Saturday, December 7, 2013

DR. SLAA AKIWA KIGOMA (ANGALIA PICHA & SOMA ALIYOTAMKA)

 








Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibroad Slaa ameendelea na ziara ya ujenzi na kukagua uhai wa chama, ambapo leo alikuwa na mikutano miwili kadri ya ratiba yake aliyopangiwa na wenyeji.

Mkutano wa kwanza ulikuwa Kijiji cha Mabamba, Jimbo la Muhambwe na mkutano wa pili ulikuwa mjini Kibondo, ambapo pamoja na mvua kubwa kunyesha watu wamejitokeza kwa wingi, wengine wakilazimika kusimama upenuni mwa maduka pembeni mwa Uwanja wa Community Centre, kumsikiliza Dkt. Slaa.

Akiwa kijijini Mabamba, Dkt. Slaa alitumia fursa hiyo kutoa salaam za rambirambi kwa msiba mzito wa Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, akimtaka Rais Jakaya Kikwete si tu kutangaza siku tatu za maombolezo bali serikali yake inapaswa kutafakari juu ya vitendo vya kikatili inavyowafanyia watu wake, kwa namna ile ile au zaidi ya walivyokuwa wakifanya makaburu wa Afrika Kusini.

Alisema kuwa kutangaza siku tatu za maombolezo wakati serikali inafanya vitendo vile vile ambavyo Mandela alivipinga kwa nguvu zote hadi akaitwa gaidi na kufungwa jela ni sawa na kumdhihaki Kamanda huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, akipigania haki na utu wa binadamu.

Aliongeza kuwa Mandela alikuwa mpigania haki ambaye hakusita kusimama na wananchi wake hata mara moja, akiwa tayari kufa kwa ajili hiyo, kiasi ambacho alibambikiwa kesi na kuitwa gaidi kutokana na sheria za kikandamizi zilizotungwa na makaburu.

"Hakuwa tayari kuwapigia magoti watawala wanaonyanyasa wananchi wasiokuwa na hatia kwa kutumia sheria mbovu, hakuwa tayari kuona watu wanafanyiwa ukatili. Aliwapinga makaburu kwa kila hali na mali. Tanzania tuliwaunga mkono wapigania uhuru wa Afrika Kusini. Wengine tukawatunza hapa kwetu, tukaanzisha undugu. Ndiyo maana nasema kwetu huu ni msiba mzito sana.

"Bahati mbaya mie huwa sipendi unafiki na kuzunguka zunguka, leo Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo. Nilitarajia serikali makini badala ya kuomboleza tu, ijitazame na kutafakari kama haifanyi matendo aliyokuwa akiyapinga Mandela. Leo hii sisi tuna ushahidi wa wazi, mabomu yanapigwa kwenye mikutano ya hadhara, vijana wetu wamesingiziwa ugaidi.

"Wamepigwa shoti za umeme, wameingiziwa vyuma na chupa sehemu za siri ili tu waseme Slaa na Mbowe waliwatuma. Ninyi hapa nasikia wanataka kuwahamisha bila hata kuwauliza, manyanyaso ya watendaji wa serikali na vyombo vya dola yako wazi, sasa haya si ndiyo walikuwa wanafanya makaburu na mengine hata tumeanza kuwazidi," alisema Dkt. Slaa akishangiliwa na wananchi.

Katibu Mkuu Dkt. Slaa pia amesisitiza kuwa kama CHADEMA kitashindwa kuchukua hatua za kukisaidia kujisahihisha, kisha kikaanza kupindisha hata misingi yake, ikiwemo kusimamia katiba yake, hakitaweza kufaa kukabidhiwa mamlaka na dhamana ya kuongoza dola.

