WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameunda tume itakayochunguza sababu
za idadi kubwa ya wanafunzi wa kidato cha nne kuvurunda katika matokeo
ya mtihani huo yaliyotangazwa hivi karibuni.
Katika matokeo hayo ambayo yanatajwa kuwa mabovu
kuliko yoyote yaliyowahi kutokea katika historia ya Tanzania, asilimia
60 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walipata daraja sifuri.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo
alisema kuwa tume hiyo inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote wiki ijayo,
ambapo itajumuisha Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi.
Lyimo aliwataja wadau wengine watakaohusika katika
uchunguzi huo kuwa ni kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kamati ya
Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari
Tanzania (Tahossa)
“Tume hiyo itahusisha asasi zisizo za kiserikali
(NGOs), zinazojishughulisha na masuala ya elimu. Wazazi, walezi na
wananchi wote kwa jumla watoe ushirikiano kwa tume, ili ifanye kazi kwa
ufanisi,” alisema Lyimo.
Akizungumzia hatua hiyo ya Pinda, Mbunge wa Iringa
Mjini, Peter Msigwa (Chadema) alisema wazo hilo ni zuri, lakini kuunda
tume bila utendaji hakutakuwa na maana katika elimu nchini.
Alisema kuwa tume nyingi zimeundwa, lakini hakuna
tume iliyowahi kuleta mabadiliko na kwamba mara nyingi matokeo ya
uchunguzi huwa ni ya kuidhalilisha Serikali.
Msigwa aliongeza kuwa tume hizo hutumia fedha za wananchi na matokeo yake hayatangazwi wala kufanyiwa kazi.
“Serikali ingewaita wadau wa elimu na kuzungumza
nao ijue wapi penye matatizo. Halafu maelezo ya wadau hao yajadiliwe
bungeni,” alisema Msigwa akiitaka Serikali kuacha kuchanganya ushabiki
wa kisiasa pindi zinapowasilishwa hoja muhimu za maendeleo ya taifa na
kuongeza:
“Juzi hoja ya Mbatia imetupwa kapuni, hata sisi
wabunge tunapeleka hoja nyingi, lakini hazifanyiwi kazi, kwa sababu ya
ushabiki.”
Kiongozi wa Jukwaa la Katiba nchini, Profesa Issa Shivji aliwataka Watanzania wasubiri kuona tume hiyo itafanya nini.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Profesa Benson Bana, alitaka suala la elimu lisichukuliwe kisiasa,
badala yake Serikali itatue kero za elimu, alizosema zinajulikana na
kwamba hakuna haja ya kumtafuta mchawi.
No comments:
Post a Comment