Saturday, September 29, 2012

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kutwaa uongozi wa halmashauri ya jiji la Mwanza

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kutwaa uongozi wa halmashauri ya jiji la Mwanza, baada ya kushinda nafasi ya Meya iliyokuwa ikishikiliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Chadema ilitwaa nafasi hiyo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ambapo diwani wa Nyakato, Josephat Manyerere alishinda.
Kwa ushindi huo, Manyerere akawa Meya wa kwanza wa jijini hilo kutoka upinzani, tangu Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika 1992.
Kwenye uchaguzi wa jana, CCM kilimsimamisha diwani wa kata ya Mkolani, Stanslaus Mabula, kuwania nafasi ya Meya wa jiji wakati Naibu Meya ikimshirikisha John Minja (diwani wa Igogo).
Kwa upande wa Chadema, kilimsimamisha diwani wa kata ya Mahina, Charles Chinchibela, kuwania nafasi ya Meya na kuacha nafasi ya Naibu Meya kuwaniwa na diwani wa kata ya Mirongo (CUF), Daud Mkama.
Matokeo ya jana yakawa CCM kuibuka ‘mbabe wa siasa za Mwanza’ baada ya Mabula kupata kura 11 dhidi ya nane za Chinchibela.
Dhoruba ya kisiasa ya CCM iliuangukia upinzani katika nafasi ya Naibu Meya ambapo mgombea wake, Minja, alipata kura 10 dhidi ya kura 8 alizopata Mkama wa CUF.
Kabla ya kufanyika uchaguzi huo, madiwani wa Chadema wakiongozwa na Mbunge wa Nyamagana, Hezekiah Wenje, walijaribu kugomea uchaguzi huo wakipinga hatua ya CCM kuwahamisha Mbunge wa viti maalum (CCM), Maria Hewa na diwani wa viti maalum (CCM), Leticia Simba, kutoka wilaya ya Ilemela kwenda Nyamagana.
Madiwani hao wa Chadema walikusudia kugomea uchaguzi huo kwa madai kwamba, Mbunge Hewa na Diwani Simba ni wakazi halali wa wilaya ya Ilemela, na hati zao za viapo bungeni na katika baraza la madiwani, zinatamka hivyo.
Hata hivyo, baada ya kujadiliana kwa kina, hatimaye madiwani hao wa Chadema walikubali kurudi na kuendelea na uchaguzi na kujikuta `wakiangukia pua’ na kuiacha halmashauri ya jiji la Mwanza katika uongozi wa CCM.

No comments:

Post a Comment