Rais wa Gambia Yahya Jammeh
ametoa amri kuwa wafanyikazi wote wa umma watafanya kazi siku nne pekee
kwa wiki kuanzia leo Ijumaa . Ijumaa sasa itakuwa siku ya mapumziko sawa
na Jumamosi na Jumapili.
Rais Jammeh anasema iwapo wananchi wa Gambia
watafanya kazi siku nne kwa wiki watapata muda zaidi wa kusali,
kushiriki maswala ya kijamii na kulima mashamba yao.Amesema kuwa mishahara yao haitapunguzwa kwa sababu kwa siku hizo nne watu watafanya kazi zaidi ya saa za kawaida ili kulipiza siku ya tano.
Shule za kitaifa hazitafunguliwa tena siku ya ijumaa.Sekta za kibinafsi zitafanya kazi hadi ijumaa lakini hazitaweza kufanya biashara yoyote na serikali siku hiyo.
Rais Jammeh mwenye historia ya kuwa na tabia za kustaajabisha, hajawapa wananchi Gambia muda wa kujiandaa kwa mfumo huo mpya.
Mwaka 2007 alitangaza kuwa anaweza kutibu ungonjwa wa Ukimwi kwa muda wa siku tatu akitumia mchanganyiko wa dawa za kienyeji. Tamko hilo lililaaniwa na wataalam wa matibabu kote duniani.
Mwaka jana wafungwa tisa waliokabiliwa na hukumu ya kifo walipigwa risasi na maafisa wa polisi huku rais Jammeh akiapa kuwaua wafungwa wote waliohukumiwa kifo katika muda wa wiki kadhaa. Baadaye alisimamisha mauaji hayo baada ya kukosolewa vikali na jamii ya kimataifa.
No comments:
Post a Comment