Friday, September 28, 2012

Wamiliki wote wa shule igeni mfano huu wa kanisa katoliki Moshi- Marufuku kupandisha ada kiholela

KANISA Katoliki Jimbo la Moshi, mkoani Kilimanjaro limepiga marufuku upandishwaji wa ada kiholela pamoja na michango isiyo ya lazima kwa shule zote zinazomilikiwa na kanisa hilo.
Kutokana na hali hiyo, wakuu wote wa shule hawataweza kupandisha ada pamoja na michango mpaka kupata baraka kwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Izack Amani.
Akizungumza kwenye mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Kisomachi inayomilikiwa na kanisa hilo, Mkurugenzi wa Elimu wa jimbo hilo,William Ruaichi, alisema wameamua kufanya hivyo, ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wazazi kutokana na baadhi ya shule kuongeza ada bila kufuata taratibu.
“Ni kweli kumekuwepo na malalamiko kwa wazazi kuwa ada ni kubwa pamoja na michango ambayo imekuwa ikitozwa na shule za Katoliki, tumekwisha kuwaandikia barua kuwa hakuna ada itakayotozwa au michango bila wakuu wa shule kuwasiliana na askofu,” alisema Ruaichi.
Alisema suala la upandishwaji wa ada wakati mwingine linatokana na baadhi ya shule kuwa na watumishi wengi wasiokuwa wa lazima pamoja na kutofanyiwa ukaguzi wa fedha, hivyo kutokuwa na matumizi ya fedha za shule hizo.
Kwa upande wake, mkuu wa shule hiyo, Flugensi massawe, alisema umefika wakati jamii kushirikiana kwa pamoja katika kutoa mchango kwenye sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuwasaidia watoto ambao wanahitaji kusoma, lakini wazazi wao hawana uwezo.
Alisema jamii haijahamasika katika kuchangia elimu kama sherehe, hivyo kutoa wito kuiga kwa nchi jirani kama Kenya ambazo wameweka vipaumbele katika kuchangia zaidi masuala ya elimu.

No comments:

Post a Comment