Tuesday, February 12, 2013

Tanzania yang’ara maajabu saba,imepata tuzo tatu za maajabu saba ya africa

TANZANIA imepata tuzo tatu za maajabu saba ya Afrika kupitia vivutio vyake bora vya utalii vya Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Serengeti ambayo viliongoza kwa kupata kura nyingi kuliko nchi nyingine yoyote.
Akitangaza matokeo hayo jana mjini hapa, rais wa taasisi iliyoandaa tuzo hiyo Dk. Phillip Imler wa Marekani, mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema ushindi huo umetokana na kuwa Tanzania ina vivutio vya kipekee.
Akielezea hifadhi ya taifa ya Serengeti, alisema kuwa ndiyo hifadhi ya kipekee iliyopata kura nyingi kutokana na tabia ya misafara ya wanyama wanaohama kwa msimu.
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema kuwa nchi za Afrika zina vivutio vingi vya utalii na fursa kubwa ya kukuza pato kupitia utalii huo.
Alisema anaamini kutokana na sifa ambayo Tanzania imeipata kupitia vivutio vyake vitatu itaendelea kuvitunza kuhakikisha kuwa vinavutia zaidi watalii na kuongeza pato la taifa.
“Afrika ina vivutio vingi vyenye kuvutia hivyo kila nchi ni lazima ijivunie rasilimali hizo kwa kuvitunza na kuviendeleza,” alisema.
Alisema kwa Tanzania ni bahati ya pekee kuweza kupata tuzo tatu za maajabu saba ya Afrika ambazo ni Mlima Kilimanjaro, Bonde la Ngorongoro pamoja na hifadhi ya Taifa ya Serengeti hivyo ni wajibu wa kuvitunza na kuviendeleza.
Alisema kuwa iwapo Watanzania wataendeleza tabia ya utunzaji wa vivutio vilivyoko nchini, nchi itaendelea kupata sifa duniani kote.
Naye Mkurugenzi wa Hifadhi za Taifa (Tanapa), Dk. Alan Kijazi, alisema Mlima Kilimanjaro ni mlima mrefu barani Afrika na hivyo una kila sababu ya kushinda na Watanzania waendelee kuutunza.
Kuhusu hifadhi ya Ngorongoro alisema kuwa imeshinda kwa kuwa na wanyama wa kila aina kama Big Seven: simba, tembo, viboko, nyati, vifaru, sokwe na mamba.
Mbali na Tanzania Dk. Imler alivitaja vivutio vingine vilivyoshinda kuwa ni Red sea Reefs, Okavango Inland delta iliyoko nchini Botswana, Sahara Desert na River Nile.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alisema ushindi huo ni historia kubwa duniani na kwamba ni jambo la Watanzania wote kujivunia.

No comments:

Post a Comment