Thursday, September 20, 2012

unajua kwa nini yanga walifungwa 3 ??? fuatilia habari hii siri imefichuka

SIKU moja baada ya mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga, kulimwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, siri ya kisago hicho imefichuka.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo, kipigo hicho hakikutokana na udhaifu wa kikosi na kuzidiwa mbinu kiuchezaji, bali mgomo baridi wa wachezaji wa timu hiyo kutaka kufikisha kilio kwa viongozi wao.
Kilio chenyewe ni kutaka uongozi kurejesha posho ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wachezaji kwa kila mechi kiasi ambacho hutofautiana kulingana na matokeo ya mechi, iwe kushinda au sare.
Habari zinasema kilichowakera wachezaji, ni hatua ya uongozi kufuta posho hizo za ziada baada ya mechi kwa wachezaji nje ya mishahara yao, wakitaka zirejeshwe kwa mchezaji kupata sh 100,000, kama timu imeshinda na sh 50,000 kwa matokeo ya sare.
Aidha wachezaji wanataka kurejeshwa kwa utaratibu wa kutoa posho kama sh 30,000 kwa mchezaji asiyepangwa katika mechi husika, mambo ambayo hayakuwa yamewekwa sawa hadi ligi hiyo inaanza Septemba 15.
“Kufungwa ni sehemu ya mchezo, lakini kipigo cha 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar, sio kusema Yanga ni dhaifu kihivyo, wachezaji wametaka kufikisha ujumbe kwa uongozi kujadili mambo yao muhimu hasa maslahi,” kilidokeza chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema, kilio chao ni kama kimesikika kwani uongozi chini ya Mwenyekiti wake Yusuph Manji, jana jioni ulipanga kukutana na wachezaji kujadili hali hiyo na kuweka mambo sawa kabla ya mambo kuwa mabaya zaidi kuelekea mechi ya watani wao Simba.
Baada ya Yanga kuanza ligi hiyo kwa sare ya bila kufungana na Prisons ya Mbeya na kufungwa 3-0 na Mtibwa Sugar, kesho itakwaana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kuelekea mechi hiyo ya kesho, baada ya timu hiyo kurejea kutoka Morogoro, imekwenda moja kwa moja kambini ikiendelea kunoa makali yake ambapo jana asubuhi ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kaunda.
Baada ya mechi ya kesho, Yanga itacheza tena Septemba 30 dhidi ya Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, kabla ya kukutana na Simba hapo Oktoba 3.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa viongozi wameona ni muhimu kujadili jambo hilo mapema ili kushinda mechi mbili za JKT Ruvu na Lyon kutuliza upepo kabla ya kukutana na mtani wao Simba.
Akizungumzia kichapo hicho cha juzi, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu, alikiri kuwa kimewashtua na mkuu wa benchi la ufundi, Tom Saintfiet, leo atatolea ufafanuzi.

No comments:

Post a Comment