Tuesday, December 24, 2013

Mgogoro wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CDM)

Mgogoro wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CDM) ambao umesababisha baadhi ya viongozi wake waandamizi kung’olewa, wengine kujiuzulu na kugawa makundi ya wanachama na kuhatarisha hata usalama wa viongozi wengine ni lazima ufikie tamati.

Japo ambao wanataka tuamini kuwa hakuna mgogoro si kwa sababu hatuuoni bali kwa sababu wanataka tusiutazame ni muhimu kuwa wakweli kwa nafsi zetu kuwa kinachoendelea na ambacho kimedumu muda mrefu ni mgogoro ambao umetishia umoja wa chama, umelegeza harakati za kuing’oa CCM madarakani na kwa hakika umeacha majeraha ambayo kwa siku kadhaa sasa yanazidi kutoneswa toneswa na jitihada za kuyaponya hazijafanyika zikatosheleza. Katika mfululizo wa makala yangu hii nitajaribu kushirikisha mawazo yangu kuhusiana na mgogoro huu. Kwa muda mrefu watu wengi – wa pande zote za mgogoro – wameniuliza maoni yangu kuhusu kinachoendelea CDM na kwa wote jibu langu limekuwa “bado nafikiri”. Ni kweli nilikuwa bado nafikiri kwa sababu naamini bila kutumia muda kufikiri kwa kina kuhusiana na tatizo, kulielewa chanzo chake na kulikabili lilivyo itakuwa vigumu kupata suluhisho la kudumu. Makala hii hadi hivi sasa ina sehemu nne – sidhani kama nitaifanya izidi sehemu tano; kwa wale wasiona mazoea ya kusoma maandishi mengi nashauri wanaweza kusubiri sehemu ya tatu nay a nne kuweza kuona mambo ambayo ninayapendekeza kufanyika. Lakini kwa wale ambao wanapenda kujua nilifikia vipi mapendekezo hiyo watajitendea hisani kunisoma toka mwanzo kuweza kuelewa msingi wa hoja yangu.

Katika Makala hii hasa hapo mbeleni nitajikita kwa kina kuonesha kwanini viongozi wakuu wa CDM ni sehemu ya mgogoro huu lakini pia ni wao ndio ambao wanaweza kuupatia suluhisho la kudumu; suluhisho ambalo litakuwa linatenda haki, linazingatia misingi ya kidemokrasia lakini pia suluhisho ambalo litasababisha wanachama wote kutambua kuwa kuelekea 2015 migogoro haikubaliki, haitavumiliwa na yeyote ambaye atakuwa sehemu ya mgogoro atashughulikiwa ipasavyo kwa staili ya kumkomo nyani giledi, mchana kweupe.

Katika sehemu ya kwanza nitaangalia nadharia ya nidhamu ya chama (party discipline), katika sehemu ya pili nitaangalia sehemu ya kwanza ya chanzo cha mgogoro, katika sehemu ya tatu nitaangalia sehemu ya pili ya chanzo cha mgogoro (ambayo inatokana na nadharia ya nidhamu ya chama) katika sehemu ya nne nitachambua viongozi wa CDM ambao naamini wamekuwa sababu ya mgogoro na kwa namna gani vyanzo vya mgogoro vimewaweka katika hili; katika sehemu ya mwisho (natumaini sitaenda zaidi ya hapo) nitaangalia namna ya kuutatua mgogoro huu kwa kutoa mapendekezo ambayo ni ya kuthubutu, yasiyo angalia sura na ambayo hayana haja ya kuomba radhi kabla ya kuyatoa.

Matumaini yangu ni kuwa hoja nitakayoiweka hapa itatoa pendekezo bora zaidi la kumaliza mgogoro CDM (na wengine wanaweza kujifunza) kuliko mapendekezo mengine yote yaliyowahi kutolewa na wengine kabla.

Fuatana nami katika sehemu ya kwanza.

NADHARIA YA NIDHAMU YA CHAMA (Party Discipline Theory)

Mambo haya matatu yanatusumbua sana na yanaligharimu taifa. Yanatusumbua kwa sababu hayaonekani kumalizika bali yanaonekana kama kuzidi na kuzidi kila siku iitwayo leo; na yanaligharimu taifa kwa sababu matokeo yake kwa ujumla wake kwenye uongozi na utendaji wa taifa letu ni hasi. Ukiangalia kwa karibu mambo yanayoendelea ndani ya chama tawala na kwenye chama kikuu chaupinzani nchini – CDM – mambo haya yameota mapembe ambayo kwa kweli hayakatiki, hayakatwi bali zaidi yanaonekana kuchongwa.

Mfano wa Jeshi

Jeshi lolote duniani ambalo limeundwa kwa ajili ya kutoa ulinzi na kupigana vita linahitaji vitu hivi vitatu kama nguzo zake kuu za kiutendaji ili kuweza kupata ushindi vitani. Majeshi yote duniani kati ya vitu ambavyo wanamfundisha askari mtarajiwa (kuruta) ni kuwa na nidhamu, kutii mamlaka iliyo juu yake na kutotumia madaraka vibaya. Makuruta wanapojiunga na jeshi wanatoka katika mazingira tofauti, wana tabia tofauti na wana mitazamo tofauti; kazi ya kwanza ya wakufunzi wa kijeshi (drill sergeants) ni kuwatengeneza hawa watu kutoka walivyokuwa na kuwapeleka wanakotakiwa kuwa.

