Friday, November 22, 2013

NAOMBA UCHUNGUZI WA KINA UFANYWE SIAMINI KAMA ZITTO KAFANYA HIVYO KWELI


Taarifa ya chama
Akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu jana Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema, Zitto, Dk Mkumbo na Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba walikuwa na mtandao wa kukiua  chama hicho, huku wakitengeneza tuhuma za kuwachafua  Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu wake, Dk Willbroad Slaa.
Alisema kuwa kamati kuu ilibaini kuwapo kwa mkakati mkubwa wa watu hao kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’, ambao umeandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’.
“Kikundi hicho vinara wake wapo wanne, Zitto anajulikana kama Mhusika Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na mtu mwingine wa nne hatujamtambua kwa sasa yeye anatumia jina la M2” alisema Lissu.
Alisema wakati wa kuhojiwa na Kamati Kuu Dk Mkumbo alikiri kuwa mhusika mkuu wa mtandao huo ni Zitto, lakini Zitto alikana kuutambua waraka huo licha ya kueleza unamhusu kwa kuwa umetaja jina lake, kauli ambayo alidai Kamati Kuu haikutaka kuiamini.
Huku akieleza jinsi watu hao walivyokuwa wakiwasiliana na kupanga mikakati ya kuimaliza Chadema kwa siri chini ya ufadhili wa fedha kutoka kwa Zitto, Lissu alisema Naibu Katibu Mkuu huyo wa zamani alikuwa akitumiwa na Chama Tawala (CCM) kuimaliza Chadema.
“Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango haramu na ambao unaichanachana katiba ya chama chetu. Ni mkakati wa vita dhidi ya chama chetu na utaratibu wetu wa kikatiba. Hatuwezi kunyamazia mkakati huu wa kutumaliza, uvumilivu umefika kikomo,” alisema.
Uamuzi
Alisema kutokana na hali hiyo kamati kuu iliamuru wahusika wote wavuliwe nyadhifa zao zote za uongozi wa chama, kukubaliana kuunda timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa sekretarieti ya makao makuu ya chama hicho ili kumtambua mtu wa nne (M2).
“Kamati ya Bunge imetakiwa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha Zitto anavuliwa nafasi zote za Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pia wote wanatakiwa kujieleza ndani  ya siku 14 kwa nini wasivuliwe uanachama na watapewa fursa ya kujitetea,” alisema.

Alisema Kamati Kuu itakutana kwa dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatima ya watuhumiwa hao.
Kauli ya Mbowe
Awali Mbowe alipinga madai kuwa Zitto ameondolewa kwa kuwa alikuwa akitaka kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, akasisitiza kuwa uamuzi huo umefanyika kwa kuwa Chadema ni chama cha watu, siyo mali ya mtu binafsi.

No comments:

Post a Comment