Sunday, November 3, 2013

January Makamba: Natafakari urais 2015

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema kuwa anatafakari iwapo awanie urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kutokana na kuwapo kwa watu wengi hasa ndani ya CCM, wanaomtaka kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Makamba ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM alisema: “Kwanza ni kweli kwamba kuna ushawishi kuhusu suala hilo kutoka kwa vijana walioko nje na ndani ya chama, wanataaluma, baadhi ya wazee na watu wengine iwe kwa makundi au mtu mmoja mmoja wamekuwa wakinishawishi kugombea kwa muda sasa.”
Aliongeza: “Mwanzoni sikuona uzito sana, yaani sikuzingatia sana, lakini kwa kadiri siku zinavyokwenda ni kwamba ushawishi umekuwa mkubwa na hivyo niseme ni jambo ambalo sasa ninalitafakari kwa kina”.
Alisema ikiwa ataamua kuwania urais, atafanya hivyo wakati mwafaka kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na chama hicho, lakini akasema kwa sasa si wakati wake. Makamba alikuwa akijibu hoja za gazeti hili lililotaka ufafanuzi wake kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba ameanza harakati za kuusaka urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Gazeti hili lilidokezwa kuwa hatua yake hiyo imemwingiza katika mvutano usio rasmi na wanasiasa ambao tayari wameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini, wakiwamo wale wa kambi ya urais aliyokuwa akidaiwa kuwa mmoja wao.
Awali iliaminika kuwa Makamba alikuwa katika kambi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini wachambuzi wa masuala ya kisisa wanasema ‘katika siku za karibuni mwenendo wake unaashiria kwamba si mmoja wa wanaomuunga mkono kiongozi huyo, bali ni mtu mwenye mipango yake binafsi ya kisiasa”.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema mwenendo wa Makamba umewakasirisha baadhi ya wanasiasa hususan wanaomuunga mkono Lowassa ambao mara kadhaa wamesikika hadharani wakimlalamikia kwamba ni msaliti.
Hata hivyo, Makamba katika maelezo yake anasema hajawahi kuwa katika kundi lolote la kumuunga mkono mtu yeyote kwani yeye haamini katika makundi. “Ninaamini katika kundi moja, nalo ni CCM,” alisema.
Aliongeza: “Kwa hiyo mtu yoyote akinikasirikia kwa sababu zozote zile za kisiasa nitamshangaa maana sijawahi mahali popote na kwa namna yoyote kujitanabaisha kwamba mimi nipo kwenye kundi fulani, au kundi la mtu yeyote.”
Sababu za mashaka
Miongoni mwa nyedo zinazotiliwa shaka za mwanasiasa huyo ni hatua yake ya kushiriki katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) uliofanyika Zanzibar ambako pamoja na mambo mengine aligawa simu zaidi ya 100 aina ya Samsung Galaxy kwa wajumbe wa mkutano huo.
Imethibitika kwamba mpango huo ulikuwa ni wake binafsi na haukuwashirikisha waliokuwa wakiamini kwamba wako naye katika harakati za kumuunga mkono Lowassa.

No comments:

Post a Comment