Saturday, February 2, 2013

Kawambwa kuwasilisha mitalaa bungeni Februari 6

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa ameagiza zichapishwe nakala 300 kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni wiki ijayo.
 
Kawambwa ametoa agizo hilo siku tatu baada ya mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia kumkalia kooni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa juu ya kuwasilisha bungeni mtalaa wa elimu.
Kwa siku tatu, kuanzia Jumatano wiki iliyopita, Mbatia alikuwa akimshinikiza Kawambwa kuwasilisha mtalaa wa Elimu ya Msingi na Sekondari ambao alisema haukuwahi kuwepo Tanzania tangu mwaka 1961.
Hata hivyo, katika hoja yake ya utetezi, Kawambwa alisema ulikuwapo na ulifanyiwa marekebisho mwaka 1967, mwaka 1979, mwaka 1997 na mabadiliko ya mwaka 2004/09 kulingana na mabadiliko yalivyokusudiwa.
Mbali na kuelezea hayo, Mbatia alimtaka Kawambwa kuwasilisha nakala ya mtalaa huo ambao hata hivyo alishindwa na kutoa sababu mbalimbali.
“Mimi niko tayari kujiuzulu ubunge ikiwa Kawambwa ataleta mtalaa hapa, nilimfuata mara
kadhaa ofisini kwake bila mafanikio,
jana (juzi) asubuhi nikamfuata nikamwambia nipatie basi ili nijiridhishe na naweza hata kufuta hoja yangu, lakini alikataa,” alisema Mbatia.
Juzi wakati akihitimisha kikao cha Bunge, Naibu Spika, Job Ndugai alisema kuwa Waziri
Kawambwa ameagiza nakala 300 za mitalaa kwa ajili ya wabunge na itawasilishwa kwa Katibu wa Bunge, Februari 6.
Awali akitolea ufafanuzi suala hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema, “Ni kweli iko kwenye hansard kwamba mitalaa ya elimu ya msingi na sekondari itawasilishwa katika kikao hiki, lakini kikao hakijamalizika, wakati wowote tutaileta.”
Akizungumza juzi jioni, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alisema, “Hiyo ya kuagiza mitalaa ni kwamba wanataka kuichakachua... kweli nakwambia, kwanini wanashindwa kuiwasilisha mapema?”.
“Hoja imetolewa, Waziri anatakiwa awasilishe mitalaa, hata hansard za kikao kilichopita aliahidi, lakini nashangaa, mimi nakwambia hakuna huo mtalaa na wanataka kuchakachua,” alisema.

No comments:

Post a Comment