Friday, September 14, 2012

Kesi hiyo namba 186 ya mwaka 2012 NDO INAMKABILI NAPE NAUYE WA CCM

HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemfungulia mashitaka Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, aliyedai kuwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapata mabilioni ya fedha kutoka nje.
Kesi hiyo namba 186 ya mwaka 2012 imefunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika semina iliyoishirikisha taasisi ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS), Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema CHADEMA haina washirika wowote wanaowapatia mabilioni ya fedha kwa ajili ya kujiimarisha wala kufanya kampeni, na kauli ya Nape ni propaganda za kisiasa zenye lengo la kukichafua chama hicho.
“Maneno yanayosambazwa na kina Nape ni propaganda za vyama, hasa Chama Cha Mapinduzi ambacho kimekuwa kikifanya kila kiwezalo kuisambaratisha CHADEMA,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa aliwatoa hofu wananchi na kukanusha kusaidiwa fedha na wafadhili katika kampeni zao na kuongeza kuwa wanaopiga propaganda kwamba chama hicho kinapatiwa fedha na wafadhili ni wazushi.
Alisema propaganda za aina hiyo zimepitwa na wakati na hawatawavumilia wanaozusha kwani mara nyingi wamedharau, lakini sasa wamechoka na kuamua kuchukua hatua za kisheria.
“Kwa mfano, leo hawa wenzetu wa KAS wametusaidia kumleta huyu aliyekuwa Naibu Waziri wa Uchumi na Maendeleo katika Serikali ya Ujerumani, Klais-Jurgen Hedrick, na wao wametusaidia kulipia ukumbi, pia wanatusaidia kuchapisha vitabu na majarida.
“Wenzetu wanajua kabisa kuwa sisi tunashirikiana na vyama kutoka Uingereza, Christian Democratic Union (CDU) cha Ujerumani na chama cha Uingereza, lakini wao pia hivyo hivyo wanashirikiana na mashirika mengine yenye mlengo ya aina hiyo hiyo ya kujengea uwezo vyama na huo ni utaratibu wa dunia nzima wa vyama rafiki kushirikiana. Dhana hiyo isipotoshwe kwa CHADEMA,” alisema Dk. Slaa.
Hata hivyo alisema wamekuwa wakishirikiana na vyama hivyo kwa miaka mitano na kwa mwaka wanapokea wastani wa sh milioni 60 kutoka KAS kwa muda wa miaka mitano na chama kingine rafiki kutoka Uholanzi huwapa sh milioni 20, ambapo CCM pia hupata mara tatu ya kiasi wanachopata CHADEMA kutokana na uwakilishi wa viti vingi bungeni.
Naye aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Uchumi na Maendeleo Ujerumani, Klaus-Jurgen Hedrich, alisema KAS haitoi fedha kwa CHADEMA kama inavyoenezwa.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amekanusha chama hicho kushabikia ushoga huku akisema tabia hizo haziendani na mila na desturi za Tanzania.
Mbowe pia alisema CHADEMA kipo kwa ajili ya watu wote na hakisimamii dini ya mtu na kinafuata misingi ya sera zake.
Alipohojiwa na gazeti hili kuhusu kesi hiyo, Nape alisisitiza kuwataka CHADEMA watangulie mahakamani kwani anatembea na boksi lenye nyaraka za ushahidi kwenye gari lake.
Hivi karibuni, Nape alikaririwa akisema CHADEMA imekuwa ikipata mabilioni ya fedha kutoka nje na kuwahadaa wananchi kwa kuwachangisha fedha kwenye harambee.
Awali Nape alipewa siku saba na CHADEMA ili kuomba radhi kutokana na kauli hiyo, jambo ambalo katibu huyo hakulitimiza na kusisitiza kwamba ana ushahidi wa hoja hiyo.
Wakati huo huo, aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Uchumi na Maendeleo nchini Ujerumani Hedrick, amelaani mauaji na vitendo vya mabavu vilivyotokea mkoani Iringa na kusababisha kifo cha mwandishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Hedrick alisema Tanzania tangu kupata uhuru imesimama vizuri katika kuhakikisha amani inakuwepo na ilijihakikishia jambo hilo kwa kuwa nchi pekee barani Afrika inayojivunia amani na utulivu.
Hedrick alisema taifa likiwa linaendelea haliwezi kuwa na chama kimoja kwani demokrasia maana yake ni kila mmoja kupata haki ya kushiriki.
Alisema uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu kwani ndio unaoleta na kujenga demokrasia ya kweli.
Akizungumzia Jeshi la Polisi, alisema kuwa kazi yao ni kulinda na kuhakikisha maisha ya watu yanakuwa salama na kuwataka waliohusika na mauaji ya Mwangosi wafikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake kwani polisi kazi yake si kuua.
“Kuna msemo ambao kila kiongozi anatakiwa auelewe; Serikali ya leo iliyopo madarakani itakuwa pinzani siku moja na chama cha upinzani kitakuwa serikali siku ya kesho,” alisema.

No comments:

Post a Comment