Kwa wale tulioshuhudia kwa karibu Vita ya Kagera na harakati za Ukombozi wa Nchi zilizoko Kusini mwa Afrika tunajua ni kwa kiasi gani jeshi letu lilijipatia heshima katika kushiriki mapambano, kutoa mafunzo na kulinda usalama wa nchi yetu. Kiasi kwamba tulijiaminisha kuwa jeshi letu ni mahiri kabisa katika eneo letu hili. Kutokana na ujuzi huo tumekuwa na kiburi cha ufahari wa jeshi letu; ndio maana tunapochokozwa na majirani zetu hatuchelewi kuanza kushadadia vita na mapambano kwa sababu tunaamini kabisa kuwa katika eneo letu hakuna nchi ambayo inaweza ikaingia vitani na sisi ikatupiga; siyo Malawi, siyo Rwanda wala siyo nani.

Siri ya mafanikio haya ya jeshi letu ni nini hasa? Je ni kwa sababu tumewekeza kwa kiasi kikubwa katika vifaa vya kijeshi? (hili si kweli); je inawezekana ni kwa sababu tuna silaha za kisasa zaidi kuliko wengine? au kwa sababu sisi ni Tanzania kana kwamba kwa kuwa Tanzania basi automatically jeshi letu ni bora zaidi? Au kuna siri kubwa zaidi na ya msingi?

Naomba kupendekeza kwa msomaji kuwa siri ya mafanikio ya jeshi lolote duniani (likiwemo la kwetu) imelala kwanza kabisa katika nidhamu (discipline). Jeshi lisilo na nidhamu haliwezi kushinda vita hata kama lina silaha, wataalamu au mabilioni ya pesa. Vitu vingine ni muhimu sana katika kufanikisha mapambano lakini hakuna kitu muhimu kama kuwa na wapiganaji walio na nidhamu iliyopitiliza; ambao wanatambua majukumu yao barabara na ambao pamoja na makamanda wao wako moyo mmoja kutafuta ushindi. Hakuna brigedi, hakuna kikosi, hakuna company ambayo inaweza kusimama peke yake au kujifanyia mambo yake kwa ajili ya sifa zake yenyewe. Jeshi lote na sehemu yote chini ya majenerali husika ndio linaenda kutafuta ushindi. Jeshini hakuna sifa ya kikosi moja au kapteni mmoja!

Nidhamu na Demokrasia

Mojawapo ya mambo ambayo yananitatiza siku za karibuni – hasa kufuatia mgogoro wa ndani wa CDM – ni ile imani ya baadhi ya watu kuwa demokrasia na nidhamu haviendani (the incompatibility of democracy and party discipline). Kwamba, katika nchi ya kidemokrasia vyama vya siasa haviitaji kuwa na nidhamu ya ndani kwani kuweka nidhamu au kusimamia nidhamu ni kuminya au kufinya demokrasia. Wenye kuamini hivyo ni wepesi kuona tishio kwa demokrasia wakati wowote chama cha siasa kinapojaribu kusimamia nidhamu ndani yake.

Matokeo yake ni kuwa wanasiasa – viongozi na wasio viongozi – wanajaribu na wengine wameshajaribu kufanya mambo bila kujali chama chao cha siasa. Kwamba, kwa vile mtu ana mawazo Fulani basi yuko tayari kuyafanyia kazi mawazo hayo (haijalishi kama ni mazuri au la) bila kujali, kukihusisha au kupata kuungwa mkono na chama chake. Hili linasababisha tujiulize swali la msingi kweli; je ni kweli kwamba demokrasia na nidhamu haviendani pamoja?

Naomba kupendekeza kwa mpendwa msomaji kuwa bila nidhamu demokrasia haiwezi kuchipuka, kustawi na kuzaa matunda. Nidhamu ni gundi inayokishika chama pamoja na siyo chama tu bali jumuiya yoyote ya watu ambao wameamua kuunganisha nia zao ili kufikia lengo moja. Hili ni kweli kwenye kwaya, bendi ya muziki, timu ya mchezo, na ukiangalia sana hata kwenye familia. Wakati wowote kunatokea kukosekana kwa nidhamu basi kikundi hicho cha watu kitaanza kuwa na nyufa, misukosuko na kama wahusika hawatawajibika ipasavyo basi kikundi au jumuiya ya watu inaweza kabisa kuparaganyika. Hapa basi kuna haja ya kuielewa hii nidhamu ya chama (party discipline)

Nidhamu ya Chama Ni Nini Basi?

Hii inaweza kutafsiriwa kama mfumo na utaratibu unaotumiwa na chama cha siasa kuhakikisa kuwa wanachama (viongozi na wasio viongozi) wanafuata msimamo wa chama badala ya kufuata tu vitu vingine ambavyo navyo vyaweza kuwa vya muhimu. Katika nchi zenye utawala wa kidemokrasia nidhamu ya chama ni utaratibu wa kichama wa kuhakikisha kuwa watendaji na viongozi wanaotokana na chama cha siasa wanazingatia na kufuata misimamo, misingi, itikadi na mwelekeo wa chama.

