Friday, November 29, 2013

Wakala adai Simba ilimbania Juma Kaseja

Wakala wa Juma Kaseja amepeleka maelezo ya mchezaji huyo (CV) kwa TP Mazembe, lakini akaweka wazi kwamba Simba ndiyo walimharibia kipa huyo kusajiliwa na klabu za FC Lupopo na Motema Pembe.
Wakala huyo aitwaye Balanga Ismail sasa ni Kocha wa Sudan Kusini iliyopigwa mabao 2-1 na Zanzibar katika mechi ya awali ya kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Nyayo.
Balanga aliliambia gazeti hili mjini hapa kwamba, watu wa Simba ndiyo walimharibia kipa huyo wa Yanga kusajiliwa na klabu hizo za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Alisema kuwa; “Tulikuwa tumeshamalizana na watu wa Lupopo,  lakini kuna watu wa Simba walipiga simu kwa bosi wa Lupopo wakamwambia kwamba huyo Kaseja achaneni naye, huwa anauza mechi, yule bosi akakasirika sana akasema achana naye haraka sana.”
“Nikazungumza na Motema Pembe wakati tunaendelea kukubaliana mkataba ikatokea hali ileile ya Lupopo, sasa nikashindwa kuelewa hawa watu wa Simba kwa nini wanamchukia hivi huyu mchezaji? kwa nini wanamharibia maisha?” alisema Ismail.
“Sasa nimezungumza na watu wa Mazembe na nimewatumia CV ya Kaseja ndiyo nasikiliza kwenye usajili ujao wanaweza kumwita, kwa vile wameniambia wanajua uwezo wake,” alisema wakala huyo aliyesaini miaka miwili kuinoa Sudan Kusini.
Kaseja amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Yanga ambayo inashiriki Ligi ya Mabingwa mwakani. Kwa mujibu wa wakala huyo watu waliokuwa wakipiga simu hizo ni watu wa Simba ingawa hajapewa majina yao halisi.

No comments:

Post a Comment