Wednesday, September 5, 2012

Simba vs Yanga ‘live’ SuperSports

MCHEZO wa raundi ya kwanza Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga, unatarajiwa kurushwa ‘live’ kupitia kituo cha televisheni cha SuperSport chenye makao yake makuu nchini Afrika Kusini.
Mechi hiyo ambayo itachezwa Oktoba 3 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa mechi tano za ligi hiyo, zitakazorushwa ‘live’ na kituo hicho kwa mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa mazungumzo ya udhamini wa kituo hicho kwa Ligi Kuu utakaoanza mwakani.
Alisema kutokana na mazungumzo hayo kutokamilika, wameona waanze kwa majaribio kwa kuonesha mechi hizo tano, na mwakani wataendelea na ratiba nyingine baada ya mipango kukamilika.
“Kama mjuavyo, SuperSport wana ratiba zao na mambo mengi, hivyo inabidi kujipanga kwanza, lakini mazungumzo yanakwenda vizuri na ndiyo maana kwa kuanzia wataonesha mechi hizo tano,” alisema.
Mbali na mechi hizo, Wambura alizitaja nyingine zitakazorushwa ‘live’ na kituo hicho ni pamoja na ule wa Azam FC dhidi ya JKT Ruvu utakaochezwa Uwanja wa Chamazi Complex, na ule wa Simba na Tanzania Prisons utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambako mechi hizo zote zitafanyika Septemba 28.
Mchezo mwingine ni kati ya Yanga dhidi ya African Lyon utakaochezwa Septemba 30 Uwanja wa Taifa, sambamba na ule wa Ruvu Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa Chamazi.
Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 15.

No comments:

Post a Comment