Kama nilivyosema hapo juu, lengo la kuwa na nidhamu ya chama ni kuhakikisha kuwa chama kinasimamia malengo yake na hatimaye kuhakikisha kuwa kinayafikia malengo hayo. Mgawanyo wa Nidhamu ya Chama

Naweza kuigawa hii nidhamu ya chama katika makundi makubwa matatu.

a. Nidhamu ya Wanachama kwa Chama

Kila mwanachama anapojiunga na chama cha siasa anakuwa amekubali malengo, nia, na madhumuni ya chama hicho. Katika kukubali mambo hayo mwanachama anakuwa amekubali kufuata Katiba ya chama, taratibu zake na miongozo yake. Hii ndiyo sababu mtu anachukua kadi ya chama na kuilipia; anaonesha kukubali kwake yaliyomo ndani ya Katiba hiyo. Kimsingi, anakuwa amekubali kufungwa na Katiba hiyo. Hili ni kwa kila mwanachama. Hivyo, kila mwanachama bila kujali uwezo wake, hali yake ya kimaisha, jinsia yake n.k anatazamiwa kufuata Katiba ya chama, taratibu zake na uongozi wake.

Kila mwanachama anapaswa kuwa na nidhamu kwa chama chake; kuanzia tawi alipo hadi ngazi za juu za chama chake. Kwa upande wa CDM Mwanachama ni lazima akubaliane na Katiba, Itikadi, na Kanuni za chama kwa mujibu wa Ibara ya 5.1.4 na 5.1.5 ya Katiba ya CDM.

b Nidhamu ya Wanachama kwa Viongozi na Viongozi kwa Wanachama

Chama cha siasa ili kiweze kusonga mbele kinahitaji kuwa na nidhamu ya viongozi kwa viongozi na viongozi na wanachama wao. Hii ina maana ya kuwa wanachama wanakuwa tayari kufuata uongozi na viongozi wanatarajiwa kuwaongoza wanachama wao vizuri na kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa wazi. Bila ya nidhamu ya aina hii kila mwanachama atakuwa kiongozi na kile kiongozi atakuwa na wanachama wake. Ni lazima kuwe na nidhamu ya aina hii ili kuhakikisha kuna utulivu, umoja, na ufanisi katika utendaji kazi au katika kusimamia majukumu mbalimbali. anatazamiwa kufuata Katiba ya chama, taratibu zake na uongozi wake.

Wanachama wanatakiwa kuwa na nidhamu ya kukubali kuongozwa; ndio maana ya kuwa na viongozi. Wanachama wasiokubali kuwa chini ya uongozi ulio halali juu yao ni sawasawa na kuwa na kundi la mifugo lisilokubali kuchungwa. Mfano huu waweza kuelezea vizuri haja ya kuwa na nidhamu kama kundi; mchungaji mzuri anajua jinsi ya kulinda mifugo yake, kuipatia lishe nzuri, kuhakikisha ina afya na inaongezeka na hatimaye kumpatia faida. Mchungaji ambaye kila wiki anachinja mifugo kwa ajili ya kufurahia tu au anauza kwa bei chee au haipi matunzo yanayostahili ni mchungaji wa hatari.

Uongozi ni hivyo hivyo; viongozi wanatakiwa kutoa uongozi mzuri kwa wale wanaowaongoza na wale wanoongozwa kukubali kuongozwa vizuri. Wanachama wasiopenda kuongozwa na wanaojifanya na wao ni viongozi wakati siyo ni sababu moja ya kukosekana kwa nidhamu. Mwanachama anayeamini anaweza kuongoza vizuri zaidi kundi anapewa nafasi katika uchaguzi kuwashawishi wanachama wenzake kumpa uongozi. Kabla ya hapo anatakiwa awe na nidhamu kukubali kuongozwa.

Viongozi nao hata hivyo kwa vile ni viongozi haina maana wanaweza kuongoza vibaya wakaachwa; ni lazima waoneshe kuwa na nidhamu ya kuongoza vizuri makundi yao. BIla kufanya hivyo watajikuta wanapata shida kusimamia wale wanaowaongoza na matokeo yake wanaweza kusababisha uasi katika kundi.

c. Nidhamu ya Viongozi kwa Viongozi

Kila chama kina ngazi mbalimbali za uongozi; kuna viongozi wa ngazi za chini, wapo wa ngazi za kati na wapo viongozi wa ngazi za juu. Japo wote wanaitwa viongozi lakini kimsingi uongozi wao ni katika maeneo ambayo wamepewa uongozi na si vinginevyo. Katika elimu ya uongozi hii inaitwa ‘ngazi za uongozi/madaraka’ (leadership hierarchy).

Ngazi za Madaraka katika demokrasia zinatoa nafasi kwa watu mbalimbali kushika uongozi katika ngazi mbalimbali na wakati huo huo kuweza kupata nafasi ya kusonga mbele katika nafasi nyingine zenye majukumu makubwa zaidi. Ni wazi kuwa kwa kadiri mtu anapanda ngazi hii ndivyo anavyozidi kukuta kuwa huku juu nafasi zinazidi kupunguza zaidi. Ndio maana uongozi wa kisiasa unakuwa kama pembetatu fulani hivi ambapo nafasi kubwa za kushika uongozi wa aina mbalimbali ziko chini kuliko juu.

Kwa mujibu wa Katiba ya CDM Ibara ya 7; Muundo wa chama unaanzia ngazi ya Msingi na kuishia Ngazi ya Taifa. CDM ina ngazi zifuatazo za muundo wa chama.

1. Msingi/Vitongoji
2. Tawi
3. Kata/Wadi
4. Wilaya
5. Mkoa
6. Jimbo/Kanda
7. Taifa

Hata hivyo ukizingatia tangazo la hivi karibuni la uchaguzi wa ndani wa chama yawezekana kukaonekana kuwa kuna utata wa muundo huu wa chama hasa linapokuja suala la Kanda na Majimbo. Kwa mujibu wa tangazo la chaguzi hizo kuanzia 1-10 Aprili 2014 kutafanyika chaguzi za majimbo na tarehe 9 Julai utafanyika uchaguzi wa Kanda.

