Friday, September 21, 2012

MUFTI SIMBA ASEMA HAKUNA MWENYE UWEZO WA kumng’oa madarakani kama muhogo

SHEIKH Mkuu wa Tanzania, Issa Bin Shaaban Simba, amesema hakuna taasisi yoyote yenye uwezo wa kumng’oa madarakani kama muhogo, kwani yeye ni kiongozi aliyechaguliwa kutokana sheria za dini ya Kiislam.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kikundi cha Jumuiya na Taasisi za Kiislamu kinachoongozwa na Sheikh Ponda Issa Ponda, kudai kwamba kiongozi huyo amekaa madarakani kinyume cha Katiba huku akishindwa kuwaletea Waislamu maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mufti Simba, alisema kuwa kauli hiyo si ya kwanza kutolewa na kikundi hicho, hususan kikimtisha kuung’oa uongozi wake madarakani.
Alisema kuwa awali mwaka 1992 wakati wa uongozi wa aliyekuwa Mufti Sheikh Hemed Bin Jumaa Bin Hemed, kikundi hicho kilikuja juu kwa madai ya kutaka kuung’oa uongozi huo madarakani.
Mufti Simba alifafanua kuwa kutokana na ghasia hizo, serikali ilichukua jukumu la kuingilia kati na kuidhinisha kuandikishwa kwa Baraza la Kiislamu, kwa madhumuni la kuwaletea Waislamu maendeleo makubwa yanayodaiwa Bakwata imeshindwa kufanya.
Hata hivyo, Mufti Simba alisema ni jambo la kustaajabisha kuwa hadi sasa ni miaka 20 tangu baraza hilo lilipoandikishwa na hakuna jambo lolote la kuwaendeleza Waislam lililofanywa, badala yake limeshindwa kuboresha hata ofisi ya zake.
Katika hilo, alichanganua kuwa si baraza, taasisi wala tawi lililoendesha shughuli zozote za maendeleo ya Kiislamu zaidi ya ghasia za maandamano, kupora misikiti pamoja na kudandia matukio kwa kuwatapeli Waislamu fedha zao ambazo huishia mifukoni mwa Ponda na wenzake.
“Matukio mbalimbali yanayoripotiwa katika kadhia yanajaribu kujenga taswira inayoonyesha kwamba mgogoro uliopo ni baina ya Waislamu na Bakwata, taswira hii si sahihi ni potofu,” alisema.
Mufti Simba alitumia fursa hiyo kuufahamisha umma wa Kiislamu kuwa ukweli halisi wa kadhia hiyo kuhusu kikundi hicho kinachojitambulisha kama Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, akisema ni kigenge cha watu wachache wenye kufuata madhehebu ya Mawahabi ambao kwa mujibu wa itikadi yao wanaamini kwamba Muislamu yeyote asiyefuata itikadi yao basi huyo siyo Muislamu na hafai kuwa kiongozi kwa ngazi yoyote ile.
Aliongeza kuwa kikundi hicho kimejivika vazi la kuendesha harakati za Kiislamu kikiwashinikiza wenzao kufuata sheria zao badala ya kutii mamlaka ya dola.
“Kikundi hicho kimekuwa kikiendesha mafunzo ya karate kwenye misikiti waliyoiteka na kuikalia kimabavu kwa kuwatumia vijana wao ili waweze kuendeleza dhuluma yao ya uporaji wakishirikiana na vituo vingine vya Kiislamu,” alisema.
Alichanganua kwamba kwa mujibu wa Katiba ya nchi kila kundi la dini lina haki ya kuendesha kwa uhuru shughuli zake za kidini bila kuingiliwa na madhehebu mengine.
Mufti Simba alitumia fursa hiyo kuwataka Waislamu nchini kutambua madhara ya vitendo vya vurugu na ghasia vinavyoendeshwa na Sheikh Ponda na kikundi chake kuwa ni uvunjaji wa sheria na kamwe havina uhusiano wowote na dini ya Kiislamu.
Akizungumzia kukaa kwake madarakani kwa muda mrefu, Mufti alisema huo ni utaratibu wa dini hiyo kwani ulitumika tangu enzi za mitume.
“Kiongozi wa kidini huondoka madarakani aidha kwa kukiuka taratibu za uongozi kama kufumaniwa, ulevi au kuondoka mwenyewe kutokana na hali mbaya ya kiafya,” alisema.
Hata hivyo, alikanusha uvumi kuwa anajihusisha na uvutaji bangi, badala yake akakiri kuwa awali alikuwa akivuta singara na kwa sasa ana miaka 6 hajihusishi tena na uvutaji huo.
Mufti alitoa wito kwa vyombo vya dola kwamba viangalie utaratibu wa kuwashughulikia watu wanaoleta vurugu kwa kujifanya viongozi wa taasisi hewa na kutoa matamko ya kutishia kuwaondoa viongozi halali.

No comments:

Post a Comment