Thursday, November 7, 2013

Ujumbe wa Rais kwa wananchi leo

Dodoma na Dar.Rais Jakaya Kikwete, leo jioni atalihutubia taifa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akitarajiwa kuzungumzia mambo makubwa manne.
Spika wa Bunge, Anne Makinda aliwaambia wabunge jana asubuhi kuwa Rais Kikwete atalihutubia Bunge kuanzia saa 10.00 jioni na kwamba atafanya hivyo kwa mujibu wa Kanuni ya 30 (1) ambayo inasema: “Rais anaweza kulihutubia Bunge siku yoyote ambayo Bunge linakutana na wakati mwingine wowote kwa mujibu wa Ibara ya 91 ya Katiba.”
Hotuba ya Rais Kikwete inatarajiwa kutoa majibu kwa masuala kadhaa kuhusu msimamo na mwelekeo wa taifa yakiwamo mchakato wa Katiba Mpya, hususan marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013 ambayo ilipitishwa mkutano uliopita.
Kamati ya Uongozi ya Bunge iliyokutana jana mchana chini ya Spika Makinda, iliridhia muswada huo kuingizwa katika ratiba ya sasa kutokana na kuwasilishwa chini ya hati ya dharura iliyosainiwa na Rais Kikwete, Oktoba 28 mwaka huu.
Kanuni ya 80 (4) ya Kanuni za Bunge inasema: “Muswada wowote wa Sheria wa Serikali wa dharura hautaingizwa kwenye shughuli za Bunge bila ya kuwa na hati iliyowekwa saini na Rais inayoeleza kuwa muswada uliotajwa katika hati hiyo ni wa dharura.”
Katika fasili ya 5 na 6 ya Kanuni, Kamati ya Uongozi ndiyo yenye dhamana ya kuidhinisha muswada wa dharura na sasa mapendekezo ya Serikali yatapita katika hatua zote tatu za kusomwa, kujadiliwa kisha kupitishwa kuwa sheria.
Matarajio ya wasomi
Mbali na mchakato wa Katiba Mpya, baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliohojiwa jana walisema kwamba Rais Kikwete hawezi kukwepa kuzungumzia mgogoro unaofukuta ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Wengine wamesema huenda akazungumzia mambo muhimu kama Operesheni Tokomeza Majangili ambayo siku chache zilizopita ilizua tafrani bungeni kiasi cha kuanzishwa uchunguzi wa jinsi ilivyoendeshwa, Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na ushiriki wa Tanzania katika vita ya kuwaondoa Waasisi wa Kundi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Gaudence Mpangala alisema kwamba Rais Kikwete anaweza kuzungumzia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mgogoro wa EAC hususan kutengwa kwa Tanzania na nchi za Uganda, Kenya na Rwanda.
“Hii Sheria ya Mabadiliko ya Katiba bado ina utata hata kama Rais aliisaini. Tunakumbuka muswada ulipopelekwa bungeni ni wabunge wachache tu wa upinzani walioijadili, lakini wengi walitoka nje na ilizua vurugu kwa vyama vya siasa na asasi za kiraia.”
Aliongeza, “Inawezekana CCM wakagoma kuijadili wakasema tulishapitisha na kama Rais akiwalazimisha, Bunge linaweza kuvunjika na kuitishwa tena uchaguzi. Ndiyo maana Rais analazimika kuhutubia Bunge ili kuweka mambo sawa.”

No comments:

Post a Comment