Kwa mujibu wa ufafanuzi wa maneno katika Katiba ya CDM “Majimbo” kimsingi ndio “Kanda”. Katiba inatafsiri Majimbo kuwa ni “mkusanyiko wa mikoa yenye mahitaji yanayofanana kiuchumi kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu.” Sasa ama kuna kurudia rudia chaguzi au majimbo kama yalivyotajwa kwenye suala la uchaguzi siyo kanda kitu ambacho kitatufanya tuulize ni nini hasa? Kama ni majimbo ya uchaguzi (constituencies) basi Katiba ya CDM haina ngazi hizo kwani Ibara ya 7:6 inapozungumzia majimbo inazungumzia kwa maana hiyo hapo juu isipokuwa kama kutatolewa ufafanuzi wa mahusiano ya kiutendaji kati ya majimbo ya uchaguzi na majimbo ya kanda. Hii ni kwa sababu katika suala la uchaguzi ‘uchaguzi wa majimbo’ umewekwa kabla ya uchaguzi wa Wilaya na ule wa Mikoa na baada ya uchaguzi wa matawi kitu ambacho kinanifanya niamini kuwa uchaguzi uliosemwa ni wa “majimbo” ni uchaguzi wa ngazi ya Kata/Wadi na sio jimbo kwani jimbo ni kanda.

Katika ngazi hizi zote – kuanzia vitongoji hadi taifa; kutakuwepo na watu ambao wataomba nafasi ya kutumikia chama chao katika ngazi hizo za uongozi; wakati huo huo wao wenyewe watakuwa wanajiweka chini ya uongozi ule wa juu yao. Hii ndio ngazi ya uongozi; kila kiongozi wa chini anatakiwa kuwa na nidhamu na viongozi wa juu na wale wajuu wanasimama na kuwajibika kwa walio chini yao.

Nidhamu ya Chama ni Suala la Vyama vya Kijamaa?

Mtu anaweza kusema kuwa suala la nidhamu ya chama ni suala la vyama vya kijamaa; kwamba katika demokrasia au mfumo wa vyama vingi vyama vya siasa havitakiwi kuweka mkazo sana katika nidhamu; kwamba nidhamu inadumaza na kudunisha ukuaji wa demokrasia. Hivyo, katika fikra za baadhi ya hawa wanaweza kuona kuwa kila mtu kujifanyia, kujiamulia au kujiendea kivyake vyake katika chama ni sehemu ya demokrasia.

Hii si kweli. Wanasayansi wa elimu ya siasa wa nchi za kidemokrasia wameandika vya kutosha juu ya umuhimu na hata ulazima wa nidhamu ya chama. Nchi zenye muda mrefu katika demokrasia ya vyama vingi kama India, Australia, Uingereza, Marekani, New Zealand, Canada n.k zinatumia nidhamu ya chama katika kuhakikisha kuwa wanachama na viongozi wanakuwa katika mstari mmoja na wanakuwa katika lengo na mwelekeo mmoja wa kichama. Kwa Marekani hata hivyo mfumo wa nidhamu ya chama hauna nguvu sana kama ilivyo Canada, India, Japan au Uingereza na Australia. Kuna sababu za Kikatiba kwanini mfumo wa nidhamu ya chama Marekani ni dhaifu kulinganisha na nchi nyingine.

Manufaa makubwa kabisa ya mfumo na usimamizi mzuri wa nidhamu katika chama ni kukiandaa kushika madaraka na kutimiza ajenda yake ya uchaguzi kwa ufanisi, weledi, umoja na kuhakikisha matokeo yake yanakuwa mazuri.

KUUELEWA MGOGORO WA CHADEMA NA KUUMALIZA KUELEKEA 2015 - 2

VYANZO VYA MGOGORO

Kwa karibu miaka kadhaa sasa ndani ya chama kikuu cha upinzani nchini CDM kumekuwepo na mvutano wa ndani baina ya makundi mbalimbali. Mvutano huu ambao wakati mwingine umekuwa ukilaumiwa chama tawala cha CCM ni muhimu kueleweka ili hatimaye suluhisho la kudumu, kamili na thabiti liweze kufikiwa. Mgogoro uliopo ni vizuri kuelewa sio mgongano wa kiitikadi au kifikra; angalau sivyo unavyojionesha hivyo. Karibu wote wanaogongana na ambao wamewahi kugongana utaona kuwa hawagongani kwa vile wanatofautiana sana kiitikadi au sera za Chama kiasi kwamba mmoja anataka kubadilisha sera za mwingine. Ukiumulika kwa karibu utaona kuwa mgogoro huu unahusisha watu zaidi (personalities) kuliko fikra au itikadi. Chacha Wangwe dhidi ya Mbowe, Slaa dhidi ya Zitto na kinyume chake, kundi la vijana dhidi ya Mbowe au Dr. Slaa; na wengine dhidi ya Zitto n.k. Na hili ni kweli siyo kwenye ngazi za juu tu za chama bali pia tumeona kwenye ngazi za chini kama ilivyotokea Mbeya, Mwanza, Arusha n.k

Mgogoro huu wengine wanaweza kuuona pia ni mgogoro wa kimaslahi zaidi ambapo watu mbalimbali wanatafuta maslahi fulani zaidi huku wengine wakitaka kuendelea na maslahi fulani. Kama ni maslahi binafsi au ya chama au ya taifa hili ni jambo jingine lakini wao wenyewe wanaogongana kila mmoja anajaribu kusema anatetea maslahi fulani. Kama ni kweli ni mgogoro wa maslahi au maslahi yana sehemu zake kwangu si la maana sana; la maana katika hoja yangu ni kuwa mgogoro huu upo, umekuwa mkubwa (umekuzwa) na hatua ambazo zimechukuliwa hadi hivi sasa naamini hazitoshi kuumaliza kabisa. Lakini kabla hatujazama zaidi kuuelewa mgogoro huu naomba nioneshe kwanini mgogoro huu upo.

