MGOMBEA urais wa Kenya kupitia Muungano wa Cord, Raila Odinga
ameunga Mkono ujumbe wa Rais wa Marekani ,Barack Obama aliyetoa kwa njia
ya mtandao wa kuhimiza amani nchini humo.
Waziri Mkuu huyo, Raila Odinga alisema kwamba Wakenya wanatakiwa kupiga kura kwa kufuata wito huo wa amani uliotolewa na Obama.
“Wakenya wote wana hamu ya kuona hakuna ghasia zitakazotokea hususan za kikabila na kidini katika kipindi hiki cha uchaguzi,’’ alisema.
Alisema urais siyo sehemu ya masilahi binafsi bali ni kwa ajili ya wananchi wake anaowaongoza kama alivyosema Obama.
Alisema kwamba, ujumbe huo wa Obama kwa Wakenya unasaidia kuondoa ghasia na tafaruku mbalimbali katika kipindi cha uchaguzi nchini humo.
“Nafurahi kusema kwamba Obama alichokisema katika hotuba yake ni mtu ambaye anaifahamu vizuri Kenya na alikuwa anaifuatilia kwa karibu zaidi kipindi cha chaguzi kuu. Hivyo Wakenya hatuna budi kuwa makini na nchi yetu,” alisema Raila.
Alisema uongozi mbaya na ukabila ni vitu ambavyo wanatakiwa kuvipiga vita nchini humo kwa hali yoyote ile kwani ndiyo vyanzo vya uchochezi.
Alisema ikiwa atachaguliwa itakuwa ndiyo mwisho wa ukabila nchini humo kwani atalipigania kwa hali na mali.
Pia aliirushia lawama tume ya mawasiliano nchini humo kuhusu kufungwa kwa vituo sita vya upeperushaji matangazo vya Royal Media Services nchini humo.
“Tunajua hili ni jaribio la baadhi ya maofisa wa Serikali kuzima vyombo vya habari kabla ya uchaguzi,” alisema.
Katika hotuba yake Obama aliwahimiza Wakenya wawaepuke watu watakaowachochea au kutumia vitisho ili wachaguliwe.
“Kenya lazima iruhusu uchaguzi Huru na wa haki, wakenya waahidi kutatua mizozo ya chaguzi mahakamani na wala si kwenye barabara,’’ alisema Obama.
No comments:
Post a Comment