Tuesday, September 25, 2012

AIBU KUU KWENYE MAHAKAMA ZETU,HAKIMU MWINGINE APANDISHWA KIZIMBANI KWA RUSHWA YA TSH 9000000

HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Pamela Kalala, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na makosa mawili ya kuomba na kupokea rushwa ya sh 900,000 kutoka kwa mke wa mshtakiwa aliyekuwa na kesi mbele yake.
Wakili wa Serikali, Allen Kasamala, mbele Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana, alidai kuwa mshtakiwa huyo aliomba rushwa tarehe mbalimbali kati ya Februari mwaka huu, Ilala, jijini Dar es Salaam.
Wakili Kasamala alidai Pamela akiwa mwajiriwa wa Mahakama, kama Hakimu Mkazi na wakala wa Sheria ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), kifungu namba 11 ya mwaka 2007, aliomba rushwa kutoka kwa Josephine Wage, mke wa mshtakiwa katika kesi ya jinai namba 703 ya mwaka 2008, jamhuri dhidi ya Abubakar Mziray na wenzake.
Kasamala alidai Pamela alitenda kosa hilo, ili kumshawishi kutoa uamuzi wa kumpendelea mumewe.
Alidai kuwa katika shtaka la pili, Hakimu Mkazi Pamela anadaiwa tarehe mbalimbali Februari mwaka huu, eneo la Manispaa ya Ilala, akiwa na wadhifa huo, alipokea sh 800,000 kutoka kwa Josephine.
Pia anadaiwa Februari 6 mwaka huu, katika eneo hilo, alipokea tena sh 100,000 kutoka kwa Josephine.
Pamela alikana mashtaka yote ambapo upande wa jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kwamba hauna pingamizi na dhamana iwapo mshtakiwa atatimiza masharti yatakayotolewa.
Hakimu Katemana alisema ili mshtakiwa apewe dhamana ni lazima asaini bondi ya sh milioni moja na awe na mdhamini mmoja mwenye barua kutoka sehemu inayotambulika ambaye naye atatakiwa kusaini hati ya sh milioni moja.
Aidha mshtakiwa huyo aliweza kutimiza masharti hayo ya dhamana ambapo hakimu Katemana alimwachilia kwa dhamana hadi Oktoba 23, mwaka huu, kesi itakapotajwa tena.
Hii si mara ya kwanza kwa mahakimu kufikishwa mahakamani hapo kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa.
Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Jamila Nzota, alifikishwa katika mahakama hiyo  mwaka 2010 na alitiwa hatiani kwa makosa hayo na kufungwa jela miaka mitatu.

No comments:

Post a Comment