Mwanza. Katika kile kinachoonekana kama
kujipigia debe katika kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa
2015, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba amewaambia viongozi wa dini Kanda ya Ziwa kwamba vijana
wanapofika kuomba ridhaa yao, muwaangalie, msiwabeze.
Huku akikataa kuweka bayana nia yake ya kuwania
urais kwa maelezo kwamba muda wa kufanya hivyo haujawadia, Makamba
aliwaambia viongozi hao wa dini kwamba wagombea hao wanapopita wawasomee
sifa za uongozi katika Biblia na kusema kumekuwapo mjadala wa sifa za
uongozi kuhusu kijana na kusema amekuwa akitoa mwito kwa vijana
wasiokuwa na makandokando kushiriki na kujitokeza katika kusaidia nchi
ipone.
Akizungumza juzi usiku mjini hapa katika chakula
cha pamoja na maaskofu na wachungaji kutoka Umoja wa Makanisa ya
Kikristo wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Makamba ambaye pia ni mbunge wa
Bumbuli (CCM), alisema: “Huu ni wakati wa kila mmoja kutafakari hatima
ya nchi yetu. Ndugu zangu… nadhani tuzungumze machache yanayohusu nchi
yetu na Taifa letu, kwa sababu sote ni Watanzania na wote tuna hamu ya
kujua na kutafakari mustakabali wa nchi yetu, umoja wetu, amani yetu na
utulivu wetu.”
Alisema vijana wengi wamekuwa waoga kwa madai
kwamba hawana fedha, uzoefu lakini akasema maaskofu na wachungaji
wanapaswa kuwa mashahidi kupitia vitabu kwani katika Yeremia imeelezwa
jinsi Mungu alivyompatia unabii Yeremia ambaye alidai yeye bado mdogo.
“Yeremia alipopewa unabii alilalamika mimi mdogo
mimi siwezi, lakini Mungu alimwambiaje, ngoja nisome, (Yeremia 1: 4-10)
…. Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako nilikujua, kabla
hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalumu, nilikuweka uwe nabii kwa
mataifa,” alisema na kuongeza:
“Bwana alimwambia usiseme, mimi ni mtoto mdogo.
Utakwenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza,
usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe.”
Alisema Tanzania inapita katika kipindi kigumu,
hivyo viongozi wa dini wanapaswa kuongoza maombi yatakayoiwezesha kupata
kiongozi mwenye sifa ya kuivusha katika kipindi hicho.
Makamba amesema nchi inakabiliwa na nyufa kama
vile rushwa, udini, ukabila, Uzanzibari na Uzanzibara, huku akirejea
hotuba ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya Machi 1995,
ambayo aliyataja mambo hayo kuwa nyufa zinazoweza kuliangamiza taifa.
Alisema Tanzania inahitaji uponyaji na ikibidi
kuanza upya kwa maana ya aina ya uongozi unaohitajika hivi sasa na
kwamba ili kutimiza lengo hilo, viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya
kutafakari na kuielekeza nchi njia sahihi ya kufuata.
“Shughuli za siasa zimeingiliwa na matapeli,
lakini hata shughuli yenu pia imeingiliwa na matapeli. Sasa tunapotafuta
uponywaji wa nchi yetu ninyi mna nafasi kubwa kwani uponyaji
tunaouzungumzia ni wa maovu ya kiroho, uongo, ubakaji na vitu kama
hivyo, ninyi mna nafasi kubwa sana,” alisema.
Alisema viongozi wa kisiasa pia wanayo nafasi yao katika kuponya taifa lakini lazima wanapofanya kazi hiyo wawe wasafi.
Alisema askofu au mchungaji akihubiri anapaswa
kuwa msafi na hata katika uongozi wa siasa anaposimama mtu na kusema
yeye ni jawabu la matatizo ya wananchi ni vizuri kumtazama sura yake
kama ameacha (maovu).