CHAMA cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa masharti
mazito mawili kwa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kikimtaka Spika
wa Bunge, Anne Makinda, kuamua
ama aliache Bunge lijadili hoja muhimu kwa taifa au lisiwepo kabisa.
Msimamo huo umekuja zikiwa ni siku chache baada ya kuibuka mvutano
mkubwa bungeni kati ya wabunge wa upinzani na kiti cha Spika kutokana na
maamuzi yake kuegemea upande mmoja wa kuibeba serikali na kuzika hoja
za wapinzani.
Wakizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya
Temeke Mwisho, viongozi wakuu wa CHADEMA kwa nyakati tofauti waliwaeleza
wananchi kile kilichojiri bungeni na kuwataka kuwaunga mkono ili
kuondoa udhalimu.
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alisema kuanzia sasa
wabunge wao hawatatoka bungeni kama njia ya kupingana na ubabe wa kiti
cha Spika badala yake watahakikisha Bunge halifanyi kazi mpaka lijadili
hoja za msingi kwa maslahi ya Watanzania.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika mkutanoni baada ya
kuhitimishwa kwa maandamano ya kuwapokea wabunge wao yaliyoanzia eneo
la Ubungo River Side na msafara wake kupita maeneo mbalimbali hadi
Temeke, Mbowe alisema wamegundua janja ya CCM.
“Tumegundua janja yao. Walidhani watatuchakachua kila mara, tutatoka
Bungeni; sasa tumeamua. Wasipotusikiliza hatutoki hadi kieleweke,”
alisema.
Mbowe alisema wakati wa Watanzania kulalamika juu ya mustakabali wa
nchi yao umekwisha na kilichobaki ni kuchukua hatua dhidi ya serikali na
wao kama wabunge weameanza kwa kuwagomea kutoka nje hali iliyoifanya
serikali iombe kukaa nao mezani kwa ajili ya mjadala wa namna ya
kuendesha Bunge hilo kwa usawa.
Aliongeza kuwa ni wakati wa Watanzania kutoa kauli moja kama watu
waliokasirishwa na ugumu wa maisha bila kujali dini kabila wala sehemu
atokayo mtu.
“Ni ujinga kugombana kwa misingi ya udini, ukabila na ukanda badala ya
kushughulikia matatizo ya msingi ya nchi yetu leo watawala wanatugawa
kwa dini zetu makabila yetu na hata tutokako ili wapate kuendelea
kutunyonya katika rasilimali zetu sasa tuamke na mwaka 2015 uwe mwisho
wa msiba wa CCM,” alisema.
Dk. Slaa amuonya JK
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alikumbushia sababu za
kwa nini alimwambia Rais Kikwete kuwa akifanya mchezo nchi
haitotawalika.
Alisema miaka miwili iliyopita akiwa katika moja ya mikutano ya chama
wakiwa wanaomba dua, askari polisi waliwapiga mabomu na hata alipochukua
hatua ya kuwasiliana na Msajili wa Vyama vya Siasa hakuweza kupokea
simu yake.
Aliongeza kuwa leo baada ya miaka miwili dhuluma na uonevu ukiwa
umetamalaki wananchi wameamua kuchukua hatua za kuiwajibisha serikali
kupitia maandamano.
Kuhusu Bunge, Dk. Slaa alisema kinachofanyika sasa chini ya uongozi wa
Spika Makinda na Naibu wake Job Ndugai ni kutaka kuwadhoofisha wabunge
wa upinzani ili wasiweze kuzungumzia shida za wananchi.
Tundu Lissu atoboa siri
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alisema kuwa Makinda na
Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge chini ya Mwenyekiti wake,
Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi, walikuwa wameleta hukumu bungeni ya
kuwasimamisha ubunge wabunge wanne wa CHADEMA kwa miezi sita.
Lissu alisema kuwa waligundua wananchi wataandamana hivyo Spika alimwita na kumshauri Ngwilizi aache kusoma hukumu hiyo.
“Walikuwa wameleta hukumu kutushtaki eti Lissu, Pauline Gekul, Joshua
Nassari na John Mnyika tufungiwe kwa miezi sita lakini wakagundua
mitaani hapatakalika wakaamua kuahirisha kuisoma.
“Tutumie nguvu ya umma kulazimisha utaratibu wa kupata Katiba mpya.
Haki isipotendeka tuingie barabarani, tuikomboe nchi yetu kwa miguu yetu
na mikono yetu,” alisema Lissu.
Katika mkutano huo, Lissu pia amesema kuna njama za kuchakachua maoni
ya Katiba kutokana na idadi ya wabunge wa CCM, na muundo wa mabaraza
uliotangazwa wa sasa, ambao wajumbe watateuliwa na kupitishwa na vikao
vya maendeleo vya kata, ambavyo wenyeviti wengi ni wa CCM.
Msigwa amvaa Kinana
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, alimtuhumu Katibu
Mkuu wa CCM kuwa ni mmoja wa watuhumiwa kwa ujangili na kwamba serikali
haimchukulii hatua, hivyo kuwaasa Watanzania wamweke mbali na tembo.