Kwanini kuna Mgogoro CDM?

Naomba kupendekeza kwa msomaji kuwa mgogoro uliopo CDM una vyanzo viwili vikubwa. Chanzo cha kwanza kikiwa Nina uhakika wapo wanaofikiria kuwa mgogoro huu chanzo chake ni ‘watu’; mimi naomba kutafutiana nao. Ni rahisi kutaja majina ya watu kama vyanzo vya mgororo lakini naamini mgogoro uliopo ni zaidi ya watu. NI sawasawa na watu wanaofikiria kuwa tatizo la utawala wa CCM ni watu kuwa wakibadilisha watu basi utawala utakuwa mzuri na kweli kwa miaka 52 sasa CCM imeendelea kubadilisha watu na namna ya utawala imeendelea kuwa vile vile. Nchi imekuwa na marais wanne, mawaziri wakuu 9 (na wapo wengine Bungeni wanataka waziri mkuu wa 10!); mawaziri wa nishati na umeme lukuki, kwenye afya wengi tu, elimu ndio usiseme kabisa!

Mtu yeyote anayetaka kufiriki vizuri ni lazima ajiulize; kama tunabadilisha watu hivi kwanini namna ya utawala haibadiliki? Je inawezekana kuwa tatizo ni zaidi ya watu? Binafsi naamini tatizo la mgogoro wa CDM kama ule ulioko CCM (ambao kwa leo naomba niuache kwani nilishawahi kuandika na mapendekezo yangu kuyatoa miaka kadhaa nyuma) lina sehemu kubwa tatu na kuzielewa sehemu hizo mbili au vyanzo hivyo viwili ndio njia pekee ya uhakika ya kuweza kuondoa mara moja na daima mgogoro huu bila kujali sura, majina, hadhi, ujiko, na vyeo vya wahusika. Vyanzo vya mgogoro ndani ya CDM ni vya pande tatu; upande mmoja ni mfumo na muundo wa chama, upane mwingine ni ukosefu wa nidhamu ya chama na upande wa tatu ni sheria ya vyama vya siasa (na Katiba ya sasa).

Hili la tatu hata hivyo siyo somo ambalo nitalizungumzia kwenye Makala hii kwani kwa wengi labda ni rahisi kueleweka zaidi kuliko haya mengine mawili. Na katika mada yangu hii kubwa ambalo nitazama ndani kidogo ni kuliangalia sana ni hilo la pili – la ukosefu wa nidhamu; la kwanza nitaliangalia kama kidokezo tu lakini pia kwa sababu litaganya hili la pili liwe bayana zaidi.

Mfumo na Muundo wa Chama

Mfumo na Muundo wa chama ni kama jukwaa ambalo juu yake wachezaji mbalimbali wanasimama. Jukwaa linalotaka kusimama mtu mmoja hutengenezwa kwa ajili ya mtu mmoja, jukwaa la kikindi kidogo huwa dogo vile vile; jukwaa ambalo linatarajiwa kuwa la kundi kubwa la watu, vifaa na vitu mbalimbali huwa kubwa na kila mojawapo hujengwa kwa kuhakikisha kuwa linakuwa imara. Jukwaa ambalo litachukua watu zaidi ya uwezo wake linaweza kuvunjika na kusababisha madhara makubwa. Jukwaa ambalo watu watakuwa wanaruka ruka n.k ni lazima liwe na uwezo mkubwa, kinga za kutosha na lililojengwa kwa ustadi mkubwa. Kile kinachofanyika kwenye jukwaa kinategemea sana ustadi, uimara na ukubwa wa jukwaa.

Katika hoja yangu hii mfumo na muundo wa chama ni kama jukwaa; udhaifu wowote katika eneo hili utajionesha katika watu wanaosimama kwenye jukwaa hilo na uwezo wake wa kuhimili mikikimikiki. Vyama vyote vya siasa vilivyoanzishwa kufuatia kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini vilijikuta vinahitaji kujijenga na kujiunda ili kuweza vyama vya kitaifa kama inavyotaka Katiba na sheria ya nchi. Tatizo ni kuwa chama pekee cha siasa kilichokuwepo na ambacho watu walijua mfumo wake kilikuwa ni CCM.

Matokeo yake ni kuwa karibu vyama vyote vilivyoanzishwa vimejikuta vikinakili kwa kiasi kikubwa sana muundo na mfumo wa CCM kiasi kwamba kuna kufanana kusiko kwa lazima kimfumo na kimuundo kati ya vyama hivi – ukiondoa tofauti kadha wa kadha. Mfumo na Muundo wa CDM umekaa kiCCM zaidi na hili ni tatizo kwa sababu ndilo pia limechangia matatizo ndani ya CCM vile vile na limechangia katika kuleta utawala mbovu nchini. Kufanana huko kwanza ni kwa mfumo wa ngazi za muundo wa chama. Hapo juu tayari nimeonesha muundo wa ngazi za CDM nioneshe jinsi muundo huu unavyoakisi muundo wa CCM.

