Akihubiri
katika Ibada ya Christmas kanisani Mwenge, Mtumishi wa Mungu Askofu Mkuu
Zachary Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship alisema kuwa
wametokea baadhi ya wanasiasa hapa nchini ambao wanajiona ni miungu watu
na kujaribu kuwazuia watu wengine hususani viongozi wa dini wasiongelee
mambo ya siasa kwa kigezo kwamba eti Biblia inasema ya Kaisari mpe
Kaisari na ya Mungu mpe Mungu, hivyo viongozi hao wa dini hawastahili
kuongelea au kujihusisha na mambo ya siasa. Akitolea ufafanuzi maneno
hayo alisema watu hao hawajui Biblia na wanajaribu kuwapotosha watu.
Alisema Yesu aliwajibu wanafunzi wake baada ya kuulizwa juu ya uhalali
wao (wanafunzi) wa kulipa kodi ya Kaisari wakati wao waliamriwa na Musa
kulipa kodi ya Mungu. Ndipo akawajibu kwamba ya Kaisari wampe Kaisari na
ya Mungu Wampe Mungu akimaanisha kwamba walipe kodi ya Kaisari na
walipe kodi ya Mungu pia kama walivyo amriwa (Luka 20: 21-25; Hesabu
31: 25-39). Hivyo yeye kama mtumishi wa Mungu hawezi kuacha kukemea
mahali penye uovu na atapongeza panapostahili kupongezwa.
Viongozi wa nchi na Rasilimali zetu.
Aliendelea kusema kuwa Tanzania ni nchi iliyo barikiwa sana kwa kuwa na
Rasilimali nyingi lakini wananchi wake ni maskini. Alisema, hii
inatokana na kuwa na viongozi ambao hawana maono ya kuwaletea wananchi
maendeleo badala yake wao wanajiangalia wenyewe na familia zao. Akasema
ndio maana mtu akipata uongozi anasema "ameula". "Kiongozi bora ni yule
mwenye kipaji cha kuzaliwa cha uongozi na sio vyeti vya darasani pekee.
Sio kila mtu anaweza kuwa Rais wa nchi, ni lazima tuhakikishe
tunamchagua kiongozi ambaye ana maono ya kututoa kutoka katika Umaskini
tulionao na kuleta maendeleo ya kiuchumi".
Siasa za chumbani, siasa haramu.
Askofu Kakobe aliwataka wanasiasa na wananchi kwa ujumla kudumisha umoja
wetu badala ya kuleta siasa za chuki. Alisema wako baadhi ya wanasiasa
ambao wamechoka kisiasa hivyo wanaleta propaganda za udini, ukabila na
ukanda. "Watu wanadiriki hata kusema chama fulani ni cha dini fulani,
eti hatutaki Rais atoke ukanda fulani. Hizi ni siasa haramu na
wanaoeneza propaganda hizo nao ni haramu".
Aliendelea kusema kuwa hatumchagui mtu au malaika wa kutupeleka Mbinguni
bali mtu wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya asali na maziwa kwa faida ya
wananchi wote. Aliwaasa wanasiasa waache siasa za chumbani za
kunyoosheana vidole kuhusu ndoa zao. "Tusiendekeze siasa za
chumbani,hatumchagui kiongozi wa kutupeleka mbinguni bali tunamchagua
kiongozi wa kutuletea neema hapa hapa Tanzania. Watu leo wanamsifia
Mandela kwamba alikuwa kiongozi bora lakini wanasahau kwamba Mandela
huyuhuyu maisha yake ya ndoa yalikuwa na kasoro kubwa. Aliweza
kuwasamehe makaburu lakini alishindwa kumsamehe mkewe Winnie. Ni nani
Kiongozi wa nchi hapa Tanzania anaweza kusema yeye ni msafi? Kwani sisi
atujui maisha ya JK? Tuache siasa za chumbani, tuchague kiongozi bora.
Pia Askofu Kakobe alishauri Chama Tawala kikubali uundwaji wa Tume Huru
ya Uchaguzi ili kuondoa malalamiko toka kwa vyama vya upinzani. Pia
alishauri siku ya uchaguzi mkuu isiwe Jumapili, Jumamosi au Ijumaa bali
serikali itenge siku yoyote katikati ya wiki ili wananchi wengi zaidi
waweze kujitokeza kupiga kura.
N.B:Tunaweza kujadili maoni ya huyu mtumishi wa Mungu kwa mustakabali wa Taifa letu.
No comments:
Post a Comment