Wednesday, September 26, 2012

HAKI HAIWEZI KUSHINDWA NA HILA ZA JK,MCH.MTIKILA ENDELEA KUSEMA KWELI NA KUSIMAMIA HAKI IPO SIKU DUNIA ITAELEWA.

 
MWENYEKITI wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameshinda kesi iliyofunguliwa na serikali, akidaiwa kuchapisha na kumiliki waraka wa uchochezi unaomkashifu Rais Jakaya Kikwete.
Hukumu ya kesi hiyo iliyovuta hisia za wengi nchini, ilitolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Elvin Mugeta.
Katika kesi hiyo ya jinai iliyofunguliwa mwaka 2010, Hakimu Mgeta alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa mshtakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na makosa mawili.
Mchungaji alikuwa akikabiliwa na makosa mawili.
La kwanza ni kuchapisha kusambaza waraka wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1),(c) cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 2002 na kosa la pili ni la kumiliki waraka huo kinyume na kifungu cha 32(2) cha sheria hiyo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mugeta alisema Mtikila katika utetezi wake alikiri kuandaa na kuumiliki waraka huo uliotolewa mahakamani hapo kama kielezo cha tatu na jumla ya mashahidi wanne waliletwa na upande wa serikali.
Alisema wakati serikali ikileta mashahidi hao, Mchungaji Mtikila hakuleta shahidi hata mmoja na badala yake alijitetea mwenyewe kwa madai kuwa hakuona sababu ya kuwaleta mashahidi kwani kufanya hivyo ni kumaliza fedha na kupoteza muda wa mahakama.
Hakimu Mugeta alisema kabla ya kutoa hukumu hiyo, alijiuliza maswali kuwa je, ni kweli waraka huo ni wa uchochezi? Je, waraka huo ulileta madhara katika jamii? Je, waraka huo ulikuwa ukitaka kumpindua Rais Kikwete kinyume na sheria za nchi?
“Mimi nimeusoma waraka huo unaodaiwa na upande wa jamhuri kuwa ni uchochezi na nimebaini kuwa si wa uchochezi kwani Mtikila ni mwanasiasa, pia ni kiongozi wa dini na waraka ule ulikuwa umejaa maneno ya kidini ambayo ndani yake Mtikila alikuwa akiwataka Wakristo wenzake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 watumie haki yao ya msingi ya kumpigia kura mgombea ambaye ni Mkristo.
“Na kumng’oa madarakani Rais Kikwete kwa njia ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu si kosa la jinai.
“Mahakama hii kwa kauli moja imeona upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi unaoonyesha Mtikila alikuwa anataka Wakristo wamuondoe Rais Kikwete Ikulu kwa njia haramu.
“Pia upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kwamba kusambazwa kwa waraka huo kulileta madhara, na wameshindwa kuleta ushahidi unaoonyesha waumini wa dini ya Kikristo walishawishika na waraka huo na wakajaribu kumuondoa Rais Kikwete madarakani kwa njia haramu,” alisema Hakimu Mugeta.

No comments:

Post a Comment