Friday, February 1, 2013

Shahidi adai kina Ponda walivamia eneo

MLINZI wa Kampuni ya Agritanza Ltd, Julius Mlanzi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi kundi la watu waliojitambulisha kuwa Waislamu lilivyofika na kutaka warejeshewe eneo la Makazi lililopo Chang’ombe, wakidai ni mali yao.

Alidai mahakamani kuwa kundi hili lilimtaka mmiliki wa eneo hilo kuwasiliana na aliyemuuzia ili arejeshewe fedha alizotoa kwa madai wao wamefika kuchukua mali yao.
Alikuwa akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda kwa madai ya wizi na uchochezi.

Katika kesi hiyo, Ponda, Kiongozi wake, Shekhe Mukadam Abdallah Swalehe (45) na washtakiwa wengine 48 wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la uchochezi na wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6 milioni.

“Watu hao walidumu pale usiku na mchana hadi Oktoba 16, mwaka jana walipokamatwa na polisi,” alidai shahidi huyo. Shahidi wa sita wa upande wa mashtaka, Hamis Mkangama, akitoa ushahidi wake mahakamani hapo alidai kuwa Oktoba 7, mwaka huu akiwa katika eneo hilo la Chang’ombe Malkazi, Shekhe Ponda akiwa na mwenzake walikwenda katika eneo hilo na kupiga picha za eneo hilo.

Mkangama alidai kuwa kabla ya Sheikh huyo kuchukua picha za eneo hilo, aliwaambia nani aliwaruhusu kujenga katika eneo hilo, na kwamba wakamjibu kuwa aliwaambia wajenge ni bosi wao Suleiman.

Shahidi huyo alidai kuwa baada ya kumwambia hivyo, Sheikh Ponda aliwaambia wasimamishe ujenzi wa uzio na wao wakamweleza kuwa hawawezi kusimama hadi bosi wao aliyewaambia wajenge awaeleze hivyo.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi huo, Hakimu Nongwa aliiahirisha kesi hiyo hadi Februari 14, mwaka huu itakapotajwa na kwamba itaendelea kusikilizwa Februari 18, 25,27 na 28, mwaka huu.

Wakati kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea na ilipomalizika askari wa Jeshi la Polisi na Magereza waliimarisha ulinzi katika eneo lote la mahakama.
Ilipofika saa 5:08 asubuhi msafara wa kumpeleka Sheikh Ponda gerezani ulianza ambapo kulikuwapo na magari sita aina ya ‘Defender’ yaliyokuwa yamebeba askari waliovalia mavazi maalumu na silaha.

Pia lilikuwapo gari la maji ya kuwasha na basi moja la Magereza lililokuwa limembeba Ponda na wenzake.

Hata hivyo wakati msafara huo, ukitoka katika eneo la mahakama Waislamu waliokusanyika katika eneo hilo walijipanga na kuanza kusema huku wakimuaga Shekhe Ponda ‘Takbiir, Allahu Akbar’ ikiwa na maana ya Mungu ni mkubwa mara kadhaa naye alikuwa akiinua mikono yake juu iliyokuwa imefungwa pingu kama ishara ya kuwaunga mkono.

Wafuasi hao wakati wakiendelea na tukio hilo, wengine walikuwa wakisambaziana vikaratasi vilivyokuwa na ujumbe ulioandikwa kuwa Bismilahir Rahmaanir Rahiimi, Kongamano, Kongamano, Kongamano.

Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu pamoja na Shura ya Maimamu (T), Waislamu wote Jumapili ya Februari 3, mwaka huu kuanzia saa 4:00 mchana Waislamu wote wakutane katika Kiwanja cha Nuurul Yaqiin ( Uwanja wa Pamba) karibu na Uwanja wa Mwembe Yanga.

“Masheikh wetu wananyimwa hata haki ya dhamana, wanazidi kuteseka jela! Sababu ni kutetea mali za Waislamu zinazozidi kuuzwa na kuporwa! Tujumuike sote pamoja katika kuonyesha mshikamano wetu na tutoe uamuzi wa pamoja nini cha kufanya, Haki lazima itendeke kwa sote kama Jamii ya Watanzania. Mwislamu wa kweli hatakubali kudhulumu wala kudhulumiwa.”Kilidai kikaratasi hicho kilichokuwa kikisambazwa na kundi hilo la wafuasi wa Ponda.

No comments:

Post a Comment