Friday, September 28, 2012

Dk. Willibroad Slaa,jJK NDO ANAIZIKA CCM KWA KUPITISHA WATUHUMIWA WA UFISADI KUGOMBEA NEC.

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibroad Slaa, amemvaa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, akisema amekitengenezea kaburi la kukizika rasmi chama chake kwa kuruhusu watuhumiwa wakubwa wa ufisadi kugombea nyadhifa mablimbali.
Dk. Slaa alisema uteuzi wa wagombea ndani ya CCM uliomalizika juzi umeonyesha wazi kwamba sasa chama hicho kinatumbukia kwenye dimbwi kubwa na pana lisiloweza kukitoa tena.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Mwanza, alikojichimbia kuhakikisha mchakato wa uchaguzi wa mameya wa jiji hilo unakwenda vizuri leo, Dk. Slaa alisema dhamira ya kweli dhidi ya CCM katika kuwaweka vijana kwenye uongozi ili kukinusuru chama hicho imezimika baada ya Kikwete kuruhusu watuhumiwa wa ufisadi na wakongwe kugombea uongozi.
“Katika hili la uteuzi wa CCM, nangojea taratibu zao zikamilike. Tulitegemea CCM muda huu ni wa kujisafisha, lakini imeshindwa kufanya hivyo. Mimi simung’unyi maneno kuhusu watuhumiwa wa ufisadi.
Mfano (anataja) ni fisadi wa fedha za rada. Mimi hapa nilishapeleka ushahidi hadi wa akaunti namba ya benki yake kwa DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini), alisema.
Alisema inashangaza kuona katika utetezi wa CCM, mtuhumiwa huyo amepatiwa nafasi licha ya kushindwa kueleza wazi fedha nyingi kwenye akaunti hiyo ya Uswisi alizipataje.
“Mtuhumiwa mkubwa kama huyu wa ufisadi eti leo CCM inampitisha awe mgombea. Kweli? Sioni dhamira ya CCM kupambana na vitendo vya kifisadi. Na hata dhamira ya vijana haipo bali imejitumbukiza kwenye dimbwi ambalo kamwe hakitatoka humo,” alisisitiza.
Kuhusu Lowassa na tuhuma zake za ufisadi wa kampuni ya kufua umeme wa dharura wa Richmond zilizosababisha kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, Dk. Slaa alisema kiongozi huyo alilazimika kujiuzulu kama sehemu ya kuwajibika, lakini ameshindwa hadi leo kumtaja mhusika hasa wa kampuni hiyo.
Alisema kama kweli Lowassa alisingiziwa katika tuhuma hizo, alipaswa kuwaeleza Watanzania nani anayehusika na ufisadi huo wa Richmond ambayo ilishindwa kuzalisha umeme licha ya kutumia mamilioni ya fedha za umma.
Kuhusu wanachama wa CCM ambao majina yao yamekatwa na NEC, Dk. Slaa alisema milango iko wazi CHADEMA kwa wale wasio mafisadi kujiunga ili kukielekeza chama hicho kushika dola mwaka 2015.
Alisema CHADEMA ni chama makini huenda kuliko vyama vingine, hivyo hakiwezi kupokea wanachama kutoka CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi, vinginevyo kitafunga milango na mapazia yake.
“Unajua, kuna watu wanaojulikana kwa ufisadi. Pia wapo wasafi wanaoomba kujiunga na CHADEMA, hivyo watu safi hawana tatizo kujiunga na CHADEMA kwa ajili ya kuunganisha nguvu kwenda kuongoza dola mwaka 2015,” alisema Dk. Slaa.

No comments:

Post a Comment