Sunday, September 30, 2012

Bundi waleta tafrani mkutano wa CCM,wadaiwa ni watu waliogeuka kuwa bundi ilikuvuruga mkutano huo.

 Nusura waangukie alipokaa Lembeli, Mgeja
Katika hali ya kushangaza iliyotokea katika uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) unaoendelea wilaya mbalimbali nchini, jana bundi wawili waliingia kwenye ukumbi wa mkutano mjini hapa.
Bundi hao nusura waangukie juu ya meza waliyokuwa wamekaa Mbunge wa Jimbo la Kahama James Lembeli na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja.
Kitendo cha bundi hao kimetafsiriwa na baadhi ya watu kuwa ni cha kishirikina. Hata hivyo, katika imani za kiafrika, bundi anapoonekana maeneo ya nyumbani kwako au kulia juu ya paa la nyumba yako, hiyo kitafsiri ni dalili mbaya sana ya mikosi itakayokuandama baada ya hapo.
Imeelezwa kuwa vitendo vya kishirikina bado vimeshamiri kwa baadhi ya watu wanaowania kupata uongozi.
Hali hiyo ilizua mtafaruku mkubwa ndani ya ukumbi wa mkutano hasa kwa wagombea wa nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM wilayani hapa ambao walionekana kuwa na wasiwasi.
“Ni ajabu kweli bundi kuingia katika ukumbi huku kukiwa na kelele kubwa na kutaka kuanguka katika meza za viongozi, kitendo hicho ni cha kushitua sana,” alisema, Diwani wa kata cha Chambo, Damas Joseph.
Alisema kuwa mambo hayo yanayohusiana na imani za kishirikina katika chaguzi za CCM, hivyo ni muhimu yakakemewa na chama kwani viongozi wanapaswa kuchaguliwa kwa haki kupitia kura zinazopigwa na wajumbe.
Hata hivyo, alisema hadi sasa hakuna malalamiko yoyote yaliyojitokeza wakati uchaguzi huo ukiendelea na kuongeza miujiza hiyo iliyojitokeza ndio iliyoshtua wajumbe.
Mwanachama mwingine wa CCM kata ya Ukune, Deo Ndilima, alisema kuwa kwa sasa bado vitendo vya kishirikina havijaisha na kuongeza kuwa hali hiyo ni ya hatari hasa katika uchaguzi na inasababisha chama kupata viongozi wasiofaa.

No comments:

Post a Comment