Friday, February 1, 2013

Mbunge ahoji mkakati wa serikali kwa waliokosa nafasi vyuo vikuu

MBUNGE wa Viti Maalum, Rita Mlaki (CCM), amehoji mkakati uliopo wa serikali katika kuhakikisha wanafunzi walio na sifa za kujiunga na vyuo vikuu na kukosa nafasi waweze kujiunga na vyuo vilivyosajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Nchini (NACTE).Pia alihoji mpango wa serikali wa kuwaelekeza wanafunzi hao kujiunga na vyuo vikuu vilivyosajiliwa kama ilivyo kwa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) inavyosaidia waliokosa nafasi kujiunga na vyuo binafsi.
Rita alizidi kuibana serikali ieleze hatua inazochukua katika kuhamasisha mfumo huo wa kuingia chuo kikuu kupitia ‘Technical Education’ ambao wengi hawaufahamu.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema kuwa serikali kupitia NACTE huandaa na kutoa orodha ya vyuo vyenye sifa ili kuwawezesha wahitaji kuvitambua vyuo hivyo.
Mulugo alisema kuwa kwa kuwa vyuo ambavyo vimetajwa na mbunge vinajiendesha kwa uhuru ulio kamili, vina wajibu wa kujitangaza ili wale wenye sifa ambao hawakuchaguliwa na vyuo vikubwa waweze kujiunga navyo.

No comments:

Post a Comment