja inaweza kufunguliwa
kwa gharama ya kati ya Sh5,000 na Sh120,000 kiasi ambacho ni kikubwa kwa
mwananchi wa kipato cha chini.
“Wananchi wengi hasa wa pembezoni wanashindwa
kudai haki mahakamani kutokana na kupanda kwa gharama za kufungua kesi.
Ilikuwa Sh.2000 lakini sasa zimepandishwa bila kuangalia wananchi
watamudu vipi,” alisema.
Wakili huyo alisema kuna haja kwa Jaji Mkuu wa
Tanzania kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi wanaotafuta haki zao
mahakamani. Akizungumzia utendaji kazi wa shirika lake, Minde alisema
katika kipindi cha mwaka huu, shirika limefanikiwa kutoa huduma ya
ushauri wa kisheria kwa wananchi 2,011.
Pia alisema shirika limefanikiwa kuwajengea uwezo
wateja 513 katika kuandaa nyaraka za mahakama na vielelezo muhimu
vinavyohitajika mahakamani na kwamba watatumia ujuzi huo katika
kupigania haki zao
No comments:
Post a Comment