CCM ina mfumo ufuatao wa kichama:
1. Shina
2. Tawi
3. Kata/Wadi
4. Jimbo
5. Wilaya
6. Mkoa
7. Taifa

Utaona kuwa CDM na CCM vinafanana muundo wao wa kingazi. Swali ambalo labda watu wengine wanaweza kulijibu ni hili: Kwanini CDM ilipoundwa hadi hivi sasa imekuwa na mfumo huu wa ngazi saba wa kichama? Swali jingine la kina zaidi ni kwanini CCM wamekuwa na mfumo huu wa ngazi za aina hii tangu enzi za TANU? Hili swali la pili ni rahisi kulijibu: CCM ilizaliwa na kuishi kwa muda mrefu kama chama cha kijamaa (socialist party) ambacho kama vilivyo vyama vingine vya aina yake hasa wakati wa vita baridi vilikuwa vinajaribu kuhakikisha kuwa chama kinamfikia kila mwananzi kuanzia kwenye nyumba mtaani (vitongoji na shina) hadi kufika ngazi ya taifa.

Vyama vyote vya kijamaa au kikomonisti kama vya China, Cuba, Vietnam n.k vina mfumo wa namna hii ambapo wananchi wana uchaguzi mmoja tu wa kujiunga na chama na uanachama wa chama hicho ni sharti kubwa la kuweza kufanikiwa katika mambo mengine mengi. CCM kwa muda mrefu ilinufaika sana na mfumo huu kwani ilihakikisha kuwa siasa zake zimeenea kuanzia ngazi za juu kabisa hadi kwenye mitaa. Ni mfumo ambao unataka kudhibiti siasa katika nchi; ni mfumo ambao hauendani na demokrasia japo unajionesha kana kwamba unatoa nafasi kwa watu kutoa maoni yao kwa wingi. Mfumo huu umeweka madaraka juu mno kama nitakavyoonesha hapa chini.

Nguvu ya Kamati Kuu

Japo ningeweza kuangalia muundo wa CDM na CCM ngazi kwa ngazi kwa namna ya pekee ningependa kuangalia madaraka ya Kamati Kuu katika vyama hivi vikuu nchini na kwanini muundo huu umepitwa na wakati na ni chanzo kimojawapo cha migogoro katika vyama vya siasa.

Kazi za Kamati Kuu ya CDM

Kwa mujibu wa Katiba ya CDM Ibara ya 7.7.16 Kamati Kuu ya chama imepewa majukumu mengi mno ya kuyasimamia kiasi kwamba inabidi mtu aulize ni kwa kiasi gani KK inaweza kuwa na ufanisi na kutimiza majukumu yake yote haya hasa ukizingatia kuwa wajumbe wake wengi pia wana wawajibu mwingine katika Bunge au chama.

Kazi za KK ya CDM ni hizi:

(a) Kufanya utafiti wa wagombea na wa Uraisi na Mgombea Mwenza na kuwasilisha ripoti zake kwa Baraza kuu kwa ajili ya mapendekezo yake kwa Mkutano Mkuu.
(b) Kuteua Wakurugenzi wa Idara Kuu za Chama Makao Makuu (c) Kuteua Makatibu wa Wilaya na Mikoa
(d) Kuthibitisha uteuzi wa Sekretarieti za Wilaya.
(e) Kutoa mapendekezo kwa Baraza Kuu juu ya rufaa za uchaguzi na kinidhamu.
(f) Kuandaa na kutoa Mapendekezo kwa Baraza Kuu, Mikakati ya kuendesha shughuli za Chama kwa kila mwaka na kwa kipindi cha miaka mitano.
(g) Kuandaa na kutoa mapendekezo kwa baraza Kuu , Mikakati ya kupata mahitaji ya raslimali za kuendesha kampeni za wagombea wa Chama katika chaguzi za kiserikali.
(h) Kuandaa na kutoa mapendekezo kwa Baraza kuu ratiba na maelekezo ya uchaguzi wa kichama.
(i) Kupitia na kutoa kwa Baraza Kuu mapendekezo ya haja ya kuzifanyia marekebisho au maboresho Kanuni za Chama ama Katiba ya Chama.
(j) Kujadili taarifa za Sekretarieti ya Kamati Kuu na kutoa maamuzi na maelekezo kwa utekelezaji.
(k) Kusimamia utendaji kazi wa Sekretarieti ya Kamati Kuu (l) Kufanya mapitio ya Sera za Chama na kutoa mapendekezo kwa Baraza Kuu kwa kuzingatia matokeo ya Utafiti uliofanywa na Sekretarieti ya Kamati Kuu.
(m) Kusimamia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza Kuu na Mkutano Mkuu.
(n) Kuwa kiungo na kudumisha mahusiano mema kati ya Chama na vyama vingine vya siasa nchini, Afrika Mashariki na nchi nyingine.
(o) Kuthibitisha ajira za watumishi wakuu wa Chama ngazi ya Taifa.
(p) Kuteua kamati au tume za kushughulikia masuala maalum ya kichama kwa muda maalumu.
(q) Kuteua wakaguzi wa mahesabu ya Chama kwa kila mwaka
(r) Kuthibitisha uteuzi wa wagombea Uspika, Ubunge na Baraza la wawakilishi Zanzibar
(s) Kuandaa agenda za Baraza Kuu na Mapendekezo ya agenda za Mkutano Mkuu.
(t) Kufanya uamuzi juu ya mpendekezo ya kufukuza Mwanachama.
(u) Kuandaa hoja za kupelekwa Bungeni na Wabunge wa Chama
(v) Kumwachisha ujumbe wa Kamati Kuu mjumbe mteule ambaye ataenda kinyume na katiba, kanuni na maadili au kushindwa kukidhi matakwa ya kuteuliwa kwake.
(w) Kuratibu utendaji wa ofisi ndogo ya Makao Makuu Zanzibar.
(x) Kusimamia utendaji kazi wa Mabaraza ya Vijana, Wanawake na Wazee.
Kuteua wajumbe maalum wawili kuingia Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya.