Alisema afadhali apige kelele ili tembo wasichukuliwe, twiga
wasisafirishwe, apige kelele watu wapate maji, kuliko kukaa kimya
aonekane ana nidhamu twiga na tembo wauawe au wasafirishwe.
Zitto: Spika lazima ang’oke
Naibu katibu mkuu wa CHADEMA (bara) Zitto Kabwe, alisema wanaandaa
hoja binafsi ya kutokuwa na imani na Spika Makinnda na naibu wake Ndugai
huku akiwataka wananchi waanze kuwawajibisha viongozi hao kuanzia sasa
kwa kuwatumia ujumbe wa kulaumu namna wanavyoendesha Bunge kibabe.
Alisema Spika Mkinda hatumii akili zake alizojaaliwa na Mwenyezi Mungu
kufanya kazi bali anashikiliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Zitto alitoa namba za simu za viongozi hao kwa wananchi na kuwataka
waanze kuwatumia ujumbe wa maandishi au kumpigia kuonyesha kuwa
hawakubaliani na utendaji wao bungeni.
Mapema katika taarifa yake Zitto alipinga uamuzi wa Spika wa kuifuta
Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) kwa kuiunganisha na ile ya
Hesabu za Serikali, akidai hayo ni maamuzi ya hovyo.
Zitto alisisitiza kuwa ni lazima Spika adhibitiwe kwa kuondolewa
katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo vinginevyo nchi itaumia.
Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema kuwa maamuzi
haya yameleta sintofahamu kwa wananchi wengi na wafuatiliaji wa masuala
ya Bunge na uwajibikaji katika nchi yetu.
Mbunge huyo ambaye kamati yake ilikuwa mwiba kwa serikali katika
kuibua kashfa za ufisadi aliweka bayana kuwa maamuzi ya Spika ni kinyume
cha kanuni za Bunge, sheria ya ukaguzi na Katiba ya nchi.
“Maamuzi ya Spika yanavuruga Bunge, ni ya hovyo na yanapaswa kupingwa na kila mdau wa uwajibikaji nchini.
Baada ya Tanzania kuingia kwenye zoezi la ubinafsishaji, mashirika mengi ya umma yaliuzwa na mengine kufa kabisa,” alisema.
Aliongeza kwua Bunge lilikuwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma
na kamati hiyo ilifutwa mwaka 1997 kufuatia hatua za ubanafsishaji na
ukweli kwamba mashirika ya umma hayatakuwapo na hivyo hapakuwa na haja
ya kuwapo kwa kamati hiyo.
Zitto alisema kuwa mwaka 2007, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) alifanya mkutano wa uwajibikaji na kulieleza taifa kuwa
kimsingi mashirika ya umma bado yapo na mahesabu yake, kwa kuwa
hayaangaliwi, ni mabaya sana na fedha za umma zinapotea.
Alisema kuwa kwa hali hiyo, CAG aliomba Bunge liunde Kamati ya Bunge
ya Mashirika ya Umma ili liweze kupokea, kujadili na kutoa maelekezo
kuhusu mahesabu ya mashirika hayo na kusimamia ufanisi wake.
“Kamati ya POAC iliundwa rasmi mwaka 2008 mwezi Februari. Nilipewa dhamana ya kuwa mwenyekiti wa kwanza wa kamati hii.
“Sababu za kuanzishwa kwa POAC bado zipo na kimsingi sababu hizo ni za maana sana sasa kuliko ilivyokuwa kabla,” alisisitiza.
Alifafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano, POAC imekuwa
ikitekeleza majukumu yake kwa umahiri na kwa uwazi kuliko kamati
nyingine zote za Bunge.
“Taarifa ya mwisho ya POAC katika Bunge iliyowasilishwa katika mkutano
wa saba wa Bunge, mwezi Aprili mwaka 2012 ulipelekea kutolewa kwa hoja
ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ambayo ilisababisha mabadiliko
makubwa ya Baraza la Mawaziri,” alisema.
Zitto alisema kuwa wakati kamati inajiandaa na taarifa yake ya mwaka 2012 kwenye Mkutano wa Kumi na Moja, Spika ameivunja.
“Ikumbukwe maagizo ya mwisho ya Kamati ya POAC yalikuwa ni kuzuia
mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa mikopo kwa serikali bila ya kuwapo kwa
mikataba,” alisema.
Aliongeza kuwa hivi sasa serikali imekopa zaidi ya sh trilioni 1.2
kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya miradi mbalimbali, mikopo
hiyo ya fedha za wafanyakazi haina mikataba yoyote na POAC iliona
hatari ya fedha za wafanyakazi kupotea na kuleta madhara makubwa kwa
wastaafu nchini.
Zitto anaamini kuwa POAC ilipaswa kuongezewa nguvu zaidi ili kufikia
uwekezaji wa serikali kwenye makampuni binafsi badala ya kuifuta.
