Ndiyo maana tunasisitiza kwamba kwenye KATIBA mpya tuangalie utaratibu
wetu wa namna ya kumpata spika na naibu spika. Kama hatufanyi hivyo
maspika wetu lazima waendeleze umbumbumbu wa kuitetea CCM iliyochoka,
kuchakaa na sasa inatafuta nani imfie, kila mwana CCM anajua itakufa,
kina ndungai na makinda wanachofanya ni kukwepa isifie mikononi mwao.
Mchezo huu wa mechi ya simba na yanga kuamuliwa na refa ambaye ni
mshabiki na mwanachama wa simba au yanga unatugharimu katika kila eneo.
Ukienda hata kwa tume ya taifa ya uchaguzi ati inateuliwa na mwenyekiti
wa CCM halafu eti tunategemea wateuliwa watende haki kwa vyama vya
upinzani.
Mchezo huu pia uko hata kwa uteuzi wa wakuu wa vyombo
vya ulinzi na usalama, nchi hii huwezi kushikilia nafasi ya KOVA na
nyingine nyingi za juu za polisi kama huiungi mkono CCM. Maafisa wa juu
wa polisi wenye msimamo wa kutetea wananchi wote kwa usawa hutawasikia
hata siku moja wamekuwa ma-RPC n.k......
Upuuzi huu unaendelea
hadi kwa jeshi la ulinzi na usalama, nako kama huishabikii CCM huwezi
kuwa mtu yeyote wa maana. Utaishia kuwa ofisa wa makao makuu ya jeshi,
basi. Tuna matatizo na uozo mkubwa sana kwenye mfumo wetu wa uongozi wa
idara na vyombo mbalimbali vya serikali usiozingatia sifa na uwezo wa
mteuliwa. Sasa tumejenga taifa ambalo ili mtu apate wadhifa muhimu sana
kwa mihimili ya dola lazima kwanza alambe nyayo za CCM.
Hata
ukienda huko mikoani, nyadhifa muhimu kama za ukuu wa wilaya na ukuu wa
mkoa zina nguvu kubwa sana. Lakini wanaoteuliwa kushika nyadhifa hizo
ATI lazima kwanza wawe makada wa CCM na watakaoitetea kwa nguvu. Mkuu wa
mkoa atatendaje haki ikiwa anateuliwa tu ki-CCM ili eti akatetee
wananchi wote na ambao hawakumchagua? Ni jambo lisilowezekana asilimia
MIA moja. Ndiyo maana wakuu wa mikoa na wilaya kila kukicha huzalisha
vurugu mahali walipo, wanasahau jukumu la kusimamia haki na wajibu wa
wananchi wote kwa ujumla, wamekaa kutetea CCM tu.
Binafsi
simshangai Job Ndungai wala wenzie, tatizo ni kubwa kupita hapo. Job
Ndugai anatekeleza kule wanachotekeleza majaji na mahakimu mahakamani
katika kesi nyingi ambazo lazima CCM ilindwe.
Job Ndungai
anafanya yale wanayofanya wakuu wa vikosi vyetu vya ulinzi na usalama
ili kuilinda CCM huku wakisahau kazi yao KUU ya kulinda raia na Mali
zao.
Sikushangazwa na chochote kwa sababu Job Ndungai na Anna
Makinda siku zote wanafanya kile wanachofanya wenzao tume ya taifa ya
uchaguzi, wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na
watendaji wa kata na vijiji... Ni kazi ile ile, kuilinda CCM hadi tone
lao mwisho la damu. ......CCM kwanza, maslahi ya wananchi baadaye!
Na ukifuatilia asili ya majukumu ya viongozi utakuta yapo mawili
makubwa. Jukumu la kwanza ni kusimamia haki na usawa kwa wananchi wote
bila kujali rangi, dini, kipato, tofauti za itikadi, jinsia n.k. Na
jukumu la pili ni kusimamia maadili na miongozo ya taaluma. Hizi ndizo
kazi KUU mbili za viongozi kokote kule waliko.
Sasa mfumo wetu
wa nchi umeoza katika eneo hili. Viongozi hawasimamii haki na usawa ili
kujenga jamii yenye matumaini makubwa. Viongozi hawasimamii maadili na
miongozo ya taaluma zao, hapo ndipo tunalipeleka taifa kuzimu.
Wanachosahau kina ndungai ni kwamba, hawatakuwepo madarakani milele.
Wataondoka tu, na killichofanyika jana DODOMA ni kiashiria kingine
sahihi kwamba CCM wamebebana weeeee hadi wamechoshana wao kwa wao.
Wamekosa mbinu za kuongoza baada ya hii ya kubebana kufikia ukomo. Na
bahati nzuri, wananchi wameanza kutambua kuwa serikali iliyoko
madarakani iko kwa ajili ya ka-kikundi kadogo ka ma-CCM wachache wezi na
mafedhuli.
Mafedhuli hawa wanaweza kukuua hadharani na bado
wakajitetea, wamefanya hivyo ULIMBOKA na wamejaribu kutengeneza kiini
macho, wamefanya hivyo kwa Mwangosi na wao wanaendelea kuponda raja,
wanafanya hivi kila siku tena waziwazi. Wanaua hadharani na wanalindana
ndani ya jamii yetu.
Kitakachotokea siku si nyingi ni anguko
rasmi la CCM. Hawana hoja za kuzuia upinzani tena, sasa ni kutumia
MAGUVU na kukwepa kujadili kila kitu. TUJIPANGE KUPOKEA KIFO NA MAZIKO
RASMI YA CCM, NDUNGAI HAJAKOSEA .... ANAENDELEZA ALICHOTUMWA NA
WATAFUNAJI WA NCHI HII.
na Julius Mtatiro
No comments:
Post a Comment