Katika mazingira yanayofanana na yale ya jana mjini Kakonko, huku pia yakihusisha watu 'wale wale', leo kijijini Dkt. Slaa alilazimika kuingilia kati kuwazuia askari polisi waliokuwa wakiwazuia vijana takriban saba waliokuwa wamelewa huku wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali (ulioonekana kuandikwa kwa hati moja) wakidai wanapingana na maamuzi ya Kamati Kuu ya kumvua nafasi ya uongozi wa chama Ndugu Zitto Kabwe.

Dkt. Slaa aliagiza vijana wale wapishwe njia ili wasimame mbele kabisa asome vizuri ujumbe walioandika kwenye mabango yao, akisema hata wale ambao hawajaandika mabango lakini wana maswali ya kuuliza kuhusu jambo lolote, watapata fursa wakati wa 'maswali na majibu' atakapokuwa amepanda jukwaani kuzungumza na wananchi.

Alisema kuwa majibu yote ya masuala ya CHADEMA mbali ya kujadiliwa kwenye vikao rasmi vya chama, majibu yake yako ndani ya katiba, ambayo ndani yake kuna maadili, kanuni, itifaki na miongozo.

Vijana wale waliokuwa na mabango, walionekana kukataa kupigwa picha za mnato na video, huku baadhi yao wakiweka mabango yao kwa namna ya kuficha sura, hasa baada ya kubainika kuwa ndiyo 'wale wale' waliobeba mabango kwenye mkutano wa jana mjini Kakonko.

Baadae vijana wale badala ya kutumia fursa waliyopewa ya kusikilizwa, walianza kufanya fujo, jambo ambalo polisi hawakukubaliana nalo, hivyo wakaanza kuwasogelea kwa ajili ya hatua, ambapo Dkt. Slaa aliwaambia kama vijana hao wameshindwa kutumia demokrasia aliyowapatia na wanaanza kuvuruga mkutano huo, basi polisi wanajua wajibu wao katika hali hiyo.

Jumla ya vijana 11 walikamatwa na polisi kisha kwenda kufunguliwa jalada kituo cha polisi.

Dkt. Slaa alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa maeneo hayo kwa ujasiri wao wa kuchagua viongozi wa serikali wanaotokana na CHADEMA, wakiwemo wanawake, akiwataka kujiandaa kufanya mabadiliko makubwa mwaka 2014, kwani utakuwa mwaka wa ukombozi wa kweli kwani ikulu ya kwanza kwa wananchi ni Serikali ya Kijiji au mtaa.
Kwa hatua hiyo waliyokwisha kupiga katika mapambano ya awamu ya pili ya kutafuta uhuru wa kweli na mabadiliko ya kimfumo na kiutawala, Katibu Mkuu alitumia mrefu kuwaambia umuhimu wa ikulu ya kwanza ambayo ni serikali ya kijiji, kisha halmashauri ya wilaya, badala ya kuanza kufikiria ikulu ya magogoni.

Ili kufikia matumaini ya kupata ikulu ya kijiji kisha halmashauri ili hatimaye wapate uongozi bora na sera makini za CHADEMA wanahitaji kuendelea kujipanga kuimarisha chama katika maeneo hayo, kwa kutumia operesheni mbalimbali zinazoendelea ndani ya chama, hususan CHADEMA ni msingi, maandalizi ya uchaguzi wa ndani na mafunzo kwa viongozi.

Katibu Mkuu pia alizungumzia dhana ya haki na amani ndani ya nchi, akihusisha na mkutano uliopaswa kufanyika mjini Arusha ambao iwapo wanasiasa wa chama tawala wangelikuwa na dhamira ya dhati ungeweza kusaidia siasa za Arusha kufanyika katika misingi inayothamini haki, matumaini na utu wa mwanadamu badala ya kusimamia kiburi cha madaraka yanayopatikana kwa maguvu ikiwemo kumwaga damu za watu wasio na hatia.

Alisema kuwa katika majadiliano yoyote yale.


Kurugenzi ya Habari

Chanzo: http://chademablog.blogspot.com/2013/12/dkt-slaa-ziarani-mikutano-ya-desemba-6.html

No comments:

Post a Comment