Monday, February 11, 2013

Njia Kilimanjaro Marathon 2013 zatangazwa

WAANDAAJI wa Kilimanjaro Marathon 2013 wametangaza kwamba mbio za mwaka huu zitafanyika katika njia zile zile zilizotumika mwaka jana.
Mbio za mwaka huu zinatarajiwa kurindima mjini Moshi mkoani Kilimanjaro Machi 3.
John Addison, Mkurugenzi Mtendaji wa Wild Frontiers, waandaaji wa tukio hilo, alisema katika taarifa jana kwamba njia zitakazotumika kwa ajili ya Kilimanjaro Marathon 2013 ni kuanzia Uwanja wa Chuo cha Ushirika (MUCCoBS) kuelekea katikati ya mji na kisha kufuata barabara kuu ya kwenda Dar es Salaam kwa takriban kilomita 8 hadi 9.
Baadaye watageuka na kurudi Moshi mjini kupitia katikati ya mji na baadaye watapandisha mwinuko kidogo kuelekea Mweka.
“Wanariadha watafurahia zaidi sehemu hii, kwa sababu ina mandhari ya kuvutia na kutakuwa na washangiliaji wengi kando ya barabara,” alisema na kuongeza.
Sehemu ya kupandisha kuelekea Mweka inahitaji kupanda kwa taratibu, lakini kwa sababu Mlima Kilimanjaro ni kivutio na uwepo wa wananchi wanaoshangilia muda unaenda haraka na kuwasaidia wakimbiaji kumaliza mapema.
Alisema kuwa hadi kituo cha Mweka ambako wanaridha wanageukia kurudi Uwanja wa Ushirika, inakuwa ni takriban kilometa 32 tangu kuanza mbio ndefu ya kilomita 42.
Baada ya hapo kipande kilichobaki kinakuwa ni mteremko kuelekea uwanjani mwisho wa mbio na njia nzima ni mteremko tu.
Aliongeza kuwa kwa wale watakaoshiriki Nusu Marathon, mbio zitaanzia Uwanja wa MUCCoBS, mahali ambapo ni tambarare na baadaye watapandisha kwenye mwinuko kidogo kuelekea Mweka kama ilivyo zile mbio ndefu kabla ya kurudi takriban kilomita 10, kuelekea tena uwanjani.
“Kutakuwa na meza za maji kama ilivyo kawaida na magari maalumu ya kunyunyizia maji mithili ya mvua kando ya barabara, huduma ambazo zimeandaliwa maalumu kuwafanya wanariadha waendelee kuwa na nguvu wakati wote wa mbio hizo,” alisema.
Kuhusu burudani, Addison alisema kuwa hali ya uwanjani itakuwa ya kusisimua kutokana na burudani za uhakika kutoka bendi za muziki wa nyumbani zitakazokuwepo, chakula cha kutosha, nyama choma, vinywaji na bila kusahau mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run ambazo pia zinatarajiwa kuleta msisimko wa aina yake.
“Ili kuhakikisha usalama wa wakimbiaji, baadhi ya barabara zitakuwa zimefungwa asubuhi siku ya mbio, lakini kutakuwepo na njia mbadala kuzunguka mji kwa ajili ya wakazi wa Moshi. Wakazi wa Moshi ambao wanatarajia kukimbia pamoja na wakimbiaji wengine watakaofika Moshi mapema, wanaweza kuanza mazoezi katika njia hizo hili kupata uzoefu wa njia na kujiandaa vizuri kwa ajili ya mbio,” alisema.
Mbio hizo zinaratibiwa na Executive Solutions na kudhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, huku wadhamini wengine wa tukio hilo wakiwa ni pamoja na Vodacom Tanzania (5km Fun Run), GAPCO (Nusu Marathon Walemavu), Tanga Cement, CFAO Motors, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, New Arusha Hoteli, Kilimanjaro Water, FastJet na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA).

No comments:

Post a Comment