Uwekezaji wa serikali kwenye makampuni kama BP, Airtel, Kilombero Sugar,
SonGas hauna uangalizi wowote.
“Spika anasema kazi za POAC zitafanywa na Kamati ya PAC; Tanzania ina
jumla ya mashirika ya umma 258 yenye thamani ya sh trilioni 10.2 mpaka
Juni mwaka 2012, hata kamati ya POAC ilikuwa haiwezi kushughulikia
mashirika yote ya umma katika mwaka mmoja, PAC itawezaje kusimamia
wizara za serikali, mikoa na wakala wa serikali na wakati huohuo
mashirika ya umma 258?” alihoji.
Zitto alisema kuwa taifa linarudi miaka ya kabla ya 2008 ambapo mashirika ya umma yalikuwa kichaka cha kuiba fedha za umma.
Hivi karibuni POAC iligundua mtindo wa wizara za serikali kupeleka
fedha kwenye mashirika na kutumia kifisadi ili kukwepa ukaguzi kwenye
wizara; mfano ukiwa ni Wizara ya Utalii kupeleka zaidi ya sh milioni
600 Bodi ya Utalii mwaka 2010/2011.
Mnyika kumvaa Maghembe
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alitoa wiki mbili kwa Waziri wa Maji,
Prof. Jumanne Maghebe kuwa endapo hatachukua hatua kujibu hoja tisa
ambazo alikuwa aziwasilishe bungeni basi ataongoza maandamano ya
wananchi wa Dar es Salaam kwenda ofisini kwa waziri.
Mnyika alieleza kusikitishwa kwake kwa kuondolewa hoja yake, akisema
ni kwa kuwa Rais Jakaya Kiwete alidanganya kuwa 2013 tatizo la maji
katika jiji la Dar es Salaam litakuwa historia.
Aliongeza kuwa hoja yake iliondolewa kinyume cha utaratibu wa kanuni,
japo ilikuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Dar es Salaam.
Maandamano na mkutano huo yaliwashirikisha takriban wabunge zaidi ya
20 wa chama hicho, viongozi waandanizi wa kitaifa na maelfu ya wananchi
waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali na kuungwa mkoni kila
mahali ulipopita msafara huo.
Askofu amkaanga Makinda
Naye askofu wa kanisa moja kubwa nchini ambaye aliomba kuhifadhiwa
jina ili kuepusha malumbano, alisema kuwa Spika Makinda na Naibu wake,
Job Ndugai, wanayumba na wanaliyumbisha Bunge.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu, askofu huyo alisema kuwa viongozi
hao wawili wametumwa na wanatumika. Na kwamba wale waliowatuma wanaona
kuwa wanafanya vizuri kwani ndilo hasa lengo.
Alisema ni juhudi za wabunge pekee, tena wenye maono ya kizalendo, ndizo zinaweza kuwaondoa madarakani kwani ni vibaraka.
“Ukimlinganisha huyu Spika na wenzake waliowahi kuongoza Bunge, huyu
ni balaa. Amevaa itikadi zaidi. Lakini tunatafsiri kuwa anatumika na
Rais.
“Huwezi kuwa na Bunge imara kama una serikali dhaifu. Ndiyo maana
katika nchi yetu sasa, mtu hawezi kuwa Spika kama Rais hajamkubali,”
alisema.
Alisema hayo tunaweza kujifunza kutokana na kauli ya Makinda ya hivi
karibuni alipotoa maoni yake kwenye tume ya kukusanya maoni ya Katiba,
pale aliposema kwamba anapendekeza Spika asitokane na chama cha siasa.
Hiyo ina maana anashinikizwa na chama chake kufanya mengi ambayo kama
si shinikizo, asingeyafanya. Hata haya yanayotokea ni shinikizo la chama
chake.
“Hali ni hiyohiyo hata katika mahakama. Serikali inaingilia sana uhuru
wa mahakama. Ndiyo maana hata Jaji Mkuu alipotoa maoni yake katika Tume
ya Marekebisho ya Katiba alisema angependa mahakama iwe huru.
“Maana yake anajua kuwa kwa sasa kuna shinikizo kutoka serikalini au
chamani katika uendeshaji wa maamuzi ya mahakama nchini. Hii ni hatari,”
alisema.
Askofu alibainisha kuwa Makinda ni tofauti na Spika aliyepita Samuel
Sitta; kwamba Sitta alikuwa na mwelekeo, alisimamia ukweli, japo
mwelekeo wake haukupendwa na watawala.
Aliongeza kuwa Sitta alikuwa mpigania haki, mpenda mabadiliko na
aliweza kuonyesha kuwa anawajali wanyonge. Hakuliyumbisha Bunge na
aliweza kusimamia maamuzi.
“Bunge haliongozwi kitaasisi, bali linaongozwa kwa matashi ya mtu binafsi au kikundi cha watu.
“Sisi tunapaswa kuwa makini katika kuchagua watu wa aina hii na
tunapaswa kuwaelimisha Watanzania ili wapambane kuondoa mfumo wa aina
hii,” alisema.
chanzo-mtanzania daima