Wednesday, September 26, 2012

HAYAWI HAYAWI SASA YAMETIMIA CCM-Mgeja, Lembeli, Mkono, Bashe, Kingwangalla, Premji watoswa

HATIMAYE Panga la Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, limewashukia vigogo wa chama hicho na kuwatupa nje ya kinyang’anyiro cha kuwania nafasi za uongozi wa jumuiya za chama na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Wakati panga hilo likiwashukia baadhi ya vigogo, Rais Kikwete ametoa kauli nzito ya kutaka wagombea waliopata kutoa kauli za vitisho dhidi ya chama hicho kufanya kile walichokusudia kukifanya.
Kikwete katika kauli yake hiyo alionekana waziwazi kukerwa na kauli za ‘patachimbika’ au zile za kutishia kujitoa na kujiunga na vyama vya upinzani.
Akizungumza kwa ukali, Kikwete ambaye juzi alitamba akisema CCM haitakufa kama inavyotabiriwa na baadhi ya watu, alihitimisha kauli yake kwa kusema watu wenye kauli za namna hiyo walikuwa hawafai kuendelea kuwa wanachama wa chama hicho.
Panga la Rais Kikwete limewaangukia wagombea wenye nyadhifa zaidi ya moja serikalini na ndani ya chama pamoja na baadhi ya wabunge.
Wengine waliokatwa na vikao hivyo vya juu vya CCM vilivyomalizika jana mjini Dodoma, ni wagombea waliokuwa wakiibua malumbano na wakati mwingine kuikosoa CCM hadharani, makada waliojipambanua kama wapiganaji na wapambanaji wa ufisadi na baadhi ya wabunge walioweka saini zao bungeni kuunga mkono hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ya kutaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ajiuzulu.
Habari kutoka ndani ya NEC, ziliwataja walioenguliwa kuwa ni pamoja na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla na Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana la CCM Taifa (UVCCM), Hussein Bashe.
Bashe na Kigwangalla ambao wamekuwa katika mvutano mkubwa wa kusaka madaraka ndani ya chama, majina yao yalipendekezwa kukatwa kuwania nafasi hiyo kuanzia kwenye sekretarieti, Kamati ya Maadili na Kamati Kuu kabla ya kuthibitishwa na NEC.
Makada hao wamekuwa kwenye mvutano wa kisiasa uliodumu toka mwaka 2010 wakati wa uchaguzi mkuu ambapo Bashe alienguliwa kuwania ubunge, Jimbo la Nzega na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Kigwangalla aliyeshika nafasi ya tatu. Nafasi ya pili ilichukuliwa na mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Lucas Selelii.
Mbali ya hao, panga hilo limemkata Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.
Mgeja na Lembeli nao wamekuwa katika mvutano mkubwa ndani na nje ya chama. Uhasama wao unachochewa na kambi mbili kubwa zenye uhasama mkubwa.
Wengine waliokatwa ni Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Mbunge wa Ludewa, Deo Filukunjombe.
Wabunge hao ni miongoni mwa waliotia saini kutaka Waziri Mkuu Pinda ang’oke. Duru za siasa zinasema kuwa msimamo wa wabunge hao kuhusu Pinda, ndio ulisababisha wakatwe kuwania NEC.

No comments:

Post a Comment