HUDUMA za matibabu na upasuaji wa moyo zitaanza kupatikana
nchini, kutokana na mipango ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na ile ya
Aga Khan.
Hatua hiyo itawawezesha wagonjwa wa moyo nchini
kutopelekwa kwa wingi nje ya nchi kama ilivyo sasa. Pia itaokoa
mamilioni ya fedha ambazo zimekuwa zikitumika kugharimia tiba hiyo nje
ya nchi.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa Hospitali za Aga
Khan Tanzania, Dk Jaffer Dharsee akiwasilisha taarifa kuhusu ongezeko la
magonjwa ya moyo nchini katika kongamano la wataalamu wa magonjwa hayo
alisema, jitihada kubwa zinafanywa ili kuhakikisha tiba ya moyo inaanza
kutolewa nchini.
Alisema Hospitali ya Muhimbili inakusudia kuanza
kutoa tiba hiyo katika kipindi cha miezi miwili ijayo baada ya ujenzi wa
taasisi yake kukamilika, wakati Hospitali ya Aga Khan itaanza kutoa
matibabu hayo mwakani. Kongamano hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki
iliyopita jijini Dar es Salaam.
Hatua ya kuwapo kwa tiba za moyo nchini,
itawezesha gharama za tiba kupungua kwa asilimia 57.1, ikilinganishwa na
gharama za tiba hizo nje ya nchi.
Dk Dharsee alisema hapa nchini gharama za tiba
zitakuwa Dola za Marekani 1,500 sawa na Sh2.4 milioni tofauti na Dola
3,500 (Sh5.6 milioni) zinazotumika kumpeleka mgonjwa kwa ajili ya
upasuaji nchi za nje kama India.
Alisema gharama hiyo inatokana na kuwapo kwa
gharama kubwa zinazohitajika kuandaa maabara hiyo ambayo ina thamani ya
Dola 200 milioni (Sh320 bilioni) bila kuingiza gharama za wataalamu wa
kuiendesha na kuhudumia wagonjwa.
Muhimbili
Habari ambazo gazeti hili lilizipata zinasema
kwamba Taasisi ya Tiba ya Moyo Muhimbili itaanza kazi zake rasmi katika
muda wa miezi miwili kuanzia sasa, baada ya kukamilika kwa jengo la
taasisi hiyo, kuanzisha maabara maalumu ya upasuaji na matibabu ya moyo
kukamilika.
Ujenzi wa jengo hilo ulianza miaka mitatu
iliyopita kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, iliyotoa
Sh16.22 bilioni wakati Serikali ya Tanzania ilichangia Sh6 bilioni.
Mei 2008 Hospitali ya Muhimbili ilianzisha Kitengo
cha Tiba ya Moyo na Figo, ambacho kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano wa
hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha alisema kwamba kimeshatoa matibabu
kwa zaidi ya wagonjwa 300 tangu kuanzishwa kwake.
Aga Khan
Aga Khan
Kwa upande wa Aga Khan, Dk Dharsee alisema hospitali yake
imewekeza kiasi cha Dola za Marekani 4.6 milioni (Sh7.36 bilioni)
kuandaa wataalamu wa kuwahudumia wagonjwa wa matatizo ya moyo.
Alisema licha ya maandalizi ya kuleta huduma za
upasuaji nchini, hospitali yake imeanza kutoa huduma za kliniki bure kwa
vipimo na tiba ndogo ndogo kila Jumatano na Alhamisi.
“Wastani wa wagonjwa 10 wanaofika hospitalini kwetu tumegundua, wanne wana ugonjwa wa moyo,” alisema Dk Dharsee.
Alisema mitindo ya maisha isiyofaa kama uvutaji wa
sigara, ulaji wa vyakula usiozingatia afya, ulevi na uzembe wa
kutofanya mazoezi mara kwa mara ndiyo vimechochea kwa kiasi kubwa
ongezeko la magonjwa ya moyo.
“Hivi sasa takriban asilimia 20 ya watu waishio
mijini wanaongezeka uzito kwa kiwango kikubwa jambo ambalo linatishia
ongezeko la magonjwa ya moyo kama shinikizo la damu na kupooza,” alisema
Dk Dharsee.
“Mwaka 2002 kulikuwa na vifo ya takriban watu
46,000 kutokana na matatizo ya moyo na idadi hiyo inategemewa kuongezeka
mpaka 63,000 ifikapo 2015 na 85,400 hapo 2031.
Aliongeza kuwa magonjwa hayo kunaiongezea Serikali
mzigo pamoja na kuathiri uchumi wa familia kwa kuwa mwaka 2005 pekee
inakadiriwa kuwa Tanzania ilipoteza Dola 100 milioni kwa ajili ya kutibu
magonjwa ya kisukari, kupooza na shinikizo la damu.
No comments:
Post a Comment