Kwa upande wa CCM kazi za Kamati Kuu zimeanishwa katika Ibara ya 109 ya Katiba ya CCM. Kazi za KK ya CCM ni nyingi vile vile na baadhi yake ni hizi:

(1) Kutoa uongozi wa Siasa katika nchi.
(2) Kusimamia utekelezaji wa shughuli za kila siku za CCM.
(3) Kueneza Itikadi na Siasa ya CCM nchini.
(4) Kusimamia kampeni za Uchaguzi na kampeni nyinginezo.
(5) Kuteua Makatibu wa CCM wa Wilaya na Katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.
(6) Unapof ika wakati wa Uchaguzi Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa itashughulikia mambo yafuatayo:-
(a) Kuf ikiria na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya Wanachama watakaosimama katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM.
(b) Kuf ikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu majina ya Wanachama wasiozidi watano wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(c) Kuf ikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya Wanachama watakao-simama katika uchaguzi wa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM.
(d) Kuf ikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya majina ya Wanachama wasiozidi watatu ambao wanaomba kugombea kiti cha Rais wa Zanzibar.
(e) Kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya Wanachama wanaoomba nafasi za uongozi katika CCM na Jumuiya zinazoongozwa na CCM ambao uteuzi wao wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.
(f ) Kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya Wanachama wanaoomba nafasi ya Ubunge na Wanachama wanaoomba nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.
(g) Kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya Taifa juu ya Wanachama wa CCM wanaoomba nafasi za uongozi katika Jumuiya za Wananchi zinazoongozwa na CCM, ngazi ya Mkoa na Taifa, ambazo uteuzi wake wa mwisho hufanywa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
(h) Kufikiria na Kufanya uteuzi wa mwisho wa wanachama wa CCM wanaoomba kugombea nafasi ya Spika wa Bunge/Baraza la Wawakilishi, Meya wa Halmashauri ya Jiji/Manispaa.
(7) Kumsimamisha uongozi kiongozi yeyote isipokuwa Mwenyekiti wa CCM na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM endapo itaridhika kwamba tabia na mwenendo wake vinamwondolea sifa za uongozi.
(8) Kuona kwamba masuala ya Ulinzi na Usalama wa Taifa na Maendeleo yanazingatiwa.
(9) Kuandaa mikutano ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.
(10) Kuwa na mikakati endelevu ya kuimarisha Chama kimapato, kudhibiti mapato na mali za Chama na kuthibitisha matumizi ya Chama katika ngazi ya Taifa .

Tuchukue kazi moja hapa na tuiangalie kwa karibu kidogo kama kwa kutumia darubini. Kwa upande wa CDM tuangalie kazi (a) ambayo inasema “Kufanya utafiti wa wagombea na wa Uraisi na Mgombea Mwenza na kuwasilisha ripoti zake kwa Baraza kuu kwa ajili ya mapendekezo yake kwa Mkutano Mkuu.” Na kwa upande wa CCM tuangalie kazi (6b) ambayo inasema “Kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu majina ya Wanachama wasiozidi watano wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Kazi hizi mbili za KK za vyama hivi zinaonesha tu kuwa hakuna mtu anayeweza kuwa Rais wa Tanzania kama hatopata Baraka kutoka kwenye Kamati Kuu ya chama. Hii ina maana KK ya kila chama ni chombo ambacho kinavutia wengi na katika uendeshaji wa chama watu walioko kwenye KK ya chama ni watu wenye nguvu kubwa sana katika chama. Ukilielewa hili utaona kuwa mgongano karibu yote ambayo imetokea ndani ya CDM hadi hivi sasa inahusisha kwa kiasi kikubwa wajumbe wa Kamati Kuu. Ikumbukwe kuwa kinachoitwa Baraza Kuu kwa upande wa CDM ni sawasawa na kile kinachoitwa Halmashauri Kuu ya Taifa.

Tungeweza hata kulinganisha kazi za vyombo hivyo na tungeona jinsi ambavyo vinafanana. Na hata kwenye ngazi ya Mkutano Mkuu utaona kuwa CCM na CDM (kama ilivyo kwa vyama vingine) bado vinafanana sana. Na siyo kwenye ngazi hizi tu hata huku chini utaweza kuona kufanana huko na maana yake katika utendaji wa chama.

Tatizo la kufanana huku ni nini basi?

Kufanana huku kuna tatizo moja kubwa; kama mfumo wa CCM umekosewa kinadharia na kiutendaji basi vyama vilivyonakili mfumo huo vitajikuta vinaingia kwenye matatizo yale yale ya CCM. Ni sawasawa na watoto darasani ambapo mmoja anayedhaniwa kuwa ana akili anafanya makosa katika kujibu swali halafu mwingine pembeni yake naye ananakili kosa. Halafu itokee mtoto wa tatu ambaye anaangalia mtoto wa kwanza akinakili kosa amsahihishe na kumuambia “hujanakili sawasawa” akiamini kuwa kinachonakiliwa kiko sawasawa. Hili la muundo na mfumo wa chama ni pana na lenye kina cha kutosha; itoshe kusema tu kuwa mfumo huu wa chama kwa CDM unachangia sana kuanzisha, kuendeleza na kukoleza matatizo na migogoro.

