Friday, September 28, 2012

NI CHADEMA VS CCM KATIKA UMEYA JIJINI MWANZA LEO

uchaguzi wa mameya wa wilaya mbili za Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza, unatarajiwa kufanyika leo huku mnyukano mkali ukiwa katika halmashauri ya Nyamagana kutokana na CCM na CHADEMA kuwa na idadi sawa ya viti vya madiwani na hivyo kutegemea kura za CUF ziamue mshindi.
Katika Halmashauri ya Ilemela, CHADEMA ina uhakika wa asilimia mia moja kutokana na kuwa na madiwani wengi kuzidi wenzao wa CCM huku mikakati yao ikilenga kuwashirikisha CUF ili waitwae pia Nyamagana.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kugawanywa na hivyo kuzaa halmashauri hizo mbili. Lakini pia Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa sasa muda kadhaa haikuwa na Meya baada ya Baraza la Madiwani kumvua wadhifa huo, Jackson Manyerere (CHADEMA).
Baada ya meya kuenguliwa, kulizuka mtafaruku ndani ya CHADEMA jijini hapa ambao ulisababisha madiwani wawili kutimuliwa uanachama kwa kile kilichodaiwa ni usaliti wa kuanzisha hoja ya kumtosa kiongozi huyo.
Hivyo kutokana na CHADEMA kutokuwa na madiwani hao, inaingia kwenye uchaguzi wa leo ikiwa na madiwani sita na mbunge Ezekiel Wenje katika wilaya ya Nyamagana wakati wenzao CCM wana madiwani saba na CUF wawili.
Kwa mnyukano huo ni dhahiri kuwa CHADEMA na CCM watakuwa wamefungana kwa kura na hivyo kuhitaji huruma ya madiwani wa CUF ili upande mmoja uibuke kidedea.
Taarifa za uhakika kutoka jijini hapa ni kwamba CHADEMA wamefanya mazungumzo ya kushirikiana na CUF kwa kuwaachia nafasi ya Naibu Meya ambayo itagombewa na diwani wao wa kata ya Mirongo, Daud Mukama.
Kwa halmashauri ya Ilemela CHADEMA wana uhakika wa kuibuka kidedea kutokana na kuwa na madiwani wanane na mbunge Highness Kiwia huku wenzao wa CCM wakiwa na madiwani sita na CUF ina mbunge wa Viti Maalum, Mkiwa Kimwanga.
Kamati za utendaji za CHADEMA katika wilaya hizo zimefanya vikao tofauti kwa kushirikiana na kamati za madiwani na kukamilisha mchakato wa kupata wagombea wao.
Kwa mujibu wa ofisa habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, kamati ya utendaji ya wilaya pamoja na madiwani wa Nyamagana walimteua aliyekuwa Naibu Meya kabla, Diwani wa Kata ya Maina, Charles Chibara, kuwa mgombea wa umeya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Kwa upande wa Ilemela, kikao cha kamati ya utendaji pamoja na madiwani walimteua Diwani wa Kata ya Nyamanoro, Abubakar Kapera, kuwa mgombea wa umeya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Kikao hicho cha Ilemela, pia kilimteua Diwani wa Kirumba, Danny Kahungu, kuwa mgombea wa nafasi ya Naibu Meya halmashauri hiyo wakati kamati ya utendaji ya Nyamagana imekubali kumwachia kugombea nafasi ya Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Diwani wa Mirongo, Daudi Mkama (CUF).
Wao CCM wamemteua Diwani ya Kata ya Mkolani, Stanslaus Mabula, kugombea nafasi ya umeya katika halmashauri ya jiji la Mwanza huku diwani wa kata ya Igogo, John Minja, akigombea unaibu meya na Ilemela wagombea ni Renatus Kalunga na naibu wake Sarah Ng’hwanu.

No comments:

Post a Comment