Tuesday, November 12, 2013

CHADEMA wanapogombanishwa na mitandao ya kijamii


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinatarajiwa sana na Watanzania kuwa mfano bora wa kuigwa na vyama vingine nchini kwa kutoa uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganaizesheni thabiti kwa ajili ya maendeleo endelevu ya jamii nzima ya Watanzania.
Ni chama ambacho ni tumaini kubwa kwa Watanzania kuleta mabadiliko baada ya kile kinachoongoza kwa miaka mingi kuwa kimechokwa na wananchiLakini Watanzania wanashangaa kwa jinsi CHADEMA kinataka kuingia kwenye mtifuano kwa masuala yanayorushwa kwenye mitandao ya kijamii, ambayo hata mtu yeyote duniani anaweza kurusha mawazo yake, ambayo sio lazma yawapendeze wanaoyasoma.
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA anaandika barua kwa Katibu Mkuu ili aseme kama hayo ndiyo msimamo wa Chama au la, kwa jambo ambalo lipo kwenye mitandao.
Na wengine waliotajwa katika andiko kwenye mitandao wanakimbilia kuuliza kwenye chama uhalisia wa andiko hilo. Hivi Chama hiki makini chenye uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganaizesheni thabiti kinaweza kutoa tamko kwa kutumia mitandao? Mbona kila mara wanapokuwa na mambo huita waandishi? Watanzania wanahoji, mbona Katibu Mkuu wa chama hicho na yeye anashambuliwa kwenye mitandao hali kadhalika mwenyekiti wake naye huandikwa kwenye mitandao. Je, wao wamwandikie nani mambo yanayotajwa kwenye mitandao kuwahusu wao kuomba kama kweli huo ndio msimamo wa chama?
Sifa zilizotajwa na Kisumo zinapaswa kuongeza umakini wa CHADEMA sio kuleta vurugu ambazo Watanzania wanazishuhudia.
Nimeambiwa na Watanzania niwaambie CHADEMA kuwa mtasambaa kwa haraka sana kama Usalama wa Taifa ambao daima hawajapenda chama chenu kishinde watafanya kazi usiku na mchana kuwawekea mambo kwenye mitandao ya kijamii ili muendelee kugombana.
Na kwa kuwa wananchi husikiliza sana vyombo vya habari ambavyo mnavitumia, basi mtavurugwa sana. Sakata la andiko kwenye mitandao kuhusu mambo ya CHADEMA Watanzania wamelifananisha na lile la kudanganywa kuwa kuna mwanaume na mwanamke walikutwa wamelala pamoja ‘wakagandana’, yaani wakashindwa kuachana. Kimaumbile haiwezekani, kiuhalisia haiwezekani ila Watanzania walimiminika kuangalia, wakakikimbilia hospitalini, na baadaye wakajitokeza watu wakasema wanauza dawa za mambo hayo kusaidia watu ambao sio waaminifu kwenye ndoa.
Tukio hilo lilipita, hadi leo ukiuliza hata madaktari wakuambie kulikuwa na nini, zimebaki stori.
Suala la Babu wa Loliondo lilivuma, Watanzania wakatoa watu hospitalini wakafia njiani wakaegemea kwenye ndoto. Hili la CHADEMA mtaingizwa mkenge na vijana wa Usalama wa Taifa mkamatane wenyewe, mtaacha kuungana kusaidia chama. Nimeambiwa mkubali kukosoana, na kurekebishana. Waliokosea kweli wakubali makosa, acheni kuwashangaza Watanzania kwa masuala ambayo ndani ya chama mnaweza kuyajadili. Mitandaoni kuna nyoka wana miguu, punda wana pembe, nyoka mwenye matege, kuku mwenye mwanya ambao hata katika muziki, Masai alipoulizwa alisema hajawahi kuviona. Mpo tayari kujadili vitu vya kusadikika kuliko uhalisia? Kazi kwenu mimi ni mjumbe tu.
 Na Josephat Isango-Mwandishi wa makala hii Tanzania daima.
imehaririwa na http://themomentoftruthtz.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment