Thursday, September 27, 2012

Malema ''Sitishiki na hatua ya mahakama'-Malema ni maarufu sana Afrika Kusini kwa ukakamavu wake wa kutetea maslahi ya wananchi

Julius Malema akiwahutubia mamia ya wafuasi wake
Julius Malema amewaambia wafuasi wake kuwa katu hatishiki na uamuzi wa mahakama kusema kuwa ana kesi ya kujibu.
Mahakama hii leo ilimwachilia kwa dhamana Malema anayekabiliwa na shtaka la kuhaulisha pesa.
Malema ambaye aliwahutubia wafuasi wake nje ya mahakama, pia anatuhumiwa kwa kutumia nafasi yake ya zamani kama kiongozi wa tawi la vijana la ANC kujitajirisha yeye na washirika wake wa biashara.
Washirika wake wengine wanne nao walikabiliwa na mashtaka sawa na hiyo katika kesi yao iliyosikilizwa hapo jana.
Katika hotuba yake kwa mamia ya wafuasi wake nje ya mahakama mjini Polokwane, bwana Malema alisema ataendelea na juhudi zake za kutetea maelefu wanaoishi katika umaskini nchini humo.
Seng'enge zilizungushwa katika eneo la mahakama hiyo iliyopo Polokwane, mji mkubwa wa jimbo analotokea mwanasiasa huyo,Limpopo.
Wafuasi wake wanasema mashtaka hayo yameshinikizwa kisiasa.
Wakiimba na kucheza nje ya mahakama hiyo wafuasi wengi wa chama hicho cha ANC tawi la vijana walishikilia mabango yaliosema 'Muacheni kiongozi wetu'.
Maafisa wa usalaman walidhibiti ulinzi na kulikuwa na utulivu mkubwa.
Julius Malema na washirika wake wa kibiashara wanashutumiwa kwa kufaidi kutokanana na mikataba ya serikali katika jimbo la Limpopo, tuhuma ambazo anazikana. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 31 pia anachunguzwa katika kesi tofauti ya ukwepaji kulipa ushuru.
Malema ni maarufu sana Afrika Kusini kwa ukakamavu wake wa kutetea maslahi ya wananchi na maisha yake ya kifahari, huku akijitambulisha kama mpiganiaji uhuru wa uchumi.
Alitimuliwa kwenye chama hicho tawala mnamo mwezi Aprili akishutumiwa kwa kuzusha migawanyiko katika chama hicho.
Ni mkosoaji mkali wa a Jacob Zuma, hivi karibuni akimshutumu rais huyo kwa alivyoushughulikia mgomo wa wachimba migodi wa Marikana.
Kwa mujibu wa mwandishi wa masuala ya Afrika, Andrew Harding, baadhi ya watu Afrika kusini wanaamini anafikishwa haraka mahakamani, ikiwa ni chini ya wiki moja baada ya kutolewa waranti ya kukamatwa kwake, ili kuimarisha nafasi ya kisiasa ya Zuma.
Mwandishi wetu anaeleza kwamba huenda ikawa ni kesi ya muda mrefu, ambayo huenda ikatoa nafasi ya kujulikana ukweli kuhusu suala hilo la rushwa, ambalo watu wengi wanaamini inaitia nchi hiyo doa.
chanzo bbc.

No comments:

Post a Comment