Hali ingekuwa hivi hivi kwa CCM kama wasingekuwa madarakani kwani ni mfumo ule ule ambao umepitwa na wakati na ambao hauendani na hali halisi ya jitihada za kujenga demokrasia nchini. CCM kinga yao ni kuwa wao wana serikali na hivyo wanajua kuwa hawawezi kwenda mbali sana na malisho. Ningeweza kuliangalia hili kwa kina lakini kama ipo haja (kama watakuwepo wa kubishia hili) basi nitazama zaidi na kuonesha mlinganisho na utofauti (contrasting) mfumo wa chama chenye sera zilizoshindwa na kiko madarakani tunahangaika nacho na chama kinachotaka kushika madaraka lakini kina mfumo wa chama kilichoshindwa.

Muundo wa sasa wa CDM hauna chombo huru cha kushughulikia migogoro au masuala makubwa ya nidhamu. Katiba ya CDM imeweka vikao vya kichama kama sehemu ya kutatulia migogoro kwa kila ngazi ya chama. Kwa maoni yangu, kukosekana kwa chombo huru cha kichama ambacho kinaweza kuhusika katika kusimamia nidhamu kuliko ilivyo sasa ambapo kwa mujibu wa Ibara ya 6.3.6.

Kukosekana kwa chombo huru cha kutatua migogoro na kusimamia nidhamu

Kwa kiasi kikubwa yote yanayotokea sasa hivi ni matokeo ya hili vile vile; kwamba hakuna chombo huru ambacho kinaweza kushughulikia migogoro katika chama, kabla haijakua na chenye uwezo wa kupendekeza hatua za nidhamu kabla mambo hayajafika mbali. Mojawapo ya mambo ambayo yameikoroga sana CDM ni kuwa kusimamia nidhamu kunahitaji vikao vya chama; na vikao vya chama vinahitaji wajumbe na wajumbe ni lazima wafikie idadi inayotakiwa ili kufanya maamuzi mbalimbali. Na kwenye chama ambapo baadhi ya wajumbe wana nyadhifa nyingine nje ya chama wakati mwingine ni vigumu mno kuita vikao kwa wakati na kwa ufanisi unaotakiwa.

Mwisho utaona kuwa hadi matatizo yanapokuwa yamefikia pasipovumilika ndio vikao vinalazimika kuchukua hatua kali – kufukuzana au kunyang’anyana vyeo n.k – wakati kama tatizo lingeweza kushughulikiwa mapema zaidi hali isingefika huku. Fikiria mtu anaweza kuwa na tatizo na wajumbe wa Kamati Kuu na yeye ni Mjumbe wa kamati kuu na kamati kuu hiyo hiyo ndiyo chombo cha nidhamu kwa ngazi hiyo na hivyo kamati kuu hiyo ambayo ndani yake ina watu wanagongana inasimama kumshughulikia mjumbe mwingine.

Au unaweza kuangalia kinyume chake kwamba Kamati Kuu ina tatizo na mmoja wa wajumbe na kwa vile ndiyo chombo cha nidhamu inaamua kumshughulikia wakati huo huo mtu anayehusika naye anatafuta mahali ambapo ni huru (impartial) na anajikuta hana isipokuwa kusubiri kikao cha juu ambacho katika mfumo wa CDM ni kikao cha Baraza Kuu.Tatizo ni kuwa wajumbe wote wa kikao cha Kamati Kuu kwa mujibu wa Ibara ya 7.7.11a nao ni wajumbe wa Baraza Kuu! Yaani mtu anataka kukata rufaa ya kikao cha chini kwenda kikao cha juu ambacho wajumbe wake ni wale wale waliomhukumu kwenye kikao cha chini!

Mfumo huu hata hivyo unazaa chanzo cha pili cha migogoro ndani ya CDM; siyo tu kwenye ngazi ya taifa bali hadi kwenye ngazi za chini kabisa. Chanzo cha tatu kama nilivyosema hapo awali sitaangalia sana. Chanzo kikubwa kabisa na chenye hatari kwa chama ni ukosefu wa nidhamu ambayo nimezungumzia katika sehemu ya kwanza; nidhamu ya chama. Kama tumeliweka jukwaa letu wazi na tukaliona udhaifu wake basi yanayotokea juu yake hayawezi kuwa mema hata kama watu wake watakuwa wamevaa suti, wanaimba kwa furaha au wamevaa magwanda na wanazungumza kwa jazba. Kwamba jukwaa haliko imara yote wanayoyafanya yanahatari ya kuwaangukia na wanaweza kusababisha matatizo hata kwa wasio husika.

Nimesema hapo juu kuwa tatizo hili au chanzo hiki cha mfumo na muundo wa chama kinasababisha tatizo la pili ambalo wote tunaliona. Hili la kwanza linahitaji kutulia na kulichambua kwa kina kuweza kuona jinsi gani linasababisha migogoro lakini hili la pili ni rahisi kulionesha kuwa linasababisha migogoro kwa sababu wahusika wamesimama kwenye mfumo mbovu wa chama; mfumo ambao ulitakiwa ubadilishwe mara tu ya uchaguzi wa 2010; mfumo ambao sidhani kama utabadilika wakati wowote sasa hivi hasa kuelekea uchaguzi wa Serikali ya Mitaa mwakani. Mfumo huu unasababisha tatizo lisilokoma la Utovu wa Nidhamu (Indiscipline).

Itaendelea kesho.

No comments:

Post a Comment