Kila Mtanzania sasa anajadili matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi mwanzoni mwa wiki hii. Matokeo hayo yanaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne walipata daraja la nne na daraja la sifuri. Dara la Sifuri limebeba asilimia 60 ya matokeo yote. Taifa limepata mtikisiko mkubwa kuona vijana wake wakiwa wamefeli kwa kiwango hiki.
Hata hivyo hii sio mara ya kwanza kupata matokeo ya namna hii. Ukiangalia matokeo ya kidato cha nne kuanzia mwaka 2009 utaona kuwa kila mwaka wanafunzi wanaofeli wanaongezeka. Mwaka 2011, wanafunzi 302,000 sawa na asilimia 89 ya wahitimu wote wa kidato cha nne walipata daraja la nne na sifuri. Mwaka 2010 wanafunzi 310,000 ambao ni asilimia 90 ya wahitimu walipata madaraja hayo ya chini kabisa na mwaka 2009 jumla ya wanafunzi 195,000 sawa na asilimia 78 ya wahitimu wote walipata madaraja ya sifuri na daraja la nne. Kila mwaka matokeo yakitangazwa kuna kuwa na mjadala wa wiki moja au mbili, wabunge tunapiga kelele kidogo kisha tunasahau kabisa suala hili mpaka matokeo mengine.
Hivi tumewahi kujiuliza hawa vijana wanaoishia kidato cha nne wanakwenda wapi? Wanafanya nini? Hii nguvu kazi kubwa ya Taifa inapotelea wapi?
Ni vema ifahamike kwamba Tanzania ni Taifa la vijana na watoto. Kwa mujibu wa taarifa za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, hivi Tanzania ina jumla ya vijana 38 milioni wa chini ya umri wa miaka 35 , hii ni sawa na idadi ya watu waliokuwepo Tanzania mwaka 2003. Asilimia 78 ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 35 na nusu ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 17. Kwa takwimu hizi ni dhahiri kwamba suala moja kubwa kuliko yote linalohusu Watanzania ni Elimu. Suala moja kubwa linaloweza kujenga au kubomoa Taifa hili ni Elimu. Suala moja kubwa linaloweza kuepuka matabaka katika nchi ni Elimu. Tena Elimu Bora, na BURE.
Kuna nadharia inaitwa ‘gawio la idadi ya watu’ na ‘bomu la idadi ya watu’. Nadharia hizi zatumika kuelezea namna mataifa yanaweza kufaidika au kupata hasara kutokana na kuwepo kwa nguvu kazi kubwa ambayo ama inatumika kwa faida ya nchi hiyo kwa kufanya kazi na kuongeza uzalishaji ama inatumika kwa kwa kukaa tu kwenye vijiwe na kupiga soga. Taifa ambalo linaandaa vijana wake kwa maarifa na stadi za kazi huvuna gawio (demograpich dividend). Mataifa yaliyofaidika na hali hii ni kama India, Uchina na Ujapani ambapo nyakati wana vijana wengi sana kuliko wazee vijana hawa walipewa ujuzi mkubwa na stadi za maisha na hivyo kuongeza uzalishaji mali kwa Taifa. Watu ndio mtaji mkuu wa Taifa lolote lile duniani. Taifa ambalo haliandai vijana wake kupata elimu huingia kwenye mgogoro mkubwa maana kundi la vijana wasio na kazi na wasio na maarifa yeyote ni sawa sawa na bomu.
Tanzania tuna chaguzi katika masuala haya mawili, ama tuvune gawio la kuwa na vijana wengi sana kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika Elimu au tusubiri bomu lilipuke. Kwa matokeo haya ya kidato cha nne kwa miaka minne iliyopita, ni dhahiri tumeamua kulipikiwa na bomu.
Tunajua chanzo cha matokeo haya. Watoto hawasomi wala kujifunza shuleni. Hasa watoto wa vijijini ambapo hakuna walimu wala vitabu. Tumejenga mataifa mawili ndani ya nchi moja, Taifa la masikini na wana shule zao, wanapata masifuri kila siku. Taifa la walalaheri wana shule zao na wanapata madaraja ya juu. Hawa ndio watakaoenda vyuoni na wenye elimu wataendelea kutawala. Suluhisho ni moja tu, kuamua kwa dhati kabisa kuwekeza kwenye elimu kwa kuhakikisha kuna walimu wa kutosha, walimu wanalipwa vizuri na kuishi kwenye mazingira mazuri. Iwe na marufuku wenye kufeli ndio wafanye kazi ya ualimu.
Ni lazima kuhakikisha kuwa kunakuwa na vitabu vya kutosha kwenye mashule. Serikali ihakikishe kwamba inaingia makubaliano na wachapishaji wa vitabu wa ndani na kutoa vitabu vinavyojenga Taifa kwa kutoa maarifa ya uhakika kwa watoto. Ieleweke kwamba shughuli ya uchapishaji wa vitabu ni ajira tosha iwapo tutawezesha wachapishaji wa ndani kutoa vitabu vingi zaidi na vyenye ubora.
Matokeo ya mwaka huu ya kidato cha nne yanatuambia jambo moja kubwa sana, kwamba sisi ni Taifa linalokufa. Tuweke siasa pembeni na kahakikisha kwamba kunakuwa na uwajibikaji kwa viongozi kutokana na matokeo ya namna ya hii ya vijana wetu. Tusione tabu kubadilisha mawaziri wa Elimu kila mwaka kwa kuwafukuza kutokana na matokeo ya mitihani ya watoto wetu. Hii itafanya Waziri ajue umuhimu wa elimu anayoisimamia. Tukate mzizi wa fitina, elimu ni suala la uwajibikaji. Makala zijazo tutaona hatua za kuchukua ili kuhakikisha hawa watoto zaidi ya 300,000 waliofeli tunawafanya nini.