Friday, February 15, 2013

HII NDO CHADEMA, TUMAINI LA WATANZANIA


MKAKATI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa kupeleka madaraka kwa wananchi kupitia kanda kumi za kichama zilizoundwa na Baraza Kuu hivi karibuni umeanza kazi rasmi kwa kila kanda kuweka mikakati yake.

Katika mgawanyo huu, Kanda ya Kaskazini ilipangwa kuwa na mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo Mkoa wa Arusha ulichaguliwa kuwa makao makuu ya Kanda ya Kaskazini.

Taarifa ya kanda hiyo kwa vyombo vya habari jana ilisema kuwa, Februari 16 na 17 mwaka huu, kutakuwa na kikao cha kwanza cha chama Kanda ya Kaskazini ambacho kitajumuisha wabunge wote kutoka mikoa ya kanda hiyo akiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe na viongozi wa chama wa mikoa.

Kwamba kikao hicho pia kitahudhuriwa na wenyeviti na mameya wa halmashauri zinazoongozwa na CHADEMA pamoja na wajumbe wa kamati kuu ya chama, wanaoishi kwenye Kanda ya Kaskazini pamoja na mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei.

Aidha, Februari 17 mwaka huu, kikao kitajumuisha viongozi kutoka majimbo yote ya Kanda ya Kaskazini takriban majimbo 30 na kuleta wajumbe zaidi ya 200 katika Jiji la Arusha.

Siku hiyo hiyo kutakuwa na uzinduzi wa kanda yenyewe na kuitambulisha timu ya uratibu, utakaohitimishwa na mkutano mkubwa wa hadhara.

Taarifa hiyo iliwaomba wananchi, wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya uzinduzi wa kanda yao na kuunga mkono mpango huu wa chama ambao mbali ya kukifanya kuwa karibu zaidi na wananchi pia katika kufanya shughuli za kisiasa kwa ufanisi wa hali ya juu.

No comments